Isa 51

Baraka Zilizowekewa Watu wa Mungu

1Nisikilizeni, ninyi mnaoifuatia haki; ninyi mnaomtafuta BWANA; uangalieni mwamba ule ambao mlitolewa kwa kuchongwa, na tundu la shimo ambalo mlitolewa kwa kuchimbuliwa.[#Mit 15:9; Mt 6:33; Rum 9:30]

2Mwangalieni Ibrahimu, baba yenu, na Sara, aliyewazaa; kwa maana alipokuwa mmoja tu nalimwita, nikambariki, nikamfanya kuwa wengi.[#Rum 4:1; Ebr 11:11]

3Maana BWANA ameufariji Sayuni; amepafariji mahali pake palipokuwa ukiwa; amefanya jangwa lake kuwa kama bustani ya Edeni, na nyika yake kama bustani ya BWANA; furaha na kicheko zitaonekana ndani yake, kushukuru, na sauti ya kuimba.[#Zab 102:13; Isa 40:1; Mwa 13:10; Yoe 2:3]

4Nisikilizeni mimi, enyi watu wangu; nisikieni, taifa langu; maana sheria itatoka kwangu, nami nitaistarehesha hukumu yangu iwe nuru ya mataifa.

5Haki yangu i karibu, wokovu wangu umekuwa wazi, na mikono yangu itawahukumu kabila za watu; visiwa vitaningoja, navyo vitautumainia mkono wangu.[#Isa 46:13; Rum 1:16]

6Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka.[#Mt 24:35; 2 Pet 3:10]

7Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao.[#Zab 37:31; Mt 10:28; Lk 12:4; Mdo 5:41]

8Maana nondo itawala kama vazi, na funza atawala kama sufu; bali haki yangu itakuwa ya milele, na wokovu wangu hata vizazi vyote.

9Amka, amka, jivike nguvu,[#Ufu 11:17; Ayu 26:12; Zab 87:4; Eze 29:3]

Ee mkono wa Bwana;

Amka kama katika siku zile za kale,

Katika vizazi vile vya zamani.

10Si wewe uliyemkata-kata Rahabu?[#Kut 14:21]

Uliyemchoma yule joka?

Si wewe uliyeikausha bahari,

Na maji ya vilindi vikuu;

Uliyevifanya vilindi kuwa njia,

Ili wapite watu waliokombolewa?

11Nao waliokombolewa na BWANA watarejea,

Watafika Sayuni, wakiimba;

Furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao;

Watapata shangwe na furaha;

Huzuni na kuugua zitakimbia.

12Mimi, naam, mimi, ndimi niwafarijiye; wewe u nani hata ukamwogopa mtu atakayekufa, na mwanadamu atakayefanywa kuwa kama majani?[#2 Kor 1:3; Zab 118:6; 1 Pet 1:24]

13Ukamsahau BWANA, Muumba wako, yeye aliyezitanda mbingu, na kuiweka misingi ya dunia; nawe unaogopa daima mchana kutwa kwa sababu ya ghadhabu yake yeye aoneaye, hapo afanyapo tayari kuharibu; nayo i wapi ghadhabu yake aoneaye?[#Ayu 9:8; 20:7]

14Yeye aliyehamishwa na kufungwa atafunguliwa kwa haraka; wala hatakufa na kushuka shimoni, wala chakula chake hakitapunguka.[#Zek 9:11]

15Maana mimi ni BWANA, Mungu wako, niichafuaye bahari, mawimbi yake yakavuma.[#Kut 14:21; Zab 74:13; 93:3,4; Isa 17:12; 43:16]

16BWANA wa majeshi ndilo jina lake. Nami nimetia maneno yangu kinywani mwako, nami nimekusitiri katika kivuli cha mkono wangu, ili nizipande mbingu, na kuiweka misingi ya dunia, na kuuambia Sayuni, Ninyi ni watu wangu.[#Kum 18:18; Yn 3:34; Isa 59:21; 65:17; 2 Pet 3:13]

17Amka, amka, simama, Ee Yerusalemu,[#Kum 28:28,34; Zab 60:3; Ufu 14:10; 16:19]

Wewe uliyenywea, mkononi mwa BWANA,

Kikombe cha hasira yake;

Bakuli la kikombe cha kulevya-levya

Umelinywea na kulimaliza.

18Hapana hata mmoja wa kumwongoza

Miongoni mwa wana wote aliowazaa,

Wala hapana hata mmoja wa kumshika mkono

Miongoni mwa wana wote aliowalea.

19Mambo haya mawili yamekupata;[#Amo 7:2]

Ni nani awezaye kukusikitikia?

Ukiwa na uharibifu, na njaa na upanga;

Niwezeje kukutuliza?

20Wana wako wamezimia,[#Omb 2:11,12]

Wamelala penye pembe za njia kuu zote

Kama kulungu wavuni;

Wamejaa hasira ya BWANA,

Lawama ya Mungu wako.

21Basi, kwa sababu ya hayo, ulisikilize neno hili, ewe uliyeteswa, na kulewa, lakini si kwa mvinyo;

22BWANA, Bwana wako na Mungu wako, awateteaye watu wake, asema hivi, Tazama, nimeondoa mkononi mwako kikombe cha kulevya-levya, hilo bakuli la kikombe cha hasira yangu; hutakinywea tena;[#Yer 50:34]

23nami nitakitia mikononi mwao wakutesao; waliokuambia nafsi yako, Inama, tupate kupita; nawe uliufanya mgongo wako kuwa kama nchi, na kama njia, kwa hao wapitao juu yake.[#Zek 12:2; Zab 66:11,12]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania