Isaya 6

Isaya 6

Mungu amwita Isaya kuwa nabii

1Mnamo mwaka aliofariki mfalme Uzia, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi kilicho juu na cha fahari. Pindo la vazi lake lilienea hekaluni mote,[#6:1 Taz 2Fal 15:7 2Nya 26:23]

2na juu yake walikuwa wamekaa malaika. Kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Mawili ya kufunika uso, mawili ya kufunika mwili na mawili ya kurukia.[#6:2 Au Maserafi.]

3Waliitana kila mmoja na mwenzake hivi:[#6:3 Taz Ufu 4:8]

“Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu,

ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi!

Dunia yote imejaa utukufu wake.”

4Sauti yao iliitikisa misingi ya milango ya hekalu, nalo likajaa moshi.[#6:4 Taz Ufu 15:8]

5Basi, mimi nikasema, “Ole wangu! Mimi nimeangamia, maana, midomo yangu ni najisi, na watu ninaoishi nao ni najisi kama mimi. Hata hivyo, kwa macho yangu mwenyewe, nimemwona Mfalme, Mwenyezi-Mungu wa majeshi.”

6Basi, mmoja wa hao malaika akaruka kunijia, akiwa ameshika mkononi koleo lililokuwa na kaa la moto alilolitwaa madhabahuni.

7Naye akinigusa nalo mdomoni, akasema: “Tazama, kaa hili limekugusa mdomo; umeondolewa hatia yako, umesamehewa dhambi yako.”

8Kisha nikamsikia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekuwa mjumbe wetu?” Nami nikajibu, “Niko hapa! Nitume mimi.”

9Naye akaniambia, “Nenda ukawaambie watu hawa:

‘Mtasikiliza sana, lakini hamtaelewa;

mtatazama sana, lakini hamtaona.’”

10Kisha akaniambia,

“Zipumbaze akili za watu hawa,

masikio yao yasisikie,

macho yao yasione;

ili wasije wakaona kwa macho yao,

wakasikia kwa masikio yao,

wakaelewa kwa akili zao,

na kunigeukia, nao wakaponywa.”

11Mimi nikauliza,

“Bwana, mpaka lini?”

Naye akanijibu,

“Mpaka hapo miji itakapobaki tupu bila wakazi,

nyumba bila watu,

na nchi itakapoharibiwa kabisa.

12Nami Mwenyezi-Mungu nitawapeleka watu mbali,

na kuifanya nchi yote kuwa mahame.

13Hata wakibaki watu asilimia kumi,

nao pia watateketezwa.

Hao watakuwa kama mvinje au mwaloni

ambao kisiki chake kimebaki baada ya kukatwa.”

(Kisiki hicho ni mbegu takatifu ya chanzo kipya.)

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania