The chat will start when you send the first message.
1BWANA asema hivi, Angalia, nitaamsha juu ya Babeli, na juu yao wakaao Leb-kamai, upepo uharibuo.[#51:1 yaani Ukaldayo, kwa fumbo.]
2Nami nitapeleka wageni mpaka Babeli, watakaompepea; nao wataifanya nchi yake kuwa tupu; kwa kuwa katika siku ya taabu watakuwa juu yake pande zote.[#Yer 15:7; 50:14; #2 Fal 19:7; Yer 4:11]
3Juu yake apindaye upinde, mwenye upinde na apinde upinde wake, na juu yake ajiinuaye katika dirii yake; msiwaachilie vijana wake; liangamizeni jeshi lake lote.
4Nao wataanguka, hali ya kuuawa, katika nchi ya Wakaldayo, hali ya kutumbuliwa katika njia kuu zake.[#Yer 49:26]
5Kwa maana Israeli, wala Yuda, hakuachwa na Mungu wake, BWANA wa majeshi; ijapokuwa nchi yao imejaa hatia juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.[#Zab 91:14; Zek 1:15]
6Kimbieni kutoka kati ya Babeli, kila mtu na ajiokoe nafsi yake; msikatiliwe mbali katika uovu wake; maana ni wakati wa kisasi cha BWANA, atamlipa malipo.[#Ufu 18:4; Yer 25:14]
7Babeli umekuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa BWANA; kilicholevya dunia yote; mataifa wamekunywa mvinyo wake; kwa sababu hiyo mataifa wameingiwa na wazimu.[#Ufu 17:2-4; 18:3; Yer 25:16]
8Babeli umeanguka na kuangamia ghafula; mpigieni yowe; twaeni zeri kwa maumivu yake; ili labda apate kuponywa.[#Isa 21:9; 1 The 5:12; Ufu 18:9; Yer 46:11]
9Tungependa kuuponya Babeli,[#Ufu 18:5; Isa 13:14; Yer 46:16]
Lakini haukuponyeka;
Mwacheni, nasi twendeni zetu,
Kila mtu hata nchi yake mwenyewe;
Maana hukumu yake inafika hata mbinguni,
Nayo imeinuliwa kufikilia mawinguni.
10BWANA ameitokeza haki yetu;[#Zab 37:6]
Njoni, tutangaze katika Sayuni
Habari za kazi ya BWANA, Mungu wetu.
11Inoeni hiyo mishale; zishikeni ngao kwa nguvu; BWANA ameziamsha roho za wafalme wa Wamedi; kwa sababu shauri lake ni juu ya Babeli auangamize; maana ni kisasi cha BWANA, kisasi cha hekalu lake.[#Isa 13:17]
12Twekeni bendera juu ya kuta za Babeli, yatieni malindo nguvu, wawekeni walinzi, tengenezeni waviziao; kwa maana BWANA ameazimia na kutenda yote aliyoyasema juu yao wakaao Babeli.[#Nah 2:1]
13Ewe ukaaye juu ya maji mengi, uliye na hazina nyingi, mwisho wako umewadia, kadiri ya tamaa zako.[#Ufu 17:1]
14BWANA wa majeshi ameapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika nitakujaza watu, kama nzige, nao watapiga kelele juu yako.[#Yer 49:13; Nah 3:15]
15Ameiumba dunia kwa uweza wake,[#Mwa 1:1; Zab 146:5,6; Isa 49:26; Mdo 14:15; Kol 1:16,17; Ebr 1:2,3; Ayu 9:8]
Ameuthibitisha ulimwengu kwa hekima yake,
Na kwa ufahamu wake amezitandika mbingu.
16Atoapo sauti yake pana mshindo wa maji mbinguni,[#Zab 135:7]
Naye hupandisha mawingu toka ncha za nchi;
Huifanyia mvua umeme,
Huutoa upepo katika hazina zake.
17Kila mtu amekuwa kama mnyama, hana maarifa;[#Yer 50:2]
Kila mfua dhahabu amefedheheshwa na sanamu yake ya kuchonga;
Maana sanamu yake ya kuyeyuka ni uongo,
Wala hamna pumzi ndani yake.
18Ni ubatili tu, ni kazi za udanganyifu;[#Yon 2:8]
Wakati wa kujiliwa kwao watapotea.
19Yeye, Fungu la Yakobo, siye kama hawa;[#Zab 16:5; 73:26; Yer 10:16; Omb 3:24]
Maana ndiye aliyeviumba vitu vyote;
Na Israeli ni kabila ya urithi wake;
BWANA wa majeshi ndilo jina lake.
20Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme;[#Isa 10:5; Yer 50:23]
21na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;
22na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke;[#2 Nya 36:17]
23na kwa wewe nitamvunja-vunja mchungaji na kundi lake; na kwa wewe nitamvunja-vunja mkulima na jozi yake ya ng’ombe; na kwa wewe nitawavunja-vunja maliwali na maakida.
24Nami nitamlipa Babeli, na wote wakaao ndani ya Ukaldayo, mabaya yao yote, waliyoyatenda katika Sayuni mbele ya macho yenu, asema BWANA.[#Yer 50:15,16]
25Tazama, mimi ni juu yako, Ee mlima uharibuo, asema BWANA; wewe uiharibuye dunia nzima; nami nitaunyosha mkono wangu juu yako, na kukufingirisha chini toka majabalini; nami nitakufanya kuwa mlima ulioteketezwa.[#Isa 13:2; Zek 4:7; Ufu 8:8]
26Wala hawatatwaa kwako jiwe moja liwe la pembeni, wala jiwe moja liwe msingi; bali wewe utakuwa ukiwa daima, asema BWANA.
27Itwekeni bendera katika nchi, pigeni tarumbeta kati ya mataifa, yawekeni mataifa tayari juu yake; ziiteni juu yake falme za Ararati, na Mini, na Ashkenazi; agizeni jemadari juu yake; wapandisheni farasi, kama tunutu.[#Isa 13:2; Yer 15:14; 50:41]
28Wekeni mataifa tayari juu yake, wafalme wa Wamedi, na maliwali wake, na maakida wake, na nchi yote ya mamlaka yake.
29Nayo nchi yatetemeka, nayo ina utungu; maana makusudi ya BWANA juu ya Babeli yasimama, kuifanya nchi ya Babeli ukiwa, isikaliwe na mtu.[#Yer 50:13]
30Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana;[#Isa 19:16; Omb 1:9; Amo 1:5]
Wanakaa katika ngome zao;
Ushujaa wao umewapungukia;
Wamekuwa kama wanawake;
Makao yake yameteketea;
Makomeo yake yamevunjika.
31Tarishi mmoja atapiga mbio kumlaki mwingine,[#Yer 50:24]
Na mjumbe mmoja atapiga mbio kumlaki mwenziwe,
Ili kumpasha habari mfalme wa Babeli,
Ya kuwa mji wake umetwaliwa kila upande.
32Navyo vivuko vimeshambuliwa,
Nayo makangaga wameyatia moto,
Nao watu wa vita wameingiwa na hofu.
33Kwa maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi; Binti Babeli amekuwa kama sakafu ya kufikichia wakati wa kukanyagwa kwake; bado kitambo kidogo na wakati wa mavuno utafika kwake.[#Isa 21:10; Yoe 3:13; Mt 13:30]
34Nebukadreza, mfalme wa Babeli, amenila, ameniseta, amenifanya kuwa chombo kitupu; amenimeza kama joka, amelijaza tumbo lake vitu vyangu vya anasa; amenitupa[#2 Nya 36:9,10; Yer 24:1]
35Udhalimu niliotendwa mimi, na uliotendwa mwili wangu, umpate Babeli; ndivyo atakavyosema yeye akaaye Sayuni; na Yerusalemu atasema, Damu yangu na iwe juu yao wakaao katika Ukaldayo.
36Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitakutetea, nami nitatwaa kisasi kwa ajili yako; nami nitaikausha bahari yake, nitaifanya chemchemi yake kuwa pakavu.[#Zek 1:15; Yer 50:38]
37Na Babeli utakuwa magofu, makao ya mbwa-mwitu, ajabu, na mazomeo, pasipo mtu wa kukaa huko.[#Isa 13:22; 2 Nya 29:8; Yer 18:16]
38Watanguruma pamoja kama wana-simba; watanguruma kama simba wachanga.
39Wakiingiwa na ukali, nitawafanyizia karamu yao, nami nitawalevya, wapate kufurahi, na kulala usingizi wa milele, wasiamke tena, asema BWANA.[#Dan 5:1,30]
40Nitawatelemsha kama wana-kondoo machinjoni, kama kondoo waume pamoja na mabeberu.
41Jinsi Sheshaki alivyotwaliwa![#Yer 25:26; 49:25; Isa 13:19; Dan 4:30; #51:41 yaani Babeli, kwa fumbo.]
Naye sifa ya dunia yote alivyoshambuliwa!
Jinsi Babeli alivyokuwa ukiwa
Katikati ya mataifa!
42Bahari imefika juu ya Babeli,[#Isa 8:7,8]
Umefunikwa kwa wingi wa mawimbi yake.
43Miji yake imekuwa maganjo;
Nchi ya ukame, na jangwa;
Nchi asimokaa mtu ye yote,
Wala hapiti mwanadamu huko.
44Nami nitafanya hukumu juu ya Beli katika Babeli, nami nitavitoa katika kinywa chake alivyovimeza; wala mataifa hawatamwendea tena; naam, ukuta wa Babeli utaanguka.[#Yer 50:2]
45Enyi watu wangu; tokeni katikati yake, mkajiokoe nafsi zenu na hasira kali ya BWANA, kila mmoja wenu.[#Ufu 18:4]
46Wala isizimie mioyo yenu, wala msiiogope habari itakayosikiwa katika nchi; maana habari itakuja mwaka mmoja, na baadaye mwaka wa pili habari itakuja, na udhalimu katika nchi, mwenye kutawala akishindana na mwenye kutawala.[#2 Fal 19:7]
47Basi angalia, siku zitakuja, ambazo katika siku hizo, nitafanya hukumu juu ya sanamu za Babeli, na nchi yake yote itatahayarika; na watu wake wote waliouawa wataanguka katikati yake.[#Isa 44:23; Yer 50:3]
48Ndipo mbingu, na nchi, na vitu vyote vilivyomo, vitaimba kwa furaha juu ya Babeli; kwa maana watu waangamizao watamjilia kutoka kaskazini, asema BWANA.[#Ufu 18:20; Yer 44:28]
49Kama vile Babeli alivyowaangusha watu wa Israeli waliouawa, ndivyo watakavyoanguka katika Babeli watu wa nchi yake nzima waliouawa.[#Ufu 18:24]
50Ninyi mliojiepusha na upanga,[#Yer 44:28]
Enendeni zenu, msisimame;
Mkumbukeni BWANA tokea mbali,
Na Yerusalemu ukatiwe mioyoni mwenu.
51Twaona haya kwa kuwa tumesikia mashutumu;[#Zab 44:15]
Fedheha imetufunikiza nyuso zetu;
Kwa sababu wageni wamepaingia
Patakatifu pa nyumba ya BWANA.
52Kwa sababu hiyo siku zinakuja, asema BWANA, nitakapozihukumu sanamu zake; na katika nchi yake yote waliojeruhiwa wataugua.
53Babeli ujapopanda mbinguni, na ujapopafanya mahali pa juu penye nguvu zake kuwa ngome, hata hivyo toka kwangu wenye kuangamiza watamwendea, asema BWANA.[#Yer 49:16; Amo 9:2]
54Sauti ya kilio kutoka Babeli,[#Isa 13:6-9; 15:5; Yer 50:22; Sef 1:10]
Na ya uangamivu mkuu toka nchi ya Wakaldayo!
55Maana BWANA amwangamiza Babeli,
Na kuikomesha sauti kuu ndani yake;
Na mawimbi yake yavuma kama maji mengi,
Mshindo wa sauti zao wafanya makelele;
56Kwa maana mwenye kuangamiza amefika kwake;[#Kum 32:35; Zab 94:1]
Naam, amefika Babeli;
Na mashujaa wake wametwaliwa;
Pinde zao zimevunjika kabisa;
Maana BWANA ni Mungu wa kisasi;
Hakika yake yeye atalipa.
57Nami nitawalevya wakuu wake, na watu wake wenye hekima, maliwali wake, na maakida wake, na mashujaa wake; nao watalala usingizi wa milele, wasiamke, asema Mfalme, BWANA wa majeshi, ambaye jina lake ni BWANA.[#Yer 46:18; 48:15]
58BWANA wa majeshi asema hivi, Kuta pana za Babeli zitabomolewa kabisa, na malango yake marefu yatateketezwa; nao watu watajitaabisha kwa ubatili, na mataifa kwa moto; nao watachoka.[#Hab 2:13]
59Neno ambalo Yeremia, nabii, alimwamuru Seraya, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa kumiliki kwake. Basi Seraya alikuwa msimamizi mkuu wa nyumba ya mfalme.
60Naye Yeremia akaandika katika kitabu habari ya mabaya yote yatakayoupata Babeli, maneno hayo yote yaliyoandikwa juu ya Babeli.
61Naye Yeremia akamwambia Seraya, Utakapofika Babeli, basi angalia uyasome maneno haya yote,
62ukaseme, Ee BWANA, umenena habari za mji huu kwamba utakatiliwa mbali, usikaliwe na awaye yote, wala wanadamu wala wanyama, lakini uwe ukiwa hata milele.[#Yer 50:3,39]
63Tena itakuwa utakapokwisha kukisoma kitabu hicho, utakifungia jiwe, na kukitupa katika mto Frati;[#Ufu 18:21]
64nawe utasema, Hivyo ndivyo utakavyozama Babeli, wala hautazuka tena, kwa sababu ya mabaya yote nitakayoleta juu yake; nao watachoka. Maneno ya Yeremia yamefika hata hapa.