1 Yohane 2

1 Yohane 2

Kristo msaada wetu

1Watoto wangu, ninawaandikieni mambo haya, kusudi msitende dhambi. Lakini, ikijatokea mtu akatenda dhambi, tunaye mmoja ambaye hutuombea kwa Baba, ndiye Yesu Kristo aliye mwadilifu kabisa.[#2:1 Ling Rom 6:11-14.; #2:1 Maneno yanayotafsiri neno moja la Kigiriki “parakletos” ambalo pengine hutafsiriwa kama mwombezi au mtetezi au hata mfariji kulingana na yale yanazungumziwa. Tazama Yoh 14:16-17. Angalia pia Yoh 14:26; 15:26; 16:7 ambapo neno msaidizi lamtaja Roho Mtakatifu. Hapa, Yesu Kristo ndiye msaidizi au mtetezi anayemwomba Baba msamaha kwa ajili yetu (angalia pia Rom 8:34; Ebr 7:25; 9:24).]

2Kristo ndiye sadaka iondoayo dhambi zetu; wala si dhambi zetu sisi tu, bali pia dhambi za ulimwengu wote.[#2:2 Taz 1Yoh 4:10. (Taz pia Rom 3:25 maelezo na Ebr 9:11-14).]

3Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua.[#2:3 Taz pia Yoh 14:15,21,23; 17:3 maelezo. Kumjua Mungu hapa sio kumjua kwa akili bali kwa moyo yaani kuwa na uhusiano naye, uhusiano ambao wamfanya mtu anayehusika kutii amri zake Mungu.]

4Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake.

5Lakini mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye:[#2:5 Fungu hili la maneno laweza kueleweka kwa maana ya: sisi tunampenda Mungu au: Mungu anatupenda sisi au hata upendo tulionao kwa ndugu kwa kuongozwa na Mungu. Hapa yamkini yahusu zaidi upendo wa Mungu kwetu sisi.]

6mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo.[#2:6 Mara nyingine tena tunatakiwa (ni lazima) kuwa kama Yesu, kuiga mwenendo wake. Taz Yoh 13:15 ambapo wafuasi wanaambiwa “wanapaswa kufanya sawa kabisa kama alivyofanya” na maelezo ya 1:7; ling 1Pet 2:21.]

Amri mpya

7Wapenzi wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe mliousikia.[#2:7-8 Kuhusu maneno: Amri mpya na Amri ya zamani yafaa kuzingatia kamili anachosema mwandishi: Amri hiyo si mpya, yaani ni ile ile waliyofundishwa tangu mwanzo (mwanzo: yaani wakati walipoongoka; au mwanzo: yaani Yesu alipofika kuhudumu). Na pia ni amri mpya (aya 8) kwa maana yaitwa hivyo na Yesu (Yoh 13:34). Ling pia 1Yoh 2:9-11 na 3:11.]

8Hata hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana ndani ya Kristo na ndani yenu pia. Maana giza linatoweka, na mwanga wa kweli umekwisha anza kuangaza.[#2:8 Yoh 1:4-5,9, kwa maana ya mwanga halisi yaani wenye kudhihirisha kuweko kwa Mungu, nao ni kinyume cha giza ambalo ladhihirisha utawala wa Ibilisi.]

9Yeyote asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu huyo bado yumo gizani.[#2:9-11 Hapa tena tuna mwanga na giza maneno ambayo ni sambamba na kupenda na kuchukia. Katika Biblia kupenda (mtu) na kuchukia (mtu) sio mambo ya kufikiri tu bali ni vitendo. Kuhusu kutembea gizani taz Yoh 11:9-10; 12:35-36.]

10Yeyote ampendaye ndugu yake yuko katika mwanga, na hamna chochote ndani yake kiwezacho kumkwaza mtu mwingine.

11Lakini anayemchukia ndugu yake yumo gizani; anatembea gizani, na hajui anakokwenda, maana giza limempofusha.

12Ninawaandikieni nyinyi watoto kwa kuwa dhambi zenu zimeondolewa kwa jina la Kristo.[#2:12-14 Mwandishi, kwa ustadi sana wa kimaandishi, anawataja wasomaji na wasikilizaji wake pamoja na sifa zao ili kuwahimiza watilie maanani yanayosemwa, wasiyumbishwe na mafundisho mengine. Tazama aya ya 12 na 14a: watoto … dhambi zenu zimeondolewa na watoto … mnamjua Baba; aya ya 13: akina baba … mnamjua aliyekuwako tangu mwanzo (kadhalika aya 14b); na aya ya 13b: vijana … mmemshinda yule mwovu (kadhalika aya 14c). Wahusika hao watatu ni vikundi mbalimbali vya waumini, kama vile viongozi n.k.]

13Nawaandikieni nyinyi kina baba kwani mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo.[#2:13 Hapa na katika aya 14 yahusu Yesu Kristo (Yoh 1:1 na 1Yoh 1:1 maelezo).]

Nawaandikieni nyinyi vijana kwa sababu mmemshinda yule Mwovu.

14Nawaandikieni nyinyi watoto kwa sababu mnamjua Baba.

Nawaandikieni nyinyi kina baba kwa kuwa mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo.

Nawaandikieni nyinyi vijana kwa sababu mna nguvu;

neno la Mungu limo ndani yenu

na mumemshinda yule Mwovu.

15Msiupende ulimwengu, wala chochote kilicho cha ulimwengu. Mtu anayeupenda ulimwengu, upendo wa Baba hauwezi kuwamo ndani yake.[#2:15 Katika Injili ya nne na barua za Yohane, neno hili laweza kuwa na maana ya watu kwa jumla (ling Yoh 3:16; 1Yoh 2:2); lakini mara nyingi lamaanisha wale wasiompokea Yesu Kristo na wanaopinga matakwa ya Mungu; vilevile lamaanisha vitu, hali na matukio ambayo huwafanya watu wajitenge mbali na Mungu (taz Yoh 1:10 maelezo). Ling Yoh 17:14-16; Yak 1:27; 1Yoh 5:19.]

16Vitu vyote vya ulimwengu — tamaa mbaya za mwili, vitu wanavyoviona watu na kuvitamani, majivuno yasababishwayo na mali — vyote hivyo havitoki kwa Baba, bali vyatoka kwa ulimwengu.[#2:16 Neno linalotumika kutafsiri neno la Kigiriki lenye maana ya maisha pia na vitu vya kidunia ambavyo vyaweza kumfanya mtu kuwa na majivuno.]

17Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye atakalo Mungu, anaishi milele.

Adui wa Kristo

18Watoto, mwisho u karibu! Mlikwisha sikia kwamba mpinzani wa Kristo anakuja, na sasa wapinzani wengi wa Kristo wamekwisha fika, na hivyo twajua kwamba mwisho u karibu.[#2:18 Au: Huu ni wakati wa mwisho: Msemo unaotaka kugusia juu ya kuja kwake Kristo kwa mara ya pili. Waamini wengi wa nyakati za mwanzoni mwa jumuiya za Wakristo walifikiri kwamba walikuwa wanaishi nyakati za mwisho na walingojea adui wa Mungu au wa Kristo (2Thes 2:3-12) wafike kwanza kabla ya mwisho wenyewe.; #2:18 Kigiriki ni “Antikristos”, yaani mtu fulani ambaye anampinga Kristo au anapania kunyakua mahali pake. Yahusu kiumbe fulani aliyefikiriwa kuwasili kabla ya wakati ule wa mwisho na ambaye atakuwa na mengi ya kumpinga Kristo. Mwandishi anamwona huyo Adui wa Kristo katika wale watu ambao kwa mafundisho yao na maisha yao wamejitenga mbali na jumuiya ya waumini (taz 1Yoh 2:22 maelezo). Mawazo kama hayo ya Adui wa Kristo yamo pia katika Mat 24:23-25 na Marko 13:21-23 na pia katika 2Thes 2:3-12; Ufu 13; 16:12-16; 17; 19:19-21, ingawaje neno lenyewe latumika tu katika 1 na 2Yoh.]

19Watu hao wametokea kati yetu lakini hawakuwa kweli wa kwetu na ndiyo maana walituacha; kama wangalikuwa wa kwetu, wangalibaki nasi. Lakini waliondoka, wakaenda zao, kusudi ionekane wazi kwamba hawakuwa kamwe wa kwetu.

20Nyinyi, lakini, mlipata kumiminiwa Roho Mtakatifu na Kristo, na hivyo mnaujua ukweli.[#2:20 Neno kwa neno: Mmepakwa mafuta na yule Mtakatifu. Ama kweli aya hii ni ngumu kuielewa hata katika lugha ya awali. Kwanza, kupakwa mafuta, ni kuwekwa wakfu, na hapa katika 1Yoh 2:20 msemo huo watumika kama ishara na yahusu Roho Mtakatifu, ambaye kama vile mafuta, anamiminwa kwa waumini; Yoeli 2:28, sehemu ambayo pia imekaririwa katika Mate 2:17 (taz pia 2Kor 1:21-22; Isa 61:1). Mwenye kufanya kitendo hicho ni Yesu Kristo au Mungu au wote pamoja.; #2:20 1Kor 2:10-16. Taz 2:3 maelezo. Baadhi ya hati za mkono zina Ninyi mnajua yote.]

21Basi, nawaandikieni, si kwa kuwa hamwujui ukweli, bali kwa sababu mnaujua; na pia mnajua kwamba uongo wowote haupatikani katika ukweli.

22Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Kristo. Mtu wa namna hiyo ni mpinzani wa Kristo — anamkana Baba na Mwana.[#2:22 Taz 2:18 maelezo.]

23Maana yeyote anayemkana Mwana, anamkana pia Baba; na yeyote anayemkubali Mwana, anampata Baba pia.[#2:23 Yoh 5:23; 14:9; 15:23. Uhusiano na Yesu unasababisha uhusiano wa mtu na Mungu.]

24Basi, ujumbe ule mliousikia tangu mwanzo na ukae mioyoni mwenu. Kama ujumbe huo mliousikia tangu mwanzo ukikaa ndani yenu, basi, mtaishi daima katika umoja na Mwana na Baba.

25Na ahadi aliyotuahidia sisi ndiyo hii: uhai wa milele.[#2:25 Angalia Yoh 3:15 maelezo. Hapa aliyetuahidia yamkini ni Yesu Kristo.]

26Nimewaandikieni mambo haya kuhusu wale wanaotaka kuwapotosha nyinyi.

27Lakini, kwa upande wenu nyinyi, Kristo aliwatia mafuta kwa Roho wake. Na kama Roho huyo akiendelea kukaa ndani yenu, hamhitaji kufundishwa na mtu yeyote. Maana yeye anawafundisheni kila kitu, na mafundisho yake ni ya kweli, si ya uongo. Basi, shikeni mafundisho ya huyo Roho na kubaki katika muungano na Kristo.

28Naam, watoto, kaeni ndani yake kusudi wakati atakapotokea tuwe hodari bila kuwa na sababu ya kujificha kwa aibu siku ya kuja kwake.

29Mnajua kwamba Kristo ni mwadilifu kabisa; basi, mnapaswa kujua pia kwamba kila mtu atendaye mambo adili ni mtoto wa Mungu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania