Law 13

Aina za Ukoma na Dalili zake

1Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

2Mtu atakapokuwa na kivimbe katika ngozi ya mwili wake, au kikoko, au kipaku king’aacho, nalo likawa pigo la ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa wanawe, makuhani mmojawapo;[#Kum 28:27; Isa 3:17; Law 10:10,11; Kum 17:8,9; Eze 22:26; Mal 2:7; Mt 8:2-4; 10:8; Lk 17:11-16; Yn 13:8-10]

3na huyo kuhani ataliangalia hilo pigo lililo katika ngozi ya mwili; na kwamba malaika yaliyo katika hilo pigo yamegeuka kuwa meupe, na hilo pigo kuonekana kwake limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili wake, ni pigo la ukoma hilo; na kuhani atamwangalia na kusema kuwa yu mwenye unajisi.

4Na hicho kipaku king’aacho, kwamba ni cheupe katika ngozi ya mwili wake, na kuonekana kwake si shimo la kuingia ndani kuliko ngozi, na malaika hayakugeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba huyo aliye na hilo pigo;

5kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limeshangaa, na pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena;

6kisha siku ya saba kuhani atamwangalia tena; na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, wala pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atasema kuwa yu safi; ni kikoko; naye atazifua nguo zake, kisha atakuwa yu safi.[#Law 11:25; 14:8]

7Lakini kwamba kikoko kimeenea katika ngozi yake baada ya kuonyesha nafsi yake kwa kuhani kwa kupata kutakaswa kwake ataonyesha nafsi yake tena kwa kuhani;

8na kuhani ataangalia, na tazama ikiwa hicho kikoko kimeenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kuwa yu najisi; ni ukoma.[#2 Sam 3:29]

9Pigo la ukoma litakapokuwa katika mtu, ndipo ataletwa kwa kuhani;[#2 Fal 5:3]

10na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pana kivimbe cheupe katika ngozi yake, na malaika yamegeuzwa kuwa meupe, tena ikiwa pana nyama mbichi iliyomea katika kile kivimbe,[#Mk 1:44; Lk 5:14; 17:14; Hes 12:10,12; 2 Fal 5:27; 2 Nya 26:19,20]

11ni ukoma wa zamani ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa yu najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye yuna unajisi.

12Tena kwamba huo ukoma ukitokeza katika ngozi yake, na ukoma ukamwenea ngozi yote, tangu kichwa hata miguuni, kama aonavyo kuhani;

13ndipo huyo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa ukoma umemwenea mwili wake wote, atasema kuwa yu safi huyo aliye na hilo pigo umegeuka kuwa mweupe wote; yeye ni safi.

14Lakini po pote itakapoonekana nyama mbichi kwake mtu huyo, atakuwa yu najisi.

15Kuhani ataiangalia hiyo nyama mbichi, naye atasema kuwa yu najisi; ile nyama mbichi ni najisi; ni ukoma.[#Kum 24:8]

16Au kama hiyo nyama mbichi iligeuka tena, na kugeuzwa kuwa nyeupe, ndipo atamwendea kuhani,[#Lk 5:12-14]

17na huyo kuhani atamwangalia; na tazama, ikiwa hilo pigo limegeuzwa kuwa jeupe, ndipo huyo kuhani atasema kuwa yu safi huyo aliyekuwa na pigo; yeye yu safi.[#Kum 32:39; Zab 147:3]

18Tena mwili wa mtu utakapokuwa na jipu katika ngozi yake, nalo limepoa,[#Kut 9:9; 15:26; Zab 38:3-7; Isa 38:21; Kum 28:27; 2 Fal 20:7; Ayu 2:7]

19na mahali palipokuwa na lile jipu pana kivimbe cheupe, au kipaku king’aacho, cheupe lakini chekundu kidogo, ndipo atamwonyesha kuhani mahali hapo;

20na kuhani ataangalia, na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na malaika yakiwa yamegeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; ni pigo la ukoma limetokea katika hilo jipu.

21Lakini kuhani akipaangalia, na tazama hamna malaika meupe ndani yake, wala hapana pa kuingia ndani kuliko ile ngozi, lakini paanza kufifia, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;

22na kwamba pameenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo.

23Lakini ikiwa kipaku hicho king’aacho kimeshangaa pale pale, wala hakienei, ni kovu ya jipu; na kuhani atasema kwamba yu safi.[#Mit 28:13; Mt 8:4; Lk 5:14; 17:14; 1 Kor 5:5; Gal 6:1; 1 Pet 4:2,3]

24Au mwili wa mtu ukiwa una mahali katika ngozi yake penye moto, na hiyo nyama iliyomea pale penye moto, kama kikiwa kipaku chekundu kidogo, au cheupe;

25ndipo kuhani atapaangalia; na tazama, yakiwa malaika yaliyo katika kile kipaku yamegeuka kuwa meupe, na kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe; ni ukoma, umetokea katika mahali penye moto; na kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo la ukoma.[#Kut 4:6,7; Hes 12:10; 2 Sam 3:29; 2 Fal 5:27; 2 Nya 26:19; Mt 8:1-3; Mk 1:40-42; Lk 5:12-14]

26Lakini kuhani akipaangalia, na tazama, malaika meupe hamna katika hicho kipaku king’aacho, nacho hakikuingia ndani kuliko ngozi, lakini chafifia; ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;

27na kuhani atamwangalia siku ya saba; kama kimeenea katika ngozi, ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo la ukoma.[#Law 10:10; Yer 15:19; Eze 22:26]

28Na kama hicho kipaku kikishangaa pale pale, wala hakikuenea katika ngozi, lakini kimefifia; ni kufura kwake pale penye moto, na kuhani atasema kwamba yu safi; kwa kuwa ni kovu la kuwasha hili.

29Tena mtu, mume au mke, akiwa na pigo juu ya kichwa, au katika ndevu zake,

30ndipo kuhani ataliangalia hilo pigo; na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, tena zikiwamo nywele za rangi ya manjano kisha nyembamba, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi, maana, ni kipwepwe, ni ukoma wa kichwa, au wa ndevu.[#Kum 24:8; Mal 2:7; 1 Kor 12:9; Kum 28:27; Isa 3:17]

31Tena kuhani akiliangalia lile pigo la kipwepwe, na tazama, kwamba kumeonekana si kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, wala hamna nywele nyeusi ndani yake, ndipo kuhani atamweka mahali huyo aliye na pigo la kipwepwe muda wa siku saba;

32na siku ya saba kuhani ataliangalia hilo pigo; na ikiwa hicho kipwepwe hakikuenea, wala hamna nywele za rangi ya manjano ndani yake, na kwamba kipwepwe hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe,

33ndipo huyo mtu atanyolewa, lakini hicho kipwepwe hatakinyoa; na kuhani atamweka mahali huyo aliye na kipwepwe muda wa siku saba tena;[#Ayu 1:20; Rum 8:13]

34na siku ya saba kuhani atakiangalia hicho kipwepwe, na tazama, ikiwa kipwepwe hakikuenea katika ngozi yake, wala hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi; ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu safi; naye atazifua nguo zake, naye atakuwa yu safi.

35Lakini hicho kipwepwe kama kikienea katika ngozi yake baada ya kutakasika kwake;

36ndipo kuhani atamwangalia; na ikiwa hicho kipwepwe kimeenea katika ngozi yake, kuhani hatatafuta hizo nywele za rangi ya manjano; yeye yu najisi.

37Lakini akiona ya kuwa hicho kipwepwe kimeshangaa, na nywele nyeusi zimemea humo; hicho kipwepwe kimepoa, naye yu safi, na huyo kuhani atasema kwamba yu safi.[#Law 10:10; Yer 15:19; Eze 22:26; 44:23]

38Mtu, mume au mke, atakapokuwa na vipaku ving’aavyo katika ngozi ya mwili, vipaku ving’aavyo vyeupe;

39ndipo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa vile vipaku ving’aavyo vilivyo katika ngozi ya mwili wake ni vyeupe kidogo; ni mba hivyo, imetokea katika ngozi; yeye yu safi.

40Kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani mwake, yeye ni mwenye upaa, yu safi.[#Isa 15:2; Amo 8:10]

41Tena kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani upande wa mbele, yeye ni mwenye upaa wa kipaji; yu safi.

42Lakini kwamba katika kile kichwa kilicho na upaa, au kile kipaji kilicho na upaa, laonekana pigo jeupe kisha jekundu kidogo; ni ukoma, unatokea katika kichwa chake cha upaa, au katika kipaji chake cha upaa.

43Ndipo kuhani atamwangalia; na tazama, kivimbe cha pigo kikiwa cheupe na chekundu-chekundu, katika kichwa chake chenye upaa, au katika kipaji chake cha upaa, kama vile kuonekana kwa ukoma katika ngozi ya mwili;[#Law 10:10; Eze 22:26]

44yeye ni mtu mwenye ukoma, yu najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa yu najisi; pigo lake li katika kichwa chake.

45Kisha mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, nguo zake zitararuliwa, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu, naye atapiga kelele, Ni najisi, ni najisi.[#Eze 24:17,22; Mik 3:7; 1 Fal 8:37; Ayu 40:4; 42:6; Isa 6:5; Zab 61:1; 72:12; Lk 17:12,13; Ufu 21:4]

46Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago.[#Hes 5:2; 12:14; 2 Fal 7:3; 15:5; 2 Nya 26:21; Lk 17:12; 1 Kor 5:5; 2 The 3:6; Ebr 12:15]

47Tena, vazi nalo ambalo pigo la ukoma li ndani yake, kwamba ni vazi la sufu, au kwamba ni la kitani;[#Isa 59:6; 64:6; Eze 16:16; Zek 3:4; Rum 1:21-31; Yud 1:23]

48likiwa limefumwa, au kusokotwa; likiwa ni la kitani au la sufu; kwamba ni katika ngozi, au kitu cho chote kilichofanywa cha ngozi;

49hilo pigo likiwa la rangi ya majani au jekundu, katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi; ni pigo la ukoma, nalo ataonyeshwa kuhani;

50na kuhani ataliangalia hilo pigo, naye atakiweka mahali kile kilicho na pigo muda wa siku saba;[#Yer 15:19; Eze 44:23]

51kisha siku ya saba ataliangalia hilo pigo; kama pigo limeenea katika hilo lililofumwa, au katika hilo lililosokotwa, au katika ngozi, ijapokuwa hiyo ngozi ina matumizi yo yote; hilo pigo ni ukoma unaokula; vazi hilo ni najisi.[#Law 14:44; Eze 16:43]

52Naye atalichoma moto vazi hilo, kwamba ni lililofumwa au kwamba ni lililosokotwa, kama ni la sufu, au la kitani, au kitu cho chote cha ngozi, ambacho kina hilo pigo ndani yake; kwa maana, ni ukoma unaokula; vazi hilo litachomwa moto;

53Na kama kuhani akitazama, na tazama, ikiwa hilo pigo halikuenea katika hilo vazi, wala katika hilo lililofumwa, wala katika hilo lililosokotwa, wala katika kitu cho chote cha ngozi;

54ndipo kuhani ataamuru kwamba wakifue kitu kile kilicho na hilo pigo, naye atakiweka mahali muda wa siku saba tena;

55kisha kuhani ataangalia, baada ya kuoshwa hilo pigo; na tazama, ikiwa hilo pigo halikugeuka rangi yake, wala halikuenea, li najisi; utakichoma moto; ni uharibifu likiwa lina upaa ndani au nje.

56Huyo kuhani akiangalia, na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, baada ya kufuliwa kwake, ndipo atalirarua hilo pigo litoke katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa;

57kisha, likionekana li vivyo katika hilo vazi, katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi, ni pigo lenye kuenea; nawe vazi hilo lenye pigo utalichoma moto.

58Na hilo vazi, lililofumwa, au lililosokotwa, au kitu cho chote cha ngozi, utakalolifua, kama hilo pigo limetoka na kuliacha, ndipo litafuliwa mara ya pili, nalo litakuwa safi.

59Na katika pigo la ukoma katika vazi la sufu, au la kitani, kama ni katika lililofumwa, au lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi, sheria yake ni hiyo, kusema kwamba ni safi, au kusema kwamba ni najisi.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania