Mwa 50

1Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilila, akambusu.[#Mwa 46:4; 2 Fal 13:14]

2Yusufu akawaagiza watumishi wake waganga, kwamba wampake baba yake dawa asioze. Waganga wakampaka dawa Israeli.[#2 Nya 16:14; Mt 26:12; Mk 14:8; 16:1; Lk 24:1; Yn 19:39,40]

3Siku zake arobaini zikaisha, maana hivyo hutimizwa siku za kupaka dawa. Wamisri wakamlilia siku sabini.[#Hes 20:29; Kum 34:8]

4Siku za kumlilia zilipopita, Yusufu alisema na watu wa nyumba ya Farao, akinena, Kama nimeona neema machoni penu, tafadhalini mkaseme masikioni mwa Farao, mkinena, Baba yangu aliniapisha, akisema,[#Est 4:2]

5Mimi ni katika kufa, unizike katika kaburi langu nililojichimbia katika nchi ya Kanaani. Basi tafadhali uniruhusu niende sasa nikamzike babangu, nami nitarudi.[#2 Nya 16:14; Isa 22:16; Mt 27:60]

6Farao akasema, Uende, ukamzike baba yako, kama alivyokuapisha.

7Basi Yusufu akaenda amzike babaye, na watumwa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, wazee wa nyumbani mwake, na wazee wote wa nchi ya Misri.

8Na nyumba yote ya Yusufu, na nduguze, na nyumba ya babaye; wakawaacha watoto wao tu, na kondoo zao, na ng’ombe zao, katika nchi ya Gosheni.

9Kisha wakaenda pamoja naye wapanda farasi, na magari; wakawa jeshi kubwa sana.

10Wakaja mpaka sakafu ya Atadi, iliyo ng’ambo ya Yordani. Wakaomboleza huko maombolezo makuu, mazito sana. Akafanya matanga ya babaye siku saba.[#Mdo 8:2; 1 Sam 31:13; Ayu 2:13]

11Nao waliokaa katika nchi, wale Wakanaani, walipoyaona matanga katika sakafu ya Atadi, wakasema, Matanga haya ya Wamisri ni makuu kwa hiyo mahali pale paliitwa Abel-Misri, iliyo ng’ambo ya Yordani.

12Wanawe wakamfanyia kama alivyo waagiza;

13kwa kuwa wanawe wakamchukuwa mpaka nchi ya Kanaani, nao wakamzika katika pango ya shamba la Makpela, iliyo mbele ya Mamre, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake pa kuzikia.[#Mwa 23:16; Mdo 7:16]

14Yusufu akarudi Misri, yeye na ndugu zake, na wote waliyokwenda pamoja naye kumzika babaye, baada ya kumzika babaye.

Yusufu Awasamehe Ndugu zake

15Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda.[#Ayu 15:21]

16Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema,

17Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye.[#Mit 28:13; Mwa 49:25]

18Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako.[#Mwa 37:7,10]

19Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu?[#Kum 32:35; Rum 12:19; Ebr 10:30]

20Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.[#Zab 56:5; Isa 10:7; Mwa 45:5,7; Mdo 3:13-15]

21Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema.[#Mwa 47:12; Mt 5:44]

Siku za Mwisho za Yusufu na Kifo Chake

22Akakaa Yusufu katika Misri, yeye na nyumba ya babaye. Akaishi Yusufu miaka mia na kumi.

23Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu.[#Ayu 42:16; Mwa 30:3]

24Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.[#Kut 8:16,17; Ebr 11:22; Mwa 26:3]

25Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu.[#Mwa 47:29; Kut 13:19; Yos 24:32]

26Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika sanduku, huko Misri.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania