Lk 10

Huduma ya wale Sabini

1Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe.[#Mt 10:7-16; #Mk 6:7]

2Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.[#Mt 9:37-38; Yn 4:35]

3Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu.[#Mt 10:16]

4Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani.[#Mt 10:7-14; Mk 6:8-11; Lk 9:3-5; #2 Fal 4:29; Lk 9:3-5]

5Na nyumba yo yote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu;

6na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu.

7Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii.[#1 Kor 9:14; 1 Tim 5:18]

8Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu;[#1 Kor 10:27]

9waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.

10Na mji wo wote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni,[#Mdo 13:51]

11Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung’uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia.[#Mdo 18:6]

12Nawaambia ya kwamba siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo.[#Mwa 19:24-28; Mt 11:24; 10:15]

Huzuni kwa Miji Isiyotubu

13Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu.[#Isa 23:1-18; Eze 26:1—28:26; Yoe 3:4-8; Amo 1:9-10; Zek 9:2-4; Mt 11:21-23]

14Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi.

15Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu.[#Isa 14:13-15]

16Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.[#Mt 10:40; Mk 9:37; Lk 9:48; Yn 5:23; 15:23; 13:20]

Kurudi kwa wale Sabini

17Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.

18Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.[#Yn 12:31; Ufu 12:8,9]

19Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.[#Zab 91:13; Mk 16:18]

20Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.[#Kut 32:32; Flp 4:3; Ufu 3:5; Mt 7:22]

Yesu Ashangilia

21Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza.[#Mt 11:25-27]

22Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.[#Yn 3:35; 10:15]

23Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi.[#Mt 13:16,17]

24Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie.[#1 Pet 1:10]

Mfano wa Msamaria Mwema

25Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?[#Mt 22:35-40; Mk 12:28-34; #Lk 18:18-20]

26Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?

27Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.[#Law 19:18; Kum 6:5]

28Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.[#Law 18:5; Mt 19:17]

29Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani?

30Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa.

31Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando.

32Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando.

33Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia,[#2 Nya 28:15]

34akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza.

35Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.

36Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi?

37Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.

Yesu Awatembelea Martha na Mariamu

38Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake.[#Yn 11:1; 12:2,3]

39Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake.

40Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.

41Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi;

42lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.[#Mt 6:33]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania