Amo 1

1Maneno ya Amosi, aliyekuwa mmoja wa wachungaji wa Tekoa; maono aliyoyaona katika habari za Israeli, siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la nchi.[#2 Sam 14:2; 2 Fal 15:1-7; 2 Nya 26:1-23; 11:6; Zab 78:70; Hos 1:1; Zek 14:5; 2 Fal 14:23-29]

Hukumu kwa Jirani za Israeli

2Naye alisema,[#Yoe 3:16]

BWANA atanguruma toka Sayuni,

Atatoa sauti yake toka Yerusalemu;

Na malisho ya wachungaji yataomboleza,

Na kilele cha Karmeli kitanyauka.

3Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Dameski, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameipura Gileadi kwa vyombo vya kupuria vya chuma;[#Isa 8:4; 2 Fal 10:33; 17:1-3; Yer 49:23-27; Zek 9:1]

4lakini nitapeleka moto uingie katika nyumba ya Hazaeli, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi.

5Nami nitalivunja komeo la Dameski, na kuwakatilia mbali wenyeji wa bondeni mwa Aveni, na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Beth-Adini; na watu wa Shamu watakwenda hali ya kufungwa hata Kiri, asema BWANA.[#Isa 7:1]

6Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Gaza, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu waliichukua katika hali ya kufungwa kabila nzima, wawatie katika mikono ya Edomu;[#2 Nya 28:18; Isa 14:29-31; Yer 47:1-7; Eze 25:15-17; Yoe 3:4-8; Sef 2:4-7; Zek 9:5-7]

7lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Gaza, nao utayateketeza majumba yake.[#2 Fal 18:8]

8Nami nitamkatilia mbali mwenyeji katika Ashdodi; na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Ashkeloni; nami nitaugeuza mkono wangu uwe juu ya Ekroni; na mabaki ya Wafilisti wataangamia, asema Bwana MUNGU.

9Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Tiro, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameitia kabila nzima katika mikono ya Edomu, wala hawakulikumbuka agano la udugu;[#Isa 23:1-18; Eze 26:1—28:19; Yoe 3:4-8; Zek 9:1-4; Mt 11:21-22; Lk 10:13-14]

10lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Tiro, nao utayateketeza majumba yake.

11Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Edomu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, akatupilia mbali huruma zake zote; hasira yake ikararua-rarua daima, akaishika ghadhabu yake milele;[#2 Nya 28:17; Isa 34:5-17; 63:1-6; Yer 49:7-22; Eze 25:12-14; 35:1-15; Oba 1-14; Mal 1:2-5]

12lakini nitapeleka moto juu ya Temani, nao utayateketeza majumba ya Bosra.

13Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya wana wa Amoni, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewapasua wanawake wa Gileadi wenye mimba, ili wapate kuongeza mipaka yao;[#Yer 49:1-6; Eze 21:28-32; 25:1-7; Sef 2:8-11]

14lakini nitawasha moto katika ukuta wa Raba, nao utayateketeza majumba yake; pamoja na kupiga kelele siku ya vita, pamoja na tufani katika siku ya chamchela;[#Kum 3:11; Eze 25:5]

15na mfalme wao atakwenda utumwani, yeye na wakuu wake wote pamoja, asema BWANA.[#Yer 49:3]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania