The chat will start when you send the first message.
1Yahusu sasa mambo yale mliyoandika: naam, ni vizuri kama mtu haoi;[#7:1-40 Kuanzia hapa katika 7:1 Paulo anayakabili masuala kadha wa kadha ambayo Wakristo wa Korintho walikuwa wameyapeleka kwake.; #7:1 Mazingira ya wakati huo ni muhimu ili kuelewa vizuri anachosema Paulo. Kwanza kabisa ni lile wazo lililosambaa miongoni mwa Wakristo wa kwanza kwamba kurudi kwake Yesu kulikuwa karibu na Wakristo wengine waliona hakuna maana kuoa kwa misingi hiyo. Hisia nyingine ni kwamba baadhi ya waumini Wakorintho walifikiri wangekuwa wamempendeza Mungu wasipokuwa na uhusiano wa mwili ulioko kati ya mume na mke (aya 1-5). Katika aya 12-16 Paulo anasema kwamba mtu ambaye si Mkristo na ameoa hukubalika kwa Mungu kwa njia ya huyo mwenzake Mkristo.]
2lakini kwa sababu ya hatari ya uzinzi, basi, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe.
3Mume atimize wajibu alio nao kwa mkewe, naye mke atimize wajibu alio nao kwa mumewe.[#7:3-4 Hapa Paulo anaonesha uwiano wa wajibu na haki zinazowahusu mume na mke.]
4Mke hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mumewe anayo; hali kadhalika naye mume, hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mkewe anayo.
5Msinyimane haki zenu, isipokuwa kama mnaafikiana kufanya hivyo kwa kitambo tu, ili mpate nafasi nzuri ya kusali. Kisha rudianeni tena mara, ili Shetani asije akawajaribuni kwa sababu ya udhaifu wenu.
6Ninayowaambieni sasa ni mawaidha, si amri.
7Ningependa watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mmoja anacho kipaji chake kutoka kwa Mungu; mmoja kipaji hiki na mwingine kile.[#7:7 Yaonekana kwamba Paulo hakuwa na mke (aya ya 8). Tena inaonekana pia kutoka katika sehemu ya pili ya aya hii kwamba Paulo anaziona hali hizo mbili (kuoa na kutooa) kama zawadi au kipaji kutoka kwa Mungu.]
8Basi, wale ambao hawajaoa na wale walio wajane nawaambia kwamba ni vema kuendelea kuwa kama mimi nilivyo.
9Hata hivyo, kama mtu hawezi kujizuia, basi na aoe; maana ni afadhali zaidi kuoa kuliko kuwaka tamaa.
10Kwa wale waliooa ninayo amri, tena si yangu, ila ni ya Bwana: mke asiachane na mumewe;[#7:10-11 Paulo anayaweka mafundisho yake katika msingi wa mapokeo ambayo mwanzo wake ulikuwa Yesu (rejea Mat 5:32; 19:9; Marko 10:11-12; Luka 16:18); wakati ule yaliwahusu Wayahudi walioolewa, hali hapa Paulo anayatumia kwa waumini Wakristo waliooa.]
11lakini kama akiachana naye, basi abaki bila kuolewa; ama la, apatanishwe na mume wake. Mume naye asimpe talaka mkewe.
12Kwa wale wengine, (mimi binafsi, si Bwana) nasema hivi: Ikiwa mwanamume Mkristo anaye mke asiyeamini, na huyo mwanamke akakubali kuendelea kuishi naye, asimpe talaka.[#7:12 Paulo alikuwa mwangalifu sana kubainisha alichofundisha yeye mwenyewe na alichoagiza Bwana Yesu. Yahusu mazingira ya namna yake yaliyohitaji mwongozo, na ambayo hayakuwako katika mafundisho ya Yesu (taz 1Kor 7:10-11).]
13Na, kama mwanamke Mkristo anaye mume asiyeamini, na huyo mwanamume akakubali kuendelea kuishi naye, basi, asimpe talaka mumewe.
14Kwa maana huyo mume asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mkewe; na huyo mke asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mumewe. Vinginevyo watoto wao wangekuwa si wa Mungu; kumbe sasa ni watoto wake Mungu.[#7:14 Wazo linaloonekana kujumuika katika visa hivi ni kwamba muungano wa ndoa ni mtakatifu, na watoto wanaozaliwa katika ndoa hiyo nao pia wanakuwa wamekubaliwa na Mungu, na kutokana na hali hiyo, mume mwaamini na mke asiye mwaamini au mke mwaamini na mume asiye mwaamini na watoto wao wanafaidika kutokana na uhusiano wao na kanisa.]
15Hata hivyo, ikiwa yule asiyeamini anataka kumwacha mwenzake aliye Mkristo, basi, na amwache tu. Hapo huyo Mkristo, mume au mke, atakuwa huru. Maana Mungu amewaiteni nyinyi muishi kwa amani.
16Wewe mama Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mume wako? Au wewe mume Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mkeo?
17Kwa vyovyote kila mmoja na aishi kufuatana na vipaji alivyogawiwa na Bwana, na kama alivyoitwa na Mungu. Hili ndilo agizo langu kwa makanisa yote.
18Kama mtu aliitwa akiwa ametahiriwa, basi asijisingizie kwamba hakutahiriwa; na kama alipoitwa hakuwa ametahiriwa, basi na asitahiriwe.[#7:18 Hatuna uhakika wa mazingira ya maneno haya. Baadhi wanafikiri Paulo alikuwa anashauri Wakristo wawe wanyofu bila kujitakia hali ambayo hawana; mtazamo huu unalingana na tabia iliyokuwako ya wakati wa utawala wa Wagiriki huko Mashariki ya Kati ambapo vijana Wayahudi kwa namna moja au nyingine walijaribu kuficha kutahiriwa kwao.]
19Maana kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; kilicho muhimu ni kuzishika amri za Mungu.
20Basi, kila mmoja na abaki kama alivyokuwa wakati alipoitwa.
21Je, wewe ulikuwa mtumwa wakati ulipoitwa? Sawa, usijali; lakini ukipata fursa ya kuwa huru, itumie.[#7:21 Tafsiri nyingine yamkini: “Lakini ukipata fursa ya kuwa huru, chagua angalau kutumia vema hali yako kama mtumwa”. Sehemu hii ya pili aya hii ni ngumu; neno kwa neno: “Lakini kama unaweza kuwa huru, tumia”.]
22Maana yeye aliyeitwa na Bwana akiwa mtumwa huyo huwa mtu huru wa Bwana. Hali kadhalika naye aliyeitwa akiwa mtu huru, huwa mtumwa wa Kristo.[#7:22 Katika mazingira ya Kiswahili na Afrika kwa jumla ambapo wazo la kuwa mtumwa linaambatana na ukatili mkuu na wa kuchukiza, inakuwa vigumu kuelewa msemo “mtumwa wa Kristo”. Ni dhahiri kwamba hapa inamaanisha kwamba huyo aliyeitwa na kuokolewa na Bwana sasa anamtumikia yeye peke yake; aya ifuatayo inaelekea kuwa inaendeleza wazo hilo hilo.]
23Nyote mmenunuliwa kwa bei; kwa hiyo msiwe tena watumwa wa watu.
24Ndugu zangu, kila mmoja wenu basi, na abaki na Mungu kama alivyokuwa wakati alipoitwa.
25Sasa, kuhusu mabikira na waseja, sina amri kutoka kwa Bwana; lakini natoa maoni yangu mimi ambaye kwa huruma yake Bwana nastahili kuaminiwa.
26Basi, kutokana na shida iliyopo sasa nadhani ingefaa mtu abaki kama alivyo.[#7:26 Yahusu, au taabu na mateso, au hali ya mwisho wa nyakati ambayo baadhi ya waumini wa kwanza walikuwa wanafikiri iko karibu (taz aya ya 29,31).]
27Je, umeoa? Basi, usitake kuachana na mkeo. Wewe hukuoa? Basi, usitake kuoa.
28Lakini ikiwa utaoa hutakuwa umetenda dhambi; na msichana akiolewa hatakuwa ametenda dhambi. Hao watakaooana watapatwa na matatizo ya dunia hii, lakini mimi ningependa hayo yasiwapate nyinyi.
29Ndugu, nataka kusema hivi: muda uliobaki ni mfupi. Na tangu sasa wale waliooa na waishi kama vile hawakuoa;
30wenye kulia wawe kama hawalii, na wenye kufurahi wawe kama hawafurahi; wanaonunua wawe kama hawana kitu;
31nao wenye shughuli na dunia hii wawe kama vile hawana shughuli sana nayo. Maana ulimwengu huu, kama tuujuavyo, unapita.
32Ningependa nyinyi msiwe na wasiwasi. Mtu asiye na mke hujishughulisha na kazi ya Bwana jinsi atakavyompendeza Bwana.
33Mwanamume aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia jinsi atakavyompendeza mkewe,
34naye amegawanyika. Mwanamke asiyeolewa au bikira hujishughulisha na mambo ya Bwana apate kujitolea mwili na roho kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii jinsi atakavyompendeza mumewe.
35Nawaambieni haya kwa faida yenu, na si kwa kuwawekeeni kizuizi. Nataka tu muwe na mpango unaofaa, mpate kumtumikia Bwana kwa moyo na nia moja.
36Kama mtu anaona kwamba hamtendei vyema mchumba wake asipomwoa, na kama tamaa zake zinamshinda, na afanye atakavyo; waoane tu; hatakuwa ametenda dhambi.[#7:36-38 Aya hizi ni ngumu kueleweka na wafafanuzi wengi wa Maandiko ya Biblia wanahitilafiana kuhusu maana yake. Wengine, badala ya “mchumba” (aya ya 36), wana “binti”.]
37Lakini kama huyo mwanamume akiamua kwa hiari moyoni mwake kutooa na kama anaweza kuzitawala tamaa zake na kuamua namna ya kufanya, basi, anafanya vizuri zaidi asipomwoa huyo mwenzake bikira.
38Kwa maneno mengine: yule anayeamua kuoa anafanya vema; naye anayeamua kutooa anafanya vema zaidi.
39Mwanamke aliyeolewa huwa amefungwa na mumewe kwa muda wote mumewe aishipo. Lakini mumewe akifa, mama huyo yuko huru, na akipenda anaweza kuolewa na mtu yeyote, mradi tu iwe Kikristo.
40Lakini, nionavyo mimi, atakuwa na heri zaidi kama akibaki hivyo alivyo. Hayo ni maoni yangu, na nafikiri mimi pia ninaye Roho wa Mungu.