Kumbukumbu la Torati 23

Waliokatazwa mkutanoni

1Aliyejeruhika konde, au aliyekatika tupu yake, asiingie mtu huyo katika mkutano wa BWANA.

2Mwana wa haramu asiingie katika mkutano wa BWANA; hata kizazi cha kumi asiingie aliye wake katika mkutano wa BWANA.

3Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa BWANA; wala hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa BWANA milele;[#Neh 13:1-2; 4:3-7; Rut 4:5]

4kwa sababu hapo mlipotoka Misri hawakuwalaki na chakula wala maji njiani; na kwa kuwa walimwajiri juu yako Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia, aje akuapize.[#Hes 22:1-6; Mwa 14:18; Kum 2:29; 1 Sam 25:11; 1 Fal 18:4; Isa 63:9; Mt 10:40,42; 25:41-46; Yos 24:9]

5Lakini BWANA, Mungu wako, hakukubali kumsikiza huyo Balaamu; BWANA, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile alivyokupenda BWANA, Mungu wako.[#Hes 23:7—24:9; Mit 26:2]

6Usitafute amani yao wala heri yao siku zako zote, milele.[#Ezr 9:12]

7Usimchukie Mwedomi; kwa kuwa ni ndugu yako; usimchukie Mmisri, kwa kuwa ulikuwa mgeni katika nchi yake.[#Mwa 25:24-26; Oba 1:12; Kut 22:21; 23:9; Kum 10:19; Law 19:34]

8Wana wao watakaozaliwa kizazi cha tatu na waingie katika mkutano wa BWANA.

Maagizo kuhusu usafi, ibada na utu

9Utakapotoka kwenda juu ya adui zako nawe u katika kambi, jilinde na kila neno baya.

10Akiwa kwenu mtu awaye yote asiyekuwa ni tohara kwa ajili ya yaliyomtukia usiku, na atoke nje ya kituo, wala asiingie ndani ya kituo;[#Law 15:16; Hes 5:2,3; 1 Kor 5:11,13]

11lakini na iwe ikaribiapo jioni, yeye ataoga maji; na jua likiisha kuchwa ataingia ndani ya kituo.

12Tena uwe na mahali nje ya kituo, kwa kutokea nje;

13nawe uwe na jembe dogo katika silaha zako; napo uotamapo nje uchimbe kwa lile jembe, na kugeuka na kukifunika kikutokacho;

14kwa kuwa BWANA. Mungu wako, yuatembea katika kituo akuokoe, na kukutolea adui zako mbele yako; kwa hiyo na kiwe kitakatifu kituo chako; asije akaona kitu kwako kisichokuwa safi, akageuka na kukuacha.[#Mwa 15:1; Law 26:12; Yer 32:40; 2 Kor 6:16; Kut 3:5]

15Usimrudishe kwa bwana wake mtumwa aliyejiponya kutoka kwa bwana wake kuja kwako;[#1 Sam 30:15]

16na akae nawe, katikati yako, ndani ya malango yako mojawapo, mahali atakapochagua palipo pema machoni pake; usimwonee.[#Kut 22:21; 23:9; Mit 22:22; Yer 7:6; Zek 7:10; Mal 3:5; Yak 2:6]

17Pasiwe na kahaba katika binti za Israeli, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israeli wanaume.[#Law 19:29; Mit 2:16; Mwa 19:5; 2 Fal 23:7]

18Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya BWANA, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yoyote; kwani haya ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako, yote mawili.

19Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu chochote kikopeshwacho kwa riba;[#Kut 22:25; Law 25:36-37; Kum 15:7-11; Neh 5:2,7; Zab 15:5; Lk 6:34]

20mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili BWANA, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki.[#Law 19:34; Kum 15:10]

21Utakapoweka nadhiri kwa BWANA, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.[#Hes 30:1-16; Mt 5:33; Ayu 22:27; Zab 61:8; Mhu 5:4,5]

22Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakuwa dhambi kwako.

23Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri BWANA, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako.[#Zab 66:13]

24Uingiapo katika shamba la mizabibu la jirani yako, utaweza kula zabibu za kukushibisha, kama upendavyo; ila usitie katika chombo chako.[#Mt 12:1; Lk 12:15; 1 Kor 6:10; Kol 3:5]

25Uingiapo katika mmea wa jirani yako waweza kuyapurura masuke kwa mkono wako; ila usisongeze mundu katika mmea wa jirani yako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya