Ufunuo 4

Mungu mwenye nguvu zote huangukiwa.

1Kisha nalitazama, nikaona mlango mbinguni uliokuwa wazi. Ndipo, sauti ile ya kwanza, niliyoisikia kama ya baragumu, iliyosema nami, iliposema: Panda huku, nikuonyeshe yatakayofanyika, haya yakiisha! Papo hapo nikawapo kiroho.[#Ufu. 1:10.]

2Nikaona kiti cha kifalme, kilikuwa kimewekwa mbinguni; humo kitini mlikuwamo mwenye kukikalia.[#Ufu. 1:10; Yes. 6:1; Ez. 1:26; 10:1.]

3Huyu aliyekaa, ukimtazama, alifanana na kijiwe cha yaspi na cha sardio; hata upindi wa Mungu ulikizunguka kiti, kwa kuutazama, ulifanana na kijiwe cha sumaradi.[#Ez. 1:26-28.]

4Tena viti 24 vya kifalme vilikizunguka kiti kile; nikaona wazee 24 waliokaa mle vitini, waliokuwa wamevaa nguo nyeupe na vilemba vya dhahabu vichwani pao.[#Ufu. 3:4; 5:10; Yes. 24:23.]

5Hapo penye kiti cha kifalme palipiga umeme na vivumo na ngurumo, tena palikuwa na mienge saba ya moto iliyowaka mbele ya kiti cha kifalme, ndio zile roho saba za Mungu.[#Ufu. 1:4; 8:5; 11:19; 16:18; Zak. 4:2.]

6Tena mbele ya kiti cha kifalme kulikuwako yenye mfano wa bahari ya kioo iliyofanana na ulanga uangazikao. Napo katikati penye kiti cha kifalme na kukizunguka kiti cha kifalme palikuwa na nyama wanne waliojaa macho mbele na nyuma.[#Ez. 1:5,22.]

7Nyama wa kwanza alifanana na simba, nyama wa pili alifanana na dume la ng'ombe, nyama wa tatu alikuwa na uso kama wa kimtu, nyama wa nne alifanana na tai mwenye kuruka.[#Ez. 1:10; 10:14.]

8Kila mmoja wao hao nyama wanne alikuwa na mabawa sita yaliyojaa macho po pote, nje ndani; hawapumziki mchana wala usiku wakisema:

Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Bwana Mungu,

yeye Mwenyezi aliyekuwapo, aliopo, atakayekuja.

9Hao nyama walipomtukuza na kumheshimu na kumshukuru yule aliyekaa kitini mwa kifalme, aliye mwenye kuwapo kale na kale pasipo mwisho,

10ndipo, wale wazee 24 walipomwangukia yule aliyekaa kitini mwa kifalme na kumtambikia yeye aliye mwenye kuwapo kale na kale pasipo mwisho; wakavitupa vilemba vyao mbele ya kiti cha kifalme wakisema:[#Ufu. 5:14.]

11Wewe Bwana na Mungu wetu, umepaswa na kupewa utukufu

na heshima na uwezo, kwani wewe uliviumba vyote;

kwa hayo, uyatakayo, vikapata kuwapo vilipokwisha

kuumbwa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania