Isaya 56

Isaya 56

Wote wanakaribishwa

1Mwenyezi-Mungu asema:

“Zingatieni haki na kutenda mema,

maana nitawaokoeni hivi karibuni,

watu wataona wazi kwamba ninawakomboeni.

2Heri mtu anayezingatia kikamilifu ninayosema,

anayeshika sheria ya Sabato kwa heshima

na kuepa kutenda uovu wowote.

3“Mgeni anayenitambua mimi Mwenyezi-Mungu asifikiri:

‘Hakika Mwenyezi-Mungu atanitenga na watu wake.’

Naye towashi asiseme:

‘Mimi ni mti mkavu tu!’

4Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema:

Towashi ashikaye sheria zangu za Sabato,

anayefanya mambo yanayonipendeza,

na kulizingatia agano langu,

5nitampa nafasi maalumu na ya sifa

katika nyumba yangu na kuta zake;

nafasi bora kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike:

Nitampa jina la kukumbukwa daima,

na ambalo halitafutwa kamwe.

6“Watu wageni watakaonikiri mimi Mwenyezi-Mungu,

watakaoniheshimu, wakapenda jina langu na kuwa watumishi wangu,

wote watakaoshika Sabato bila kuikufuru,

watu watakaozingatia agano langu,

7hao nitawaleta katika mlima wangu mtakatifu,[#56:7 Taz Mat 21:13; Marko 11:17; Luka 19:46]

na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala;

tambiko na sadaka zao zitakubaliwa madhabahuni pangu.

Maana nyumba yangu itaitwa:

‘Nyumba ya sala kwa ajili ya watu wote’.

8“Hii ni kauli yangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu

ninayewakusanya Waisraeli waliotawanyika.

Licha ya hao niliokwisha kukusanya,

nitawakusanya watu wengine wajumuike nao.”

Viongozi wa Israeli walaumiwa

9Enyi wanyama wote wakali,

nanyi wanyama wote wa mwituni,

njoni muwatafune watu wangu.

10Maana viongozi wao wote ni vipofu;

wote hawana akili yoyote.

Wote ni kama mbwa bubu wasiobweka,

hulala tu na kuota ndoto,

hupenda sana kusinzia!

11Hao ni kama mbwa wenye uchu sana,

wala hawawezi kamwe kutoshelezwa.

Wachungaji hao hawana akili yoyote;

kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe.

12Huambiana, “Njoni, twende kutafuta divai;

njoni tunywe tushibe pombe!

Kesho itakuwa kama leo,

tena itakuwa sikukuu kubwa zaidi.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania