Kum 4

Musa Awaamuru wawe Watiifu

1Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wa baba zenu.[#Eze 20:11; Rum 10:5]

2Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za BWANA, Mungu wenu, niwaamuruzo.[#Ufu 22:18-19; Kum 12:32; Yos 1:7; Mit 30:6; Mt 15:9]

3Macho yenu yameona aliyoyatenda BWANA kwa sababu ya Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, BWANA, Mungu wako, amewaangamiza kutoka kati yako.[#Hes 25:1-9]

4Bali ninyi mlioambatana na BWANA, Mungu wenu, mnaishi kila mmoja wenu, hata leo.

5Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama BWANA, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki.

6Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili.[#Ayu 28:28; Zab 19:7; 111:10; Mit 1:7; 2 Tim 3:15; 1 Fal 10:6,9; Dan 1:20; 4:9; Mal 3:12; Mdo 4:13]

7Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo?[#2 Sam 7:23; Kut 25:8; 29:45; Law 26:12; 1 Fal 6:13; Zab 46:1; 145:18; Isa 55:6; Zek 2:10; Efe 2:17; Yak 4:8]

8Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.

9Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako;[#Mit 4:23; 23:19; 3:1,3; 4:21; Mwa 18:19; Kum 6:7; 11:19; Zab 78:5,6; Mit 22:6; Efe 6:4]

10siku ile uliyosimama mbele za BWANA wako huko Horebu, BWANA aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na kuwafundisha watoto wao.[#Kut 19:9,16; 20:18; Ebr 12:18]

11Mkakaribia, mkasimama chini ya ule mlima; mlima ukawaka moto mpaka kati ya mbinguni, kwa giza na mawingu, na giza kuu.[#Kut 19:16-18; Ebr 12:18-19]

12BWANA akasema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lo lote; sauti tu.[#Kut 20:22; 1 Fal 19:12]

13Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe.[#Kut 31:18; 34:28; Kum 9:10]

14BWANA akaniamuru wakati ule niwafundishe maagizo na hukumu, mpate kuzitenda katika nchi ile mtakayoivukia ili kuimiliki.[#Kut 21:1]

15Jihadharini nafsi zenu basi; maana hamkuona umbo la namna yo yote siku ile BWANA aliyosema nanyi kutoka kati ya moto;[#Yos 23:11; Mit 4:23,27; Yer 17:21; Mal 2:15; Isa 40:18; Mdo 17:24-29]

16msije mkajiharibu nafsi zenu, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa sura yo yote, mfano wa mwanamume au mwanamke,[#Kut 20:4; Law 26:1; Kum 5:8; 27:15; Rum 1:23]

17mfano wa mnyama ye yote aliye duniani, au mfano wa ndege ye yote arukaye mbinguni,[#Rum 1:23]

18au mfano wa kitu cho chote kitambaacho juu ya ardhi, au mfano wa samaki ye yote aliye majini chini ya nchi;

19tena usije ukainua macho yako hata mbinguni, na ulionapo jua, na mwezi, na nyota, jeshi la mbinguni lote pia, ukashawishwa na kuviabudu, na kuvitumikia, ambavyo BWANA, Mungu wako amewagawanyia watu wote chini ya mbingu zote.[#Kum 17:3; Ayu 31:26; Yer 8:2; Mwa 2:1; 2 Fal 17:16; 21:3]

20Bali BWANA amewatwaa ninyi, na kuwatoa katika tanuu ya chuma, katika Misri, mpate kuwa watu wa urithi kwake, kama mlivyo leo hivi.[#Kut 19:5; Kum 7:6; 14:2; 26:18; Tit 2:14; 1 Pet 2:9]

21Tena BWANA alinikasirikia kwa ajili yenu, akaapa ya kwamba sitavuka Yordani, na ya kwamba sitaingia nchi ile njema, awapayo BWANA, Mungu wenu, iwe urithi.[#Hes 20:12]

22Lakini mimi nitakufa katika nchi hii, sina ruhusa kuvuka Yordani; bali ninyi mtavuka, na kuimiliki nchi ile njema.[#2 Pet 1:13]

23Jihadharini nafsi zenu, msije mkalisahau agano la BWANA, Mungu wenu, alilolifanya nanyi, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa umbo la kitu cho chote ulichokatazwa na BWANA, Mungu wenu,

24kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.[#Ebr 12:29; Kut 24:17; Kum 9:3; Isa 33:14; Kut 20:5; Kum 6:15; Isa 42:8; 48:11]

25Utakapozaa wana, na wana wa wana, mkisha kuwa katika nchi siku nyingi, mkajiharibu na kufanya sanamu ya kuchonga kwa umbo la kitu cho chote, mkafanya ambayo ni maovu machoni pa BWANA, Mungu wako, na kumtia hasira;[#2 Fal 17:17]

26nawashuhudizia mbingu na nchi hivi leo, kwamba karibu mtaangamia kabisa juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki, hamtafanya siku zenu ziwe nyingi juu yake, ila mtaangamizwa kabisa.[#Kum 30:18,19; Isa 1:2; Mik 6:2]

27Na BWANA atawatawanya kati ya mataifa, nanyi mtasalia watu kidogo hesabu yenu kati ya makabila, mtakakopelekwa mbali na BWANA.[#Kum 28:36; Law 26:33; Kum 28:62,64; Neh 1:8; Eze 12:15; 32:26]

28Na huko mtatumikia miungu, kazi za mikono ya watu, miti na mawe, ambao hawaoni, wala hawasikii, hawali, wala hawanusi.[#Kum 28:36,64; Yer 16:13; Eze 20:32,39; Mdo 7:42]

29Lakini huko, kama mkimtafuta BWANA, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote.[#Yer 29:13; 2 Nya 15:4; Neh 1:9; Isa 55:6]

30Na wakati uwapo katika mashaka, ukiisha kupatwa na mambo haya yote, siku za mwisho, utamrudia BWANA, Mungu wako, na kuisikiza sauti yake;[#Mwa 49:1; Kum 31:20; Yer 23:20; Hos 3:5; Yer 4:1,2; Yoe 2:12]

31kwa kuwa BWANA, Mungu wako, ni Mungu wa rehema; hatakukosa wala kukuangamiza, wala hatalisahau agano la baba zako alilowaapia.[#Kut 34:6; Hes 14:18; 2 Nya 30:9; Neh 9:31; Ayu 8:8; Zab 86:5,15; 103:8; 111:4; Yon 4:2]

32Maana uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya mbingu hata pembe hii, kwamba kumetukia neno lo lote kama neno hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili?[#Ayu 8:8; Kut 15:11; 1 Sam 2:2; 2 Sam 22:31,32; Isa 44:6,8; 45:5,18; Mt 24:31; Mk 12:29]

33Je! Watu wakati wo wote wameisikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife?

34Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara, na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu, kama vile BWANA, Mungu wenu, alivyowatendea ninyi katika Misri, mbele ya macho yenu?

35Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa BWANA ndiye Mungu, hapana mwingine ila yeye.[#Mk 12:29,32; Kum 32:39; 1 Sam 2:2; 2 Sam 22:32; Isa 45:5,18]

36Kutoka mbinguni amekusikizisha sauti yake, ili akufundishe; na juu ya nchi alikuonyesha moto wake mkuu; ukasikia maneno yake toka kati ya moto.[#Kut 19:9,19; 20:18,22; 24:16; 1 Nya 29:11; 2 Nya 20:6; Ebr 12:18]

37Na kwa sababu aliwapenda baba zenu, kwa sababu hiyo aliwachagua wazao wao baada yao, akakutoa katika Misri kwa kuwako pamoja nawe, kwa uweza wake mwingi,

38ili kufukuza mbele yako mataifa, walio wakubwa, wenye nguvu kukupita wewe, ili kukuingiza, na kukupa nchi yao iwe urithi, kama ilivyo leo.

39Kwa hiyo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa BWANA ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine.[#Yos 2:11; Isa 42:8; Dan 4:35]

40Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo BWANA, Mungu wako, milele.[#Law 22:31; Kum 5:16; 6:3,18; 12:25,28; 22:7; Efe 6:3]

Miji ya Ukimbizi Mashariki mwa Yordani

41Ndipo Musa akabagua miji mitatu ng’ambo ya Yordani upande wa matokeo ya jua;[#Yos 20:8-9; Hes 35:6]

42ili kwamba amwuaye mtu apate kukimbilia huko, amwuaye jirani yake pasipo kujua, wala hakumchukia tangu hapo; ili apate kuishi akimbiliapo mmojawapo miji hiyo;

43nayo ni hii, Beseri ya barani iliyo katika nchi tambarare, kwa Wareubeni; na Ramothi iliyo Gileadi, kwa Wagadi; na Golani iliyo Bashani, kwa Wamanase.

Utangulizi wa Sheria ya Mungu

44Na torati Musa aliyowawekea wana wa Israeli ni hii;

45haya ndiyo mashuhudizo, na amri, na hukumu, Musa alizowaambia wana wa Israeli walipotoka Misri;

46ng’ambo ya Yordani, katika bonde lililoelekea Beth-peori, katika nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni ndiye aliyepigwa na Musa na wana wa Israeli, walipotoka Misri;[#Kum 3:29]

47wakaishika nchi yake, ikawa milki yao, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, ndio wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa ng’ambo ya Yordani upande wa matokeo ya jua;[#Hes 21:35; Kum 3:3,4]

48toka Aroeri, iliyo juu ya ukingoni pa bonde la Arnoni, hata mpaka mlima wa Sioni (nao ndio Hermoni),[#Kum 2:36; 3:12; Zab 133:3]

49na Araba yote iliyo ng’ambo ya Yordani upande wa mashariki, hata mpaka bahari ya Araba, chini ya matelemko ya Pisga.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania