Ayu 12

Ayubu Ajibu: Mimi Nachekwa Sana

1Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2Hapana shaka ninyi ndinyi watu halisi,

Nanyi mtakapokufa, ndipo na hekima itakoma.

3Lakini mimi pia, nina fahamu kama ninyi;

Mimi si duni yenu ninyi;

Naam, ni nani asiyejua mambo kama hayo?

4Mimi ni mtu wa kuchekwa na jirani yake,[#Ayu 16:20; Zab 91:15; Yer 33:3; Mik 7:7]

Ni mtu niliyemwita Mungu, naye akanijibu;

Huyo mwenye haki, aliye mtimilifu, amekuwa ni kicheko.

5Katika mawazo yake huyo aliye na raha mna kudharau mashaka;[#Mit 14:2]

Tayari kwa ajili ya wenye kuteleza miguu.

6Hema za wapokonyi hufanikiwa,

Na hao wamkasirishao Mungu hukaa salama;

Mikononi mwao Mungu huleta vitu vingi.

7Lakini sasa waulize hao wanyama, nao watakufundisha;

Na nyuni wa angani, nao watakuambia;

8Au nena na nchi, nayo itakufundisha;

Nao samaki wa baharini watakutangazia.

9Katika hawa wote ni yupi asiyejua,

Kwamba ni mkono wa BWANA uliofanya haya?

10Ambaye nafsi ya kila kilicho hai i mkononi mwake,[#Hes 16:22; Dan 5:23; Mdo 17:28]

Na pumzi zao wanadamu wote.

11Je! Sikio silo lijaribulo maneno,

Kama vile kaakaa lionjavyo chakula?

12Wazee ndio walio na hekima,

Na katika kuishi siku nyingi iko fahamu.

13Hekima na amri zina yeye [Mungu];

Yeye anayo mashauri na fahamu.

14Tazama, yuavunja, wala haiwezekani kujenga tena;[#Ufu 3:7]

Humfunga mtu, wala haiwezekani kumfungua.

15Tazama, yuayazuia maji, nayo yakatika;[#1 Fal 17:1; Mwa 7:11]

Tena, huyapeleka, nayo yaipindua dunia.

16Kwake yeye ziko nguvu, na makusudi kufanikiwa;

Huyo adanganywaye, na mdanganyi pia ni wake.

17Yeye huwaondoa washauri hali wametekwa nyara,

Naye huwafanya waamuzi kuwa ni wapumbavu.

18Yeye hulegeza kifungo cha wafalme,

Na kuwafunga viuno vyao kwa mshipi.

19Yeye huwaondoa makuhani hali wametekwa nyara.

Na kuwapindua mashujaa.

20Huondoa matamko ya hao walioaminiwa,

Na kuondoa fahamu za wazee.

21Humwaga aibu juu ya hao wakuu,

Na kulegeza mshipi wa wenye nguvu.

22Huvumbua mambo ya siri tokea gizani,[#Mt 10:26; 1 Kor 4:5]

Na hicho kilicho giza tupu huleta mwangani.

23Huyaongeza mataifa, na kuyaangamiza;

Huyaeneza mataifa mbali, na kuyaacha.

24Huwaondolea moyo wakuu wa watu wa nchi,

Na kuwapoteza nyikani pasipokuwa na njia.

25Wao hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga,

Naye huwafanya kupepesuka kama vile mlevi.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania