The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
2“Waambie watu wa Israeli hivi: Mwanamke akipata mimba, akajifungua mtoto wa kiume, atakuwa najisi kwa muda wa siku saba kulingana na siku zake zihusikanazo na hali ya wanawake.
3Mtoto huyo atatahiriwa katika siku yake ya nane.[#Taz Mwa 17:12; Luka 2:21]
4Kisha mama mtoto ataendelea kuwa najisi kwa muda wa siku thelathini na tatu. Wakati huo, kamwe asiguse chochote kilichowekwa wakfu wala kuingia mahali patakatifu mpaka siku za kutakasika kwake zitakapotimia.
5Lakini, kama amejifungua mtoto wa kike, basi, atakuwa najisi kwa muda wa majuma mawili kama ilivyo anapokuwa katika siku zake. Ataendelea katika kutakasika kwake kwa muda wa siku sitini na sita.
6“Siku za kutakaswa kwake zitakapotimia, iwe amepata mtoto wa kiume au wa kike, atamletea kuhani mlangoni mwa hema la mkutano mwanakondoo wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na kinda la njiwa au hua, kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi.
7Kuhani atamtolea mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumfanyia huyo mama ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu. Hivyo huyo mwanamke atakuwa safi kutokana na damu yake. Huo ni mwongozo kuhusu mwanamke yeyote anayejifungua mtoto wa kiume au wa kike.
8“Kama hawezi kutoa mwanakondoo, basi, ataleta hua wawili au makinda mawili ya njiwa; mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuondolea dhambi. Kuhani atamfanyia mama huyo ibada ya upatanisho, naye atakuwa safi.”[#Taz Luka 2:24]