The chat will start when you send the first message.
1Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nakimbilia usalama kwako;
uniokoe na wote wanaonidhulumu, unisalimishe.
2La sivyo, watakuja kunirarua kama simba,
wakanivutia mbali, pasiwe na wa kuniokoa.
3Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu!
Kama nimetenda moja ya mambo haya:
Kama nimechafua mikono yangu kwa ubaya,
4kama nimemlipa rafiki yangu mabaya badala ya mema,
au nimemshambulia adui yangu bila sababu,
5basi, adui na anifuatie na kunikamata;
ayakanyage maisha yangu;
na kuniulia mbali.
6Inuka ee Mwenyezi-Mungu, kwa hasira yako,
uikabili ghadhabu ya maadui zangu.
Inuka, ee Mungu wangu,
wewe umeamuru haki ifanyike.
7Uyakusanye mataifa kandokando yako,
nawe uyatawale kutoka juu.
8Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wayahukumu mataifa;
unihukumu kadiri ya uadilifu wangu,
kulingana na huo unyofu wangu.
9Uukomeshe uovu wa watu wabaya,[#Taz Ufu 2:23]
uwaimarishe watu walio wema,
ee Mungu uliye mwadilifu,
uzijuaye siri za mioyo na fikira za watu.
10Mungu ndiye ngao yangu;
yeye huwaokoa wanyofu wa moyo.
11Mungu ni hakimu wa haki;
kila siku hulaumu maovu.
12Watu wasipoongoka,
Mungu atanoa upanga wake;
atavuta upinde wake na kulenga shabaha.
13Atatayarisha silaha zake za hatari,
na kuipasha moto mishale yake.
14Tazama! Mtu mbaya hutunga uovu,
hujaa uharibifu
na kuzaa udanganyifu.
15Huchimba shimo, akalifukua,
kisha hutumbukia humo yeye mwenyewe.
16Uharibifu wake utamrudia yeye mwenyewe;
ukatili wake utamwangukia yeye binafsi.
17Nitamshukuru Mwenyezi-Mungu kwani ni mwema;
nitaimba sifa za jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu.