The chat will start when you send the first message.
1Ni nani huyu ajaye kutoka Edomu,[#63:1-6 Taz Isa 34:5-17; Yer 49:7-22; Eze 25:12-14, 35:1-15; Amo 1:11-12;]
anayefika kutoka Bosra na mavazi ya madoa mekundu?
Ni nani huyo aliyevaa mavazi ya fahari,
anatembea kwa nguvu zake kubwa?
Ni mimi Mwenyezi-Mungu
ninayetangaza ushindi wangu;
nami ni mwenye nguvu ya kuokoa.
2Lakini mbona nguo yako ni nyekundu,
nyekundu kama ya mtu anayekamua zabibu?
3“Naam, nimekamua zabibu peke yangu,[#63:3 Taz Ufu 14:20, 19:13,15]
wala hakuna mtu aliyekuja kunisaidia.
Nimeyakanyaga mataifa kwa hasira yangu,
niliyapondaponda kwa ghadhabu yangu.
Nguo zangu zimejaa madoa ya damu yao,
imeyachafua kabisa mavazi yangu.
4Niliamua kuwa siku ya kulipiza kisasi imefika;
wakati wa kuwakomboa watu wangu umefika.
5Nilitazama na hapakuwa na wa kunisaidia;[#63:5 Taz Isa 59:16]
nilishangaa hapakuwa na wa kuniunga mkono.
Lakini nilijipatia ushindi kwa mkono wangu,
ghadhabu yangu ilinihimiza.
6Kwa hasira yangu niliwaponda watu,
niliwalewesha kwa ghadhabu yangu;
damu yao niliimwaga chini ardhini.”
7Nitasimulia fadhili za Mwenyezi-Mungu;
nitataja matendo yake yote yastahiliyo sifa,
kwa sababu ya yote aliyotutendea,
wema wake mkuu aliowapa Waisraeli kwa huruma yake,
kadiri ya wingi wa fadhili zake.
8Maana alisema juu yao:
“Hakika, hawa ni watu wangu;
watoto wangu ambao hawatanidanganya.”
Basi yeye akawa Mwokozi wao.
9Katika taabu zao zote,
hakumtuma mjumbe mwingine kuwasaidia,
ila yeye mwenyewe alikuja kuwaokoa.
kwa upendo na huruma yake aliwakomboa.
Aliwabeba na kuwachukua tangu zamani.
10Lakini wao walikuwa wakaidi,
wakaihuzunisha roho yake takatifu.
Basi, Mungu akageuka, akawa adui yao;
yeye mwenyewe akapigana nao.
11Ndipo walipokumbuka siku za zamani,[#63:11 Kiebrania: Alipozikumbuka.]
wakati wa Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu.
Wakauliza, “Yuko wapi sasa Mwenyezi-Mungu,
aliyewaokoa wachungaji wa kundi lake baharini?
Yuko wapi yule aliyeiweka roho yake takatifu kati yao,
12ambaye kwa mkono wake wenye nguvu[#63:12 Taz Kut 14:21]
alifanya maajabu kwa njia ya Mose,
akapasua bahari na kuwaongoza watu wake,
na kujipatia jina la milele?
13Aliwaongoza katikati ya vilindi vya bahari,
wakapita humo kama farasi bila kujikwaa.
14Kama ng'ombe wapelekwavyo malishoni bondeni,
ndivyo roho ya Mungu ilivyowapumzisha watu wake.
Ndivyo ee Mungu ulivyowaongoza watu wako,
nawe ukajipatia jina tukufu.”
15Ututazame kutoka mbinguni ee Mungu, uone,
utuangalie kutoka makao yako matakatifu na matukufu.
Iko wapi bidii yako kwa ajili yetu na nguvu yako?
Usiache kutuonesha upendo wako.
16Maana wewe ndiwe Baba yetu;
Abrahamu, mzee wetu, hatujali,
naye Israeli hatutambui;
lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ni Baba yetu.
Wewe umeitwa tangu kale: “Mkombozi wetu.”
17Ee Mwenyezi-Mungu, mbona unatukosesha njia zako?
Mbona unatufanya kuwa wakaidi hata tusikuogope?
Rudi ee Mungu kwa ajili ya watumishi wako,
makabila ambayo daima yalikuwa mali yako.
18Kwa kitambo tu sisi watakatifu wako tulimiliki nchi,
lakini maadui zetu wakaja wakaharibu maskani yako.
19Tumekuwa kama watu ambao hujawatawala kamwe,
kama watu ambao hawakujulikana kwa jina lako.