The chat will start when you send the first message.
1Unilinde ee Mungu;
maana kwako nakimbilia usalama.
2Namwambia Mungu: “Wewe u Bwana wangu;
sina jema lolote ila wewe.”
3Ni bora sana hao watakatifu walioko nchini,
kukaa nao ndiyo furaha yangu.
4Lakini wanaoabudu miungu mingine,[#16:4 Maana katika Kiebrania si dhahiri.]
watapata mateso mengi.
Tambiko ya damu sitaitolea kamwe,
na majina ya miungu hiyo sitayataja.
5Wewe ee Mwenyezi-Mungu ndiwe riziki yangu kuu,
majaliwa yangu yamo mikononi mwako.
6Umenipimia sehemu nzuri sana;
naam, urithi wangu ni wa kupendeza.
7Namsifu Mwenyezi-Mungu kwa kuniongoza,
usiku dhamiri yangu yanionya.
8Namweka Mwenyezi-Mungu mbele yangu daima;[#Taz Mate 2:25-28]
yuko pamoja nami, wala sitatikisika.
9Kwa hiyo nitafurahi kwa moyo wote na kushangilia,
nami nitakaa salama salimini.
10Naam wewe hutaiacha nafsi yangu kuzimu,[#Taz Mate 13:35]
hutaniacha mimi mwaminifu wako nipate kuoza.
11Wanionesha njia ya kufikia uhai;
kuwako kwako kwanijaza furaha kamili,
katika mkono wako wa nguvu mna mema ya milele.