Isa 45

Koreshi, Chombo cha Mungu

1Haya ndiyo BWANA amwambiayo Koreshi, masihi wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya wafalme; ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa.[#Zab 73:23; Isa 41:13; #45:1 Au, mtiwa mafuta (taz. 1 Sam 2:10).]

2Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma;

3nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.[#Kut 33:12]

4Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua.[#Isa 44:1; Mdo 17:23; Gal 1:8,9; Efe 2:12; 1 The 4:5]

5Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua;[#Kum 4:35; Zab 18:32]

6ili wapate kujua toka maawio ya jua, na toka magharibi, ya kuwa hapana mwingine zaidi ya mimi; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine.[#Zab 102:15; Mal 1:11]

7Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni BWANA, niyatendaye hayo yote.[#Amo 3:6]

8Dondokeni, enyi mbingu, toka juu,[#Zab 85:11]

Mawingu na yamwage haki;

Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu,

Nayo itoe haki ikamee pamoja;

Mimi, BWANA, nimeiumba.

9Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?[#Rum 9:20; Isa 64:8; Yer 18:6]

10Ole wake amwambiaye baba yake, Wazaa nini? Au mwanamke, Una utungu wa nini?

11BWANA, Mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni.[#Yer 31:9; Isa 29:23]

12Mimi nimeiumba dunia, nimemhuluku mwanadamu juu yake; Mimi, naam, mikono yangu mimi, imezitanda mbingu, na jeshi lake lote nimeliamuru.[#Yer 27:5]

13Mimi nimemwinua katika haki, nami nitazinyosha njia zake zote; ataujenga mji wangu, naye atawaacha huru watu wangu waliohamishwa, si kwa kulipwa fedha, wala kwa kupewa zawadi, asema BWANA wa majeshi.[#Ezr 1:1; Rum 3:24]

14BWANA asema hivi, Kazi ya Misri, na bidhaa ya Kushi, na Waseba, watu walio warefu, watakujilia, nao watakuwa wako; watakufuata; watakuja katika minyororo; wataanguka chini mbele yako, watakuomba, wakisema, Hakika Mungu yu ndani yako; wala hapana mwingine, hapana Mungu tena.[#Zab 68:31; Isa 49:23; Zek 8:22; 1 Kor 14:25]

15Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako, Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi.[#Kum 29:29; Zab 36:6; Isa 8:17; Rum 11:33]

16Watatahayarika, naam, watafadhaika, wote pia; wale wafanyao sanamu wataingia fadhaa pamoja.

17Bali Israeli wataokolewa na BWANA kwa wokovu wa milele; ninyi hamtatahayarika, wala kufadhaika, milele na milele.[#2 Sam 23:5; Zab 103:17; Hos 1:7; Rum 11:26]

18Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine.

19Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, BWANA, nasema haki; nanena mambo ya adili.[#Kum 30:11; Neh 9:13; Zab 19:8; Rum 7:12]

Miungu Haiwezi kuokoa Babeli

20Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka; hawana maarifa wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga; wamwombao mungu asiyeweza kuokoa.[#Yer 44:28; Rum 1:22]

21Hubirini, toeni habari; naam, na wafanye mashauri pamoja; ni nani aliyeonyesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, BWANA? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi.

22Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine.

23Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa.[#Mwa 22:16; Yer 22:5; Ebr 6:13; Mwa 31:53; Kum 6:13; Zab 63:11; Rum 14:11; Flp 2:10-11]

24Mmoja ataniambia, Kwa BWANA, peke yake, iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye, na wote waliomkasirikia watatahayarika.

25Katika BWANA wazao wote wa Israeli watapewa haki, na kutukuka.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania