Zaburi 111

Zaburi 111

Mungu asifika kwa matendo yake

1Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Nitamshukuru Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote,

nikijumuika na jamii ya watu waadilifu.

2Matendo ya Mwenyezi-Mungu ni makuu mno!

Wote wanaoyafurahia huyatafakari.

3Kila afanyacho kimejaa utukufu na fahari;

uadilifu wake wadumu milele.

4Amesababisha matendo yake ya ajabu yakumbukwe;

Mwenyezi-Mungu ni mwema na mwenye huruma.

5Huwapa chakula wenye kumcha;

hasahau kamwe agano lake.

6Amewaonesha watu wake nguvu ya matendo yake,

amewapa nchi za mataifa mengine ziwe mali yao.

7Matendo yake ni ya haki na ya kuaminika;

kanuni zake zote ni za kutegemewa.

8Amri zake zadumu daima na milele;

zimetolewa kwa haki na uadilifu.

9Aliwakomboa watu wake

na kufanya nao agano la milele.

Yeye ni mtakatifu na wa kutisha mno!

10Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa hekima;

wote wanaozitii amri zake hujaliwa busara.

Sifa zake zadumu milele.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania