1 Wakorintho 1

1 Wakorintho 1

1Mimi Paulo, niliyeitwa kuwa mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Sosthene,[#1:1 Gal 1:1 maelezo.; #1:1 2Kor 1:1; Gal 1:1.; #1:1-3 Namna hii ya kuanzia barua ilikuwa kawaida ya wakati huo wa Agano Jipya. Taz Rom 1:1-7 maelezo.]

2tunawaandikia nyinyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho. Nyinyi mmefanywa watakatifu katika kuungana na Kristo Yesu, mkaitwa muwe watu wa Mungu, pamoja na watu wote popote wanaomwomba Bwana wetu Yesu Kristo aliye Bwana wao na wetu pia.[#1:2 Kigiriki: “hegiasmenois”. Neno “watakatifu” lina maana ya kuwa “watu wake Mungu”. Taz Rom 1:7 maelezo na rejea 1Kor 6:11.]

3Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.

Baraka za Mungu

4Ninamshukuru Mungu wangu daima kwa ajili yenu kwa sababu amewatunukia nyinyi neema yake kwa njia ya Kristo Yesu.[#1:4 Taz Rom 6:11 maelezo. Mazingira ya maandishi katika matumizi ya msemo huo ambao hutumiwa mara nyingi na Paulo yanadokezea maana yake hapo. Neno kwa neno kutoka Kigiriki ni “katika Kristo Yesu” na hapa inaonekana kwamba Mungu ametutunukia neema kwa njia ya Kristo Yesu, au kwa kuungana na Yesu Kristo (aya ya 5).]

5Maana, kwa kuungana na Kristo mmetajirishwa katika kila kitu. Mmejaliwa elimu yote na uwezo wote wa kuhubiri.

6Maana ujumbe juu ya Kristo umethibitishwa ndani yenu,

7hata hampungukiwi kipaji chochote cha kiroho mkiwa mnangojea kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo.

8Yeye atawaimarisheni nyinyi mpaka mwisho mpate kuonekana bila hatia siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo.[#1:8 Yaani siku atakapokuja tena. Fil 1:6; 1Thes 3:13; 5:23.]

9Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita nyinyi muwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu.[#1:9 Rejea Kumb 7:9; 1Thes 5:24.]

Mgawanyiko katika jumuiya ya waumini

10Ndugu, nawasihini kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo: pataneni nyote katika kila jambo msemalo; yasiweko mafarakano kati yenu; muwe na fikira moja na nia moja.[#1:10—4:21 Katika sehemu ya kwanza ya barua hii anapambana na mazingira yasiyo ya kawaida yaliyokidhi katika kanisa na ambayo aliarifiwa juu yake na watu waliomtembelea. Paulo anashughulikia kwanza hali ya kuweko na vikundi ambavyo viliungana na viongozi kadhaa tofauti hata kusababisha mgawanyiko. Paulo anachukua fursa hiyo kuwafundisha waumini juu ya umoja wa kikristo (1:10-17), hekima ya kweli (1:18—3:4), kuhusu kuwa mtume (3:5—4:5) na juu ya majivuno (4:6-21).]

11Ndugu zangu, habari nilizopata kutoka kwa watu kadhaa wa jamaa ya Kloe, zaonesha wazi kwamba kuna kutoelewana kati yenu.[#1:11 Anatajwa tu hapa. Kloe ni jina la mwanamke.]

12Nataka kusema hivi: kila mmoja anasema chake: mmoja husema, “Mimi ni wa Paulo”, mwingine: “Mimi ni wa Apolo”, mwingine: “Mimi ni wa Kefa,” na mwingine: “Mimi ni wa Kristo.”[#1:12 Taz Mate 18:24—19:1. Huyu Mkristo alikuwa mzaliwa wa Aleksandria, Afrika ya Kaskazini, na alihubiri Habari Njema kule Korintho.; #1:12 Jina la Kiaramu la Petro (taz Mat 16:18 maelezo), nalo latumiwa na Paulo katika 1 Wakorintho na katika Wagalatia.]

13Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?

14Namshukuru Mungu kwamba sikumbatiza mtu yeyote miongoni mwenu isipokuwa tu Krispo na Gayo.[#1:14 Mate 18:8; #1:14 Rom 16:23 (rejea pia Mate 19:29 ambapo huenda yahusu mtu huyo huyo), Yeye alitoa nyumba yake itumiwe kwa ajili ya mikutano ya Wakristo na malazi kwa waliokuwa wanasafiri.]

15Kwa hiyo hakuna awezaye kusema amebatizwa kwa jina langu. (

16Samahani, nilibatiza pia jamaa ya Stefana; lakini zaidi ya hawa, sidhani kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote).[#1:16 1Kor 16:15.]

17Kristo hakunituma kubatiza, bali kuhubiri Habari Njema; tena, niihubiri bila kutegemea maarifa ya hotuba za watu, kusudi nguvu ya kifo cha Kristo msalabani isibatilishwe.[#1:17 Au, “hekima”. Biblia husema sana juu ya hekima ya kweli (taz Yak 3:13-18). Lakini hapa yahusu hekima ya kidunia (ling 1:19-21).]

Kristo ni nguvu na hekima ya Mungu

18Maana ujumbe kuhusu kifo cha Kristo msalabani ni jambo la kipumbavu kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea, lakini kwetu sisi tulio katika njia ya wokovu, ujumbe huo ni nguvu ya Mungu.[#1:18 Ujumbe uleule unaeleweka tofauti na wale wanaokolewa na wale wanaopotea (rejea 2 Kor 2:15-16; 4:3).]

19Maana Maandiko Matakatifu yasema:

“Nitaiharibu hekima yao wenye hekima,

na elimu ya wataalamu nitaitupilia mbali.”

20Yu wapi basi, mwenye hekima? Yu wapi basi, mwalimu wa sheria? Naye bingwa wa mabishano wa nyakati hizi yuko wapi? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upumbavu.[#1:20 Taz namna hiyohiyo ya kusema katika Yobu 12:17; Isa 19:12; 44:25.]

21Maana, kadiri ya hekima ya Mungu, watu hawawezi kumjua Mungu kwa njia ya hekima yao wenyewe. Badala yake, Mungu amependa kuwaokoa wale wanaoamini kwa njia ya kile ambacho wenye hekima wanakiona kuwa ni upumbavu, yaani ujumbe tunaohubiri.[#1:21 Ulimwengu haukutumia ujuzi uliokuwa nao (rejea Rom 1:19-20) ili kujua hekima ya kweli ya Mungu iliyodhihirishwa kwa kifo cha Yesu Kristo (aya ya 24).]

22Wayahudi wanataka ishara, na Wagiriki wanatafuta hekima;[#1:22 Wayahudi walitafuta ishara, yaani miujiza ya ajabu (rejea Mat 12:38-39; 16:1-4; Yoh 4:48). Wagiriki walikuwa mashuhuri kwa shule zao za filosofia. Neno “Filosofia” linamaanisha kupenda hekima. Rejea Mate 17:18-32.]

23lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa. Kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo, na kwa watu wa mataifa ni upumbavu;[#1:23 Wazo kwamba kifo cha mtu, tena kwa kusulubiwa, kingeweza kusababisha kukombolewa au kuokolewa kwa watu ni jambo ambalo kwa wasioamini haliwezi kupokelewa. Nao Wayahudi pia hawakuamini kwamba Masiha angeweza kusulubiwa. Aidha nao wasio Wayahudi hawangeweza kukubali kwamba mtu aliyesulubiwa angeweza kuheshimiwa na kupewa sifa za Mungu mwenyewe.]

24lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu.[#1:24 Rom 1:6. Kuhusu Kristo kama hekima ya Mungu rejea Kol 2:3.]

25Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu kuliko nguvu za binadamu.

26Ndugu, kumbukeni wakati mlipoitwa: wengi wenu hawakuwa wenye hekima hata kwa fikira za binadamu; wengi hawakuwa wenye nguvu au watu wa tabaka la juu.

27Ndiyo kusema, Mungu aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni upumbavu, ili awaaibishe wenye hekima; na aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni dhaifu, ili awaaibishe wenye nguvu.[#1:27 Au, “yasiyo muhimu”, neno kwa neno “yasiyo na kizazi” yaani wasio wa tabaka ya juu (aya ya 26).]

28Mungu ameyachagua yale ambayo kwa fikira za dunia ni mambo yaliyo duni na yanayodharauliwa, mambo ambayo hata hayakuwako, ili kwa hayo ayafutilie mbali yale ambayo kwa fikira za binadamu ni mambo ya maana.

29Basi, hakuna mtu awezaye kujivunia chochote mbele ya Mungu.

30Mungu mwenyewe ndiye aliyewaunganisha nyinyi na Kristo Yesu. Mungu amemfanya Kristo awe hekima yetu; kwa njia yake sisi tunapatanishwa na Mungu, tunakuwa watu wake Mungu na kukombolewa.[#1:30 Kwa maneno mengine; “tunakubaliwa na Mungu kuwa waadilifu”. Neno kwa neno “amekuwa uadilifu wetu” (au “haki yetu” katika tafsiri za awali za Kiswahili). Kulingana na fikra za Paulo, hapa yahusu kitenzi chenye maana ya kwamba Mungu huwafanya watu wawe na uhusiano mwema naye, huwafanya wakubalike kuwa waadilifu (taz 6:11 na pia Rom 1:17).]

31Basi, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:

“Mwenye kutaka kujivuna,

na ajivunie kazi ya Bwana.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania