Mik 6

Mungu Awashutumu Waisraeli

1Basi sasa, sikieni asemavyo BWANA; Simama, ujitetee mbele ya milima, vilima navyo na visikie sauti yako.

2Sikieni, enyi milima, mateto ya BWANA, na ninyi, enyi misingi ya dunia iliyo imara; kwa maana BWANA ana mateto na watu wake, naye atahojiana na Israeli.[#Hos 12:2]

3Enyi watu wangu, nimewatenda nini? Nami nimewachosha kwa habari gani? Shuhudieni juu yangu.[#Zab 50:7; Isa 5:3,4; Yer 2:5,31]

4Kwa maana nalikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya utumwa, nami naliwapeleka Musa, na Haruni, na Miriamu, watangulie mbele yako.[#Kut 4:10-16; 12:50-51; 15:20]

5Enyi watu wangu, kumbukeni sasa alivyouliza Balaki, mfalme wa Moabu, na alivyojibu Balaamu, mwana wa Beori; kumbukeni toka Shitimu hata Gilgali, mpate kuyajua matendo ya haki ya BWANA.[#Ufu 2:14; Hes 25:1; Amu 5:11; Hes 22:2—24:25; Yos 3:1—4:19]

Matakwa ya Mungu

6Nimkaribie BWANA na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka za kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja?[#Zab 15:1; Yn 6:28]

7Je! BWANA atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu?[#Zab 50:9; Isa 1:11; 2 Fal 16:3]

8Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!

Udanganyifu na Udhalimu Kuadhibiwa

9Sauti ya BWANA inaulilia mji, na mtu mwenye akili ataliona jina lako; isikieni hiyo fimbo na yeye aliyeiagiza.

10Je! Hata sasa hazina za uovu zingalimo nyumbani mwa wabaya, na kipimo kilichopunguka, ambacho ni chukizo?

11Je! Naweza kuwa safi nami nina mizani ya udhalimu, na mfuko wa mawe ya kupimia ya udanganyifu?[#Hos 12:7; Amo 3:10]

12Kwa maana matajiri wake wamejaa jeuri, na wenyeji wake wamesema uongo, na ulimi wao una udanganyifu kichwani mwao.

13Basi, kwa ajili ya hayo, mimi nami nimekupiga kwa pigo liumizalo sana; nimekufanya kuwa ukiwa, kwa sababu ya dhambi zako.

14Utakula, lakini hutashiba; na fedheha yako itakuwa kati yako; nawe utahama, lakini hutachukua kitu salama; na hicho utakachochukua nitakitoa kwa upanga.

15Utapanda, lakini hutavuna; utazikanyaga zeituni, lakini hutajipaka mafuta; na hizo zabibu, lakini hutakunywa divai.

16Kwa maana amri za Omri ndizo zishikwazo, na matendo yote ya nyumba ya Ahabu, nanyi mnakwenda katika mashauri yao; ili nikufanye kuwa ukiwa, na wenyeji waliomo humo kuwa zomeo; nanyi mtayachukua matukano waliyotukanwa watu wangu.[#1 Fal 16:23-34; 21:25-26]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania