2 Nya 12

Wamisri Waishambulia Yuda

1Ikawa ulipothibitika ufalme wa Rehoboamu, naye amepata nguvu, aliiacha torati ya BWANA, na Israeli wote pamoja naye.[#2 Nya 11:17; Kum 8:14; 1 Fal 14:22-24]

2Ikawa katika mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu; kwa kuwa walikuwa wamemwasi BWANA;[#1 Fal 14:24,25]

3mwenye magari elfu moja na mia mbili, na wapanda farasi sitini elfu; na watu wasiohesabika, waliotoka Misri pamoja naye; Walubi, na Wasukii, na Wakushi.[#2 Nya 16:8]

4Akaitwaa miji yenye maboma iliyokuwa ya Yuda, akaja Yerusalemu.

5Ndipo akaja Shemaya nabii kwa Rehoboamu, na kwa wakuu wa Yuda, waliokusanyika Yerusalemu kwa sababu ya Shishaki, akawaambia, BWANA asema hivi, Ninyi mmeniacha mimi, kwa hiyo nami nimewaacha ninyi mkononi mwa Shishaki.[#2 Nya 11:2; Kum 28:25; 2 Nya 15:2]

6Ndipo wakajinyenyekeza wakuu wa Israeli na mfalme; wakasema, BWANA ndiye mwenye haki.[#Kut 10:3; Law 26:40-42; 2 Nya 33:12,19; 34:27; Zab 78:34; Yak 4:10; Kut 9:27]

7Naye BWANA alipoona ya kwamba wamejinyenyekeza, neno la BWANA likamjia Shemaya, kusema, Wamejinyenyekeza; sitawaharibu; lakini nitawapa wokovu punde, wala ghadhabu yangu haitamwagika juu ya Yerusalemu kwa mkono wa Shishaki.[#1 Fal 21:28,29]

8Walakini watamtumikia; ili wapate kujua utumwa wangu, na huo utumwa wa falme za nchi.[#Isa 26:13; Kum 28:47,48]

9Basi Shishaki, mfalme wa Misri, akapanda juu ya Yerusalemu, akazichukua hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao za dhahabu alizozifanya Sulemani.[#1 Fal 14:25,26; 10:16,17; 2 Nya 9:15,16]

10Mfalme Rehoboamu akafanya ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme.[#2 Sam 8:18; 23:23; 1 Nya 11:25]

11Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa BWANA, wakaja walinzi wakazichukua, wakazirudisha tena chumbani mwa walinzi.

12Naye alipojinyenyekeza, ghadhabu ya BWANA ikamgeukia mbali, asimharibu kabisa; tena yalionekana katika Yuda mambo mema.[#Mwa 18:24; 1 Fal 14:13; 2 Nya 19:3]

13Basi mfalme Rehoboamu akajitia nguvu katika Yerusalemu, akatawala; maana Rehoboamu alikuwa na umri wa miaka arobaini na mmoja alipoanza kutawala, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua BWANA miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke huko jina lake. Na jina la mamaye aliitwa Naama Mwamoni.[#1 Fal 14:21; 2 Nya 13:7; 2 Nya 6:6; Zab 48:1-3]

14Naye akatenda yaliyo maovu, kwa kuwa hakuukaza moyo wake amtafute BWANA.[#Mt 7:7; Mdo 9:11]

15Basi mambo yake Rehoboamu, ya kwanza na ya mwisho, je! Hayakuandikwa katika tarehe za Shemaya nabii na Ido mwonaji, kwa jinsi ya kuandika nasaba? Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote.[#2 Nya 9:29; 13:22]

16Rehoboamu akalala na babaze, akazikwa katika mji wa Daudi. Na Abiya mwanawe alitawala mahali pake.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania