The chat will start when you send the first message.
1Habari hii yahusu Neno la uhai lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe.[#1:1-4 Utangulizi huu una mambo muhimu yanayozungumziwa ambayo yapatikana pia katika utangulizi wa Injili ya nne (Yoh 1:1-18). Mwandishi anautumia utangulizi huu kuimarisha imani ya waumini juu ya Yesu Kristo: kwamba yeye alikuwa na mwili kweli, na kwamba waumini wasiyumbishwe ila wazingatie mafundisho waliyopokea tangu mwanzo kuhusu Yesu Kristo.; #1:1 Haya ni maneno yanayomtaja Yesu Kristo ambaye ndiye Neno na ambaye alikuwako tangu mwanzo, yaani alikuwako kabla ya kuumbwa chochote (Yoh 1:1 na pia Mwa 1:1).; #1:1 Kwa kusema hivyo mwandishi anataka kusisitiza ukweli kwamba Yesu Kristo alikuwa na mwili (Yoh 1:14).]
2Uhai huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uhai huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu.[#1:2 Au: Tunashuhudia. Ling Yoh 15:27.]
3Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni nyinyi pia, ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo.[#1:3 Umoja uliopo kati ya waumini una msingi wake katika umoja kati ya Baba na Mwanawe Yesu Kristo. Hilo ni wazo muhimu pia katika Injili ya nne (Yoh 14:20; 15:4-6; 17:11,20-23).]
4Tunawaandikia nyinyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike.[#1:4 Hati nyingine za mkono zina “yenu”.]
5Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake.[#1:5—2:11 Sehemu hii ina umoja wa kimaandishi na inaunganishwa na neno muhimu “mwanga” mwanzoni na lingine, kinyume chake, “giza” mwishoni. Mara sita tunaambiwa kwa kiasi mambo wanayoshikilia wapinzani kuhusu dhambi, utii na upendo.; #1:5 Hapa pana mlinganuo kati ya mwanga, kielezo au mfano wa utakatifu, ukweli na uhai, pamoja na giza kielezo au mfano unaotumika kumaanisha dhambi, uwongo na kifo (ling 1Yoh 2:8-11). Mlinganuo wa mwanga - giza ni muhimu pia katika Injili ya Yohane (Yoh 1:5).]
6Tukisema kwamba tuna umoja naye, na papo hapo tunaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo wala hatuishi kwa ukweli kwa maneno na matendo.[#1:6 Namna hii ya kusema inarudiwa mara kwa mara aghalabu kwa madhumuni ya kuwaonya waumini dhidi ya mawazo na mafundisho ya wapinzani wa imani ya kweli kuhusu maisha adili.; #1:6 Neno hili linarudiwa mara nyingi katika barua hii; latumika kutaja njia au mwenendo wa kufuata ambao ulifunuliwa na Mungu katika nafsi ya Mwanawe Yesu Kristo na ambao huwaongoza waumini katika uhai wa milele (ling Yoh 1:14,17; 14:6).]
7Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi, tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote.[#1:7 Hapa ni dhahiri kwamba tunatakiwa kumwiga Yesu (au Mungu); taz 2:6; 3:3,16; 4:11.; #1:7 Yaani kifo cha Yesu Kristo msalabani, kifo ambacho kiliwakomboa watu (ling Efe 1:7; 1Pet 1:2 maelezo).; #1:7 Ling Ebr 9:14; Ufu 7:14.]
8Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe, na ukweli haumo ndani yetu.
9Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote.[#1:9 Ling Zab 32:5; Meth 28:13; Yak 5:16.]
10Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.