Neh 6

Kushindwa kwa Adui

1Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati, na Tobia, na Geshemu, Mwarabu na adui zetu hao wengine, kwamba nimeujenga ukuta, wala hayakusalia mavunjiko ndani yake; (ijapokuwa hata wakati ule sijaisimamisha milango katika malango);[#Neh 2:10; 3:1-3]

2Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudi kunifanyia mabaya.[#Mit 26:24; 1 Nya 8:12; Neh 11:25,35; Zab 12:2; Mit 26:24; Mhu 4:4; Mik 7:4,5]

3Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?[#Mit 14:15]

4Nao wakaniletea maneno kama hayo mara nne; nikawajibu maneno kama yale.[#Mit 1:10]

5Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumwa wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake;

6nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mwakusudi kuasi; ndiyo sababu waujenga huo ukuta; nawe wataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo.[#Yer 9:3; Rum 3:8; 2 Kor 6:8; 1 Pet 2:12; Neh 2:19; Ezr 4:13; Lk 23:2]

7Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu, kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa ataarifiwa mfalme sawasawa na maneno haya. Njoo sasa basi, na tufanye shauri pamoja.

8Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni.[#Ayu 13:4; Zab 36:3; Isa 59:4; Dan 11:27]

9Kwani hao wote walitaka kutuogofisha, wakisema, Italegea mikono yao katika kazi, isifanyike. Lakini sasa nitaitia mikono yangu nguvu.[#Kum 33:25; Zab 56:3; Isa 41:10; 2 Kor 12:9]

10Nikaingia nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, aliyekuwa amefungwa; naye akasema, Tukutane nyumbani mwa Mungu, ndani ya hekalu, tukaifunge milango ya hekalu; kwa maana watakuja kukuua; naam, wakati wa usiku watakuja kukuua.[#Mit 26:24]

11Nami nikasema, Je! Mtu kama mimi nikimbie? Naye ni nani, akiwa kama nilivyo mimi, atakayeingia hekaluni ili kuponya maisha yake? Sitaingia.[#Mit 28:1]

12Nikatambua, na tazama, siye Mungu aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri.[#Eze 13:22]

13Kwa sababu hii aliajiriwa, ili mimi niogope, nikafanye hivyo na kutenda dhambi, kisha wao wawe nazo habari mbaya, ili wanishutumie.

14Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, Tobia na Sanbalati sawasawa na hayo matendo yao, na yule nabii mke Noadia, na hao manabii waliosalia, waliotaka kuniogofya.[#Neh 13:29; Eze 13:17]

Ukuta Wakamilika

15Basi huo ukuta ukamalizika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli, katika muda wa siku hamsini na mbili.

16Ikawa adui zetu wote waliposikia, ndipo makafiri wote waliotuzunguka wakaogopa, nao wakakata tamaa sana machoni pao wenyewe; maana waliitambua kazi hiyo ilivyotendwa na Mungu wetu.[#Neh 2:10; 4:1; 6:1; Zab 126:2]

17Tena siku zile wakuu wa Yuda walimletea Tobia nyaraka nyingi, nazo nyaraka za Tobia zikawafikilia.

18Kwa maana walikuwa watu wengi katika Yuda waliomwapia, kwa sababu alikuwa mkwewe Shekania, mwana wa Ara; naye Yehohanani mwanawe amemwoa binti Meshulamu, mwana wa Berekia.

19Tena waliyanena mema yake mbele yangu, nayo maneno yangu humwambia yeye. Tobia naye akaniletea mimi nyaraka za kuniogofisha.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania