Yer 32

Yeremia Anunua Shamba Wakati wa Kuzingirwa

1Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, katika mwaka wa kumi wa Sedekia, mfalme wa Yuda, nao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa Nebukadreza.[#Yer 39:1; 2 Fal 25:1-7]

2Basi, wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli liliuzunguka Yerusalemu; na Yeremia, nabii, alikuwa amefungwa ndani ya uwanda wa walinzi, uliokuwa katika nyumba ya mfalme wa Yuda.[#Neh 3:25; Mt 5:12; Yer 33:1; 37:21]

3Kwa maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga, akisema, Kwa nini unatabiri, na kusema, BWANA asema hivi, Angalia, nitatia mji huu katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atautwaa;[#Yer 21:4-7]

4tena, Sedekia, mfalme wa Yuda, hatapona kutoka katika mikono ya Wakaldayo, lakini hakika yake atatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli, atanena naye mdomo kwa mdomo, na macho yake yatatazama macho yake;[#2 Fal 25:4-7; Yer 39:5; 52:9]

5naye atamchukua Sedekia mpaka Babeli, naye atakuwako huko hata nitakapomjilia, asema BWANA; mjapopigana na Wakaldayo hamtafanikiwa.[#Yer 27:22; 21:4; Mit 21:30]

6Yeremia akasema, Neno la BWANA limenijia, kusema,

7Tazama, Hanameli, mwana wa Shalumu, mjomba wako, atakujia, akisema, Jinunulie shamba langu lililoko Anathothi; maana haki ya ukombozi ni yako, ulinunue.[#Law 25:24-32; Rut 4:4]

8Basi Hanameli, mwana wa mjomba wangu, akanijia ndani ya uwanda wa walinzi, sawasawa na lile neno la BWANA, akaniambia, Tafadhali, ulinunue shamba langu lililoko Anathothi, katika nchi ya Benyamini; maana haki ya urithi ni yako, na haki ya ukombozi ni yako; ujinunulie. Ndipo nikajua kama neno hili ni neno la BWANA.[#Yer 1:1]

9Basi nikalinunua shamba lile lililoko Anathothi kwa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, nikampimia fedha yake, shekeli kumi na saba za fedha.[#Mwa 23:16]

10Nami nikaitia sahihi ile hati, na kuipiga muhuri, nikawaita mashahidi, nikampimia ile fedha katika mizani.[#Isa 8:2]

11Nikaitwaa ile hati ya kununua, ile iliyopigwa muhuri kama ilivyo sheria na ada, na ile nayo iliyokuwa wazi;

12na ile hati ya kununua nikampa Baruku, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, mbele ya uso wa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, na mbele ya mashahidi wale walioitia sahihi hati ya kununua, mbele ya Wayahudi wote walioketi katika uwanda wa walinzi.[#Yer 36:4]

13Nami nikamwagiza Baruku mbele yao, nikisema,

14BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Twaa hati hizi, hati hii ya kununua, hati hii iliyopigwa muhuri, na hii iliyo wazi pia, ukazitie katika chombo cha udongo, zipate kukaa siku nyingi.

15Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyumba na mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.

Yeremia Aomba apate Kuelewa

16Hata nikiisha kumpa Baruku, mwana wa Neria, hati ile ya kununua, nalimwomba BWANA, nikisema,[#Mwa 32:9-12; Dan 9:1; Flp 4:6,7]

17Aa! Bwana MUNGU, tazama, wewe umeziumba mbingu na nchi, kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyoshwa; hapana neno lililo gumu usiloliweza;[#2 Fal 19:15; Mwa 18:14; Zek 8:6; Mt 19:26; Mk 10:27; Lk 1:37; Rum 4:21]

18wewe uwarehemuye watu elfu nyingi, uwalipaye baba za watu uovu wao vifuani mwa watoto wao baada yao; Mungu aliye mkuu, aliye hodari, BWANA wa majeshi ndilo jina lake;[#Kut 20:6; Kum 5:9,10; Zab 45:3-6; Isa 9:6; Tit 2:13; Yer 10:16]

19mkuu wa mashauri, mweza katika kutenda; ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya njia zake, na kwa kadiri ya matunda ya matendo yake,[#Isa 28:29; Ayu 34:21; Zab 33:13-15; Mit 5:21; Yer 16:17; 17:10; Zab 62:12; Mhu 12:14; Mt 16:27; Yn 5:29]

20wewe uliyeweka ishara na ajabu katika nchi ya Misri hata siku hii ya leo, katika Israeli na kati ya watu wengine; na kujifanyia jina kama ilivyo leo;[#Kut 9:16; 1 Nya 17:21; Isa 63:12]

21ukawatoa watu wako, Israeli, katika nchi ya Misri, kwa ishara, na kwa ajabu, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mkuu;[#Kut 6:6; 2 Sam 7:23]

22ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kwamba utawapa, nchi iliyojaa maziwa na asali;[#Kut 3:8; Yer 11:5]

23nao wakaingia, wakaimiliki; lakini hawakuitii sauti yako, wala hawakuenda katika sheria yako; hawakutenda neno lo lote katika haya uliyowaagiza wayatende; basi, kwa sababu hii umeleta juu yao mabaya haya yote;[#Neh 9:26; Dan 9:10]

24angalia maboma haya; wameujia mji huu ili kuutwaa; na mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo wanaopigana nao, kwa sababu ya upanga, na njaa, na tauni; na hayo uliyosema yamekuwa; na, tazama, wewe unayaona.[#Yer 14:12; Yos 23:15]

25Nawe, Ee Bwana MUNGU, umeniambia, Jinunulie shamba lile kwa fedha, ukawaite mashahidi; iwapo mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo; je! Itakuwaje?

Hakikisho la Mungu Kuhusu Kurudi kwa Watu

26Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia, kusema,

27Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?[#Isa 64:8; Zab 115:3]

28Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitautia mji huu katika mikono ya Wakaldayo, na katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, naye atautwaa;[#2 Fal 25:1-11; 2 Nya 36:17-21]

29na Wakaldayo, wanaopigana na mji huu, watakuja, na kuutia moto mji huu, na kuuteketeza, pamoja na nyumba zake, ambazo juu ya dari zake wamemfukizia Baali uvumba, na kuwamiminia miungu mingine vinywaji, ili kunikasirisha.[#Yer 21:10; 19:13]

30Maana wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wametenda yaliyo mabaya tu mbele za uso wangu, tangu ujana wao; maana wana wa Israeli wamenichokoza tu kwa matendo ya mikono yao, asema BWANA.[#Eze 20:28]

31Kwa kuwa mji huu umekuwa sababu ya kunitia hasira, na sababu ya ghadhabu yangu, tangu siku ile walipoujenga hata siku hii ya leo; ili niuondoe usiwe mbele za uso wangu;[#Sef 3:1; 2 Fal 23:27]

32kwa sababu ya mabaya yote ya wana wa Israeli, na ya wana wa Yuda, waliyoyatenda ili kunitia hasira, wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao, na watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu.[#Isa 1:4-6; Dan 9:8]

33Tena wamenigeuzia visogo vyao, wala si nyuso zao; ingawa naliwafundisha, niliondoka mapema na kuwafundisha, lakini hawakusikiliza ili wapate mafundisho.[#Yer 7:13]

34Bali waliweka machukizo yao ndani ya nyumba iliyoitwa kwa jina langu, ili kuinajisi.[#2 Fal 23:4,5; Yer 7:30-31; 19:1-6; Eze 8:5]

35Tena walijenga mahali palipoinuka kwa Baali, palipo katika bonde la mwana wa Hinomu, ili kuwapitisha wana wao na binti zao katika moto kwa ajili ya Moleki, jambo nisilowaagiza; wala halikuingia moyoni mwangu kwamba walitende chukizo hilo; wapate kumkosesha Yuda.[#Law 18:21; 2 Fal 23:10; Yer 7:31; 19:5]

36Basi sasa, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, katika habari za mji huu, ambao ninyi mnasema juu yake maneno haya, Umetiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli, kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni;

37Tazama, nitawakusanya, na kuwatoa katika nchi zote nilikowafukuza, katika hasira yangu, na uchungu wangu, na ghadhabu yangu nyingi; nami nitawaleta tena hata mahali hapa, nami nitawakalisha salama salimini;[#Kum 30:3; Yer 23:6]

38nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao;[#Yer 24:7]

39nami nitawapa moyo mmoja na njia moja, wapate kunicha sikuzote; kwa mema yao, na ya watoto wao baada yao;[#Eze 11:19]

40nami nitafanya agano la milele pamoja nao, kwamba sitageuka wala kuwaacha, ili niwatendee mema; nami nitatia kicho changu mioyoni mwao, ili wasiniache.[#Isa 55:3; Yer 31:33]

41Naam, nitafurahi juu yao niwatendee mema, nami nitawapanda katika nchi hii kweli kweli, kwa moyo wangu wote, na kwa roho yangu yote.[#Kum 30:9; Yer 24:6]

42Maana BWANA asema hivi, Kama nilivyoleta mabaya makuu haya yote juu ya watu hawa, vivyo hivyo nitaleta juu yao mema hayo yote niliyowaahidia.[#Yer 31:28]

43Na mashamba yatanunuliwa katika nchi hii, mnayoitaja, mkisema, Ni ukiwa, haina mwanadamu wala mnyama; imetiwa katika mikono ya Wakaldayo.[#Yer 33:10]

44Watu watanunua mashamba kwa fedha, watazitia sahihi hati zake, na kuzipiga muhuri, na kuwaita mashahidi, katika nchi ya Benyamini, na katika mahali palipo pande zote za Yerusalemu, na katika miji ya Yuda, na katika miji ya nchi yenye vilima, na katika miji ya nchi tambarare, na katika miji ya Negebu; kwa maana nitawarudisha wafungwa wao, asema BWANA.[#Yer 17:26; 33:7]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania