The chat will start when you send the first message.
1Basi, Wafilisti walipigana vita dhidi ya Waisraeli; nao Waisraeli walikimbia mbele ya Wafilisti na kuuawa katika mlima wa Gilboa.
2Lakini Wafilisti wakamzingira Shauli na wanawe, kisha wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-shua wana wa Shauli.
3Vita vilikuwa vikali sana dhidi ya Shauli. Wapiga mishale walipomwona walimjeruhi.
4Ndipo Shauli alipomwambia mtu aliyembebea silaha, “Chomoa upanga wako unichome nife, ili watu hawa wasiotahiriwa wasije wakanidhihaki.” Lakini huyo aliyembebea silaha hakuthubutu; kwa sababu aliogopa sana. Hivyo, Shauli alichukua upanga wake mwenyewe akauangukia.
5Halafu yule aliyembebea silaha alipoona kuwa Shauli amekufa, naye pia akauangukia upanga wake, akafa.
6Hivyo ndivyo Shauli alivyokufa, yeye na wanawe watatu, na jamaa yake yote.[#10:6 Si watu wote wa jamaa yake waliangamia. Mwanawe aitwaye Ishboshethi (Eshbaali) aliponea na kushika nafasi ya baba yake kama mtawala — ingawa kwa muda (2Sam 2:8-9).]
7Nao watu wa Israeli walioishi bondeni walipoona jeshi limewakimbia maadui, na ya kuwa Shauli na wanawe wamekufa, waliihama miji yao wakakimbia. Wafilisti wakaenda na kukaa katika miji hiyo.[#10:7 Yamkini hapa yahusu bonde la Yezreeli ambalo lilikuwa kaskazini ya Mlima Gilboa.]
8Kesho yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa, waliikuta maiti ya Shauli na wanawe mlimani Gilboa.
9Walimvua mavazi, wakachukua kichwa chake pamoja na silaha zake, halafu walituma wajumbe katika nchi yote ya Filistia kutangaza habari njema kwa sanamu zao na watu.
10Waliziweka silaha za Shauli katika hekalu la miungu yao; kisha wakakitundika kichwa chake katika hekalu la Dagoni.[#10:9-10 Ilikuwa desturi huko Mashariki ya Kati ya Kale kuchukua kichwa na sehemu nyingine za mwili za adui aliyeshindwa ili kutangaza ushindi na pia kama ishara ya onyo kwa maadui. Taz pia kisa kile cha Daudi na Goliathi (1Sam 17:54). “Dagoni” alikuwa mungu maarufu kupita miungu yote ya wafilisti. Inajulikana pia kwamba yapata mwaka 2000 K.K. kulikuwa na hekalu kubwa lililojengwa kule Ugariti kwa heshima ya mungu huyo. Nyaraka za Ugariti nazo zinataja kwamba Dagoni alikuwa baba yake mungu maarufu aitwaye Baali.]
11Lakini watu wa Yabesh-gileadi waliposikia yote Wafilisti waliyomtendea Shauli,
12mashujaa wote waliondoka na kuuchukua mwili wa Shauli na miili ya wanawe, wakaileta mpaka Yabeshi. Wakaizika mifupa yao chini ya mwaloni huko Yabeshi, nao wakafunga kwa muda wa siku saba.[#10:12 Itakumbukwa kwamba moja ya mambo aliyotenda Shauli mara baada ya kuwa mfalme ilikuwa kuwaokoa watu wa Yabeshi (1Sam 11:1-13). Kwa hiyo Shauli alipofariki, ili kuonesha heshima zao watu wa Yabeshi waliuchukua mwili wake na miili ya wanawe wakaizika kwa heshima.]
13Shauli alikufa kwa sababu ya kutokuwa mwaminifu; hakuwa mwaminifu kwani hakutii neno la Mwenyezi-Mungu na alikwenda kwa mwaguzi kumtaka shauri,[#10:13 Kufa kwake Shauli kunachukuliwa kama adhabu au hukumu ya Mwenyezi-Mungu kwa vile Shauli alikosa kuwa mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu. Tukio la Shauli la kutaka ushauri kwa mzimu kule Endori (jambo ambalo yaonekana lilikatazwa katika Kumb 18:9-14) linachukuliwa kama upeo wa makosa yake (1Sam 28).]
14badala ya kumwendea Mwenyezi-Mungu ili kumtaka shauri. Kwa sababu hiyo Mwenyezi-Mungu akamuua, na ufalme wake akampa Daudi mwana wa Yese.