Zaburi 48

Zaburi 48

Siyoni mji wa Mungu

1Mwenyezi-Mungu, ni mkuu; astahili kusifiwa sana

katika mji wake na mlima wake mtakatifu.

2Mlima Siyoni huko kaskazini, wapendeza kwa urefu;[#Taz Mat 5:35]

mji wa Mfalme mkuu ni furaha ya ulimwengu.

3Mungu anazilinda ngome zake;

yeye amejionesha kuwa ngome ya usalama.

4Wafalme walikusanyika,

wakaenda pamoja kushambulia.

5Lakini walipouona mji wa Siyoni, wakashangaa;

wakashikwa na hofu, wakatimua mbio.

6Hofu kuu iliwashika,

wakasikia uchungu kama mama anayejifungua,

7kama waliokumbwa na kimbunga cha mashariki

ambacho huzivunjavunja meli za Tarshishi.

8Yote tuliyosikia tumejionea wenyewe

katika mji wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi,

naam, katika mji wa Mungu wetu;

Mungu atauimarisha milele.

9Ee Mungu, twazitafakari fadhili zako,

tukiwa hekaluni mwako.

10Jina lako lasifika kila mahali,

sifa zako zaenea popote duniani.

Kwa mkono wako umetenda kwa haki;

11watu wa Siyoni na wafurahi!

Watu wa Yuda na washangilie,

kwa sababu ya maamuzi yako ya haki!

12Tembeeni huko Siyoni mkauzunguke,

mkaihesabu minara yake.

13Zitazameni kuta zake

na kuchunguza ngome zake;

mpate kuvisimulia vizazi vijavyo, kwamba:

14“Huyu ni Mungu, Mungu wetu milele!

Atakuwa kiongozi wetu milele!”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania