1 Wamakabayo 6

1 Wamakabayo 6

Kifo cha Antioko wa Nne

(2 Mak 1:11-17; 9:1-29; 10:9-11)

1Mfalme Antioko wa Nne alipokuwa anapita Mesopotamia mikoa ya nyanda za juu alisikia habari za mji Elimaisi katika nchi ya Persia, ambao ulisifika sana kwa utajiri wake wa fedha na dhahabu.[#6:1 Namna ya Kigiriki ya kuandika “Elamu” jina la eneo la milima upande wa kusini-mashariki mwa nchi ya sasa ya Irani.]

2Hekalu lake lilikuwa na utajiri mwingi, limejaa ngao za dhahabu, deraya, na zana za vita zilizoachwa humo na Aleksanda, mwana wa mfalme Filipo wa Makedonia, aliyekuwa mtawala wa kwanza wa Wagiriki.[#6:2 Tafsiri yamkini ya makala ngumu.; #6:2 Utajiri wa hekalu ulisababisha matatizo ya kiuchumi kwa wafalme.]

3Antioko akafika Elimaisi, akajaribu kuutwaa na kuuteka nyara mji huo, lakini hakufanikiwa, kwa vile wakazi wake walikuwa wameigundua mipango yake,

4wakakusanya majeshi yao kumpinga. Basi, Antioko akarudi Babuloni na moyo mzito.

5Huko Persia Antioko akafikiwa na mjumbe aliyemwarifu kwamba majeshi aliyoyapeleka Yudea yalikuwa yameshindwa;

6kwamba Lisia na jeshi lake lenye nguvu alikuwa amelazimika kuwakimbia Wayahudi; kwamba Wayahudi walikuwa wameimarika zaidi kutokana na silaha na zana za vita na nyara walizokuwa wameteka kutoka kwa majeshi ya maadui;

7kwamba walikuwa wamebomolea mbali ile madhabahu ya mungu wa uongo aliyokuwa ameijenga Antioko juu ya madhabahu Yerusalemu; kwamba walikuwa wamelizungushia hekalu kuta ndefu kama ilivyokuwa kabla yake, na kwamba walikuwa wameuchukua na kuuhami mji wa Beth-zuri, mmoja wa miji ya mfalme Antioko.[#6:7 Wayahudi hawakuwa na haki ya kujenga mji huu ambao ulikuwa mali ya Antioko.]

8Mfalme aliposikia habari hiyo, akashikwa na mshangao na fadhaa, akajitupa kitandani na kuugua, kwa sababu mambo yalikuwa yamekwenda kinyume cha matazamio yake.[#6:8 Ukweli ni kwamba Antioko alikufa kabla ya kazi ya ujenzi wa Yerusalemu kukamilika.]

9Kwa muda mrefu alilala kwa ugonjwa huo, akizamishwa kitandani kwa mawimbi mazito ya huzuni, hata akatambua kwamba alikuwa anakufa.

10Basi, akawaita rafiki zake wote, akawaambia: “Usingizi sipati, na moyo wangu umepondeka kwa huzuni na wasiwasi.

11Kwanza nilijiuliza mwenyewe kwa nini yamenipata matatizo haya, ambapo katika utawala wangu nimekuwa mwema na ninayependwa na wote!

12Halafu nikakumbuka maovu niliyofanya kule Yerusalemu nilipochukua kutoka hekaluni vyombo vyote vya fedha na dhahabu, nikajaribu, bila sababu ya maana, kuwaangamiza wakazi wa Yudea.

13Najua hicho ndicho kisa cha mikasa hii iliyonipata, nami karibu ninakufa kwa kukata tamaa katika nchi hii ya kigeni.”[#6:13 Kwa mwandishi, chochote kilichotukia nje ya Siria kilitukia katika nchi ya kigeni.]

14Kisha akamwita Filipo, mmoja wa washauri wake wakuu, akamkabidhi milki yake yote.[#6:14 Huyu ni tofauti na yule anayetajwa katika 2Mak 5:22; 8:8.]

15Akampa taji yake, vazi lake, na pete yake ya mhuri, akamwamuru amlee na kumwelimisha mwanawe, Antioko wa Tano, hata awe mfalme.

16Mfalme Antioko akafariki dunia hapo, mwaka 149.[#6:16 Huo ni sawa na 163 K.K.]

17Lisia aliposikia kwamba mfalme amekufa, akamfanya kijana Antioko awe mfalme badala ya baba yake, na akampa jina Eupatori. Lisia alikuwa amemlea Antioko wa Tano tangu utoto.[#6:17 Yahusu jina Antioko V. Jina Eupatori lina maana ya “mwana wa baba wa tabaka ya wakuu”.]

Kampeni ya Antioko wa Tano na Lisia

(2 Mak 13:1-22)

18Wakati huo, maadui waliokuwa katika ngome ya Yerusalemu walikuwa wanawavizia watu wa Israeli katika eneo la kuzunguka hekalu. Walikuwa wanajaribu kwa namna nyingi kuwaumiza Wayahudi na hivyo kuwaimarisha watu wa mataifa.

19Basi, Yuda akaamua kuwaangamiza, akawakusanya watu wake wote ili kuwazingira maadui.

20Watu wakakusanyika wakaizingira ngome hiyo mnamo mwaka 150, na wakajenga minara na mitambo mingine ya kurushia silaha.[#6:20 Huu ni sawa na 162 K.K.]

21Lakini baadhi ya maadui waliozingirwa wakatoroka, na Wayahudi waovu kadha, wakajiunga nao.

22Basi, wakaenda kwa mfalme, wakasema, “Hivi unangoja nini kulipa kisasi kwa maovu waliyofanyiwa wananchi wenzetu?

23Sisi tulikubali kumtumikia baba yako, kushika amri zake, na kutii sheria zake.

24Lakini tulipata faida gani? Sasa wananchi wenzetu wamekuwa maadui zetu. Kwa kweli, wamemuua kila mmoja wetu waliyemwona, na wametupora mali zetu.

25Lakini hawajatudhuru sisi tu; wamewashambulia jirani zao wote.[#6:25 Wamakabayo waliendeleza nguvu yao ya utawala hata nje ya Yudea.]

26Na sasa wameizingira ngome ya Yerusalemu, wanataka kuiteka. Tena wameliimarisha hekalu na kuuhami mji wa Beth-zuri.

27Usipowazuia upesi, watafanya mengi zaidi, nawe hutaweza kuwazuia.”

28Mfalme aliposikia hayo alikasirika sana. Akawakusanya makamanda wote wa jeshi, maofisa wote wa askari wapandafarasi, na washauri wake wakuu.

29Hali kadhalika akakodi askari wa kulipwa kutoka nchi nyingine na visiwa vya Ugiriki.

30Jeshi lake likawa na askari wa miguu laki moja, wapandafarasi 20,000, na tembo wa vita 32.

31Basi, wakapita Idumea na kwenda kuuzingira mji wa Beth-zuri, ambako mapigano yalichukua muda mrefu. Jeshi la mfalme likajenga hapo mitambo ya kurushia silaha, lakini waliokuwa mjini walijitetea kwa ushujaa, wakatoka nje na kuichoma moto hiyo mitambo ya maadui.

32Kisha Yuda akaondoa vikosi vyake kutoka katika ngome ya Yerusalemu, akapiga kambi Beth-zekaria, kukabiliana na kambi ya mfalme.[#6:32 Huo ulikuwa yapata kilomita 20 kusini-mashariki ya Yerusalemu.]

33Mapema asubuhi iliyofuata, mfalme akapeleka jeshi lake kwa haraka katika barabara ya kwenda Beth-zekaria. Huko vikosi vyake vikajipanga, tayari kwa vita; wakapiga tarumbeta.

34Wakawanywesha tembo wao maji ya rangi ya zabibu na forosadi ili kuwachochea kwa ajili ya vita.

35Hao tembo wakawagawa kwa vikosi vya askari wa miguu: kwa kila tembo mmoja askari wa miguu 1,000 deraya za chuma na kofia za shaba. Pia kwa kila tembo waliteuliwa askari wapandafarasi 500, ambao daima walifuatana na tembo wao.

36Hao walimtangulia huyo tembo kokote alikokwenda, wala hawakumwacha.

37Mgongoni pa kila tembo kilifungwa kwa ukanda maalumu kibanda imara cha miti. Mbali ya mwendeshaji, (Mhindi), kila tembo alipandwa na askari wanne wenye silaha.[#6:37 Yaani mwenyeji wa India ambaye alikuwa na ujuzi wa kuongoza tembo.]

38Lisia akawapanga wapandafarasi waliobaki mbavuni mwa jeshi, upande huu na ule, ambapo waliweza kukingwa na askari wa miguu wakati wao wenyewe wanawashambulia maadui.

39Jua liliziangaza ngao zao za dhahabu na shaba, milima ikarudisha mwanga wake ikimetameta kama mienge ya moto.

40Sehemu ya jeshi la mfalme ilitawanywa kwenye vilima virefu, na nyingine kwenye tambarare, askari wakasonga mbele kwa taratibu na nidhamu.

41Wote walitetemeka waliposikia mshindo wa miguu yao na mgongano wa silaha zao. Ama hakika, jeshi lao lilikuwa kubwa sana na lenye nguvu.

42Lakini Yuda na jeshi lake wakajitia vitani, wakawaua wanajeshi 600 wa mfalme.

43Eleazari Avarani aligundua kwamba tembo mmoja alikuwa mkubwa zaidi kuliko wengine, na kwamba alikuwa amevikwa deraya ya kifalme. Akadhani mfalme mwenyewe amempanda tembo huyo.

44Hivi akajitoa mhanga kuwaokoa watu wake na kujipatia mwenyewe sifa ya kudumu milele.

45Kwa ujasiri akamkimbilia huyo tembo, katikati ya kikosi cha askari wa miguu. Akasonga mbele kwa kasi, huku anapita akiua watu kulia na kushoto kwake, hata askari wa mfalme wakamwepa kila upande.

46Akapenyeza chini ya tembo na kumchoma mkuki tumboni. Tembo akafa, akamwangukia Eleazari na kumwua.

47Lakini Wayahudi walipoona nguvu ya jeshi la mfalme na ukali wa mashambulio yake, wakarudi nyuma.

48Mfalme na jeshi lake wakasonga mbele ili kuwashambulia Wayahudi mjini Yerusalemu, wakapiga kambi Yudea na kwenye mlima Siyoni.

49Mfalme akafanya amani na Wayahudi wa Beth-zuri, nao wakaondoka mjini hapo, kwa sababu hawakuwa na chakula cha kutosha mwaka huo wa Sabato, ambapo watu hawalimi wala hawapandi.

50Mfalme akauteka mji wa Beth-zuri na kuweka kikosi cha kuulinda.

51Halafu akalizunguka hekalu na kulizingira kwa muda mrefu. Akaandaa na kutega zana za kubomolea kuta, mitambo ya kurushia silaha, na vyombo vya kutupia moto, mawe na mishale, na makombeo.[#6:51 Maelezo ya mbinu za vita za wakati huo.]

52Wayahudi nao wakatengeneza mitambo ya vita dhidi ya ile ya maadui, mapambano yakaendelea kwa siku nyingi.

53Lakini hapakuwa na chakula kilichobaki kwa sababu ulikuwa mwaka wa Sabato, na watu waliokuwa wamewakimbia watu wa mataifa mengine na kujificha Yudea walikuwa wamekula chakula chote kilichowekwa akiba Yudea.

54Uhaba wa chakula ulikuwa mkubwa hivi hata watu wengi wakawa wamerudi nyumbani kwao; wachache tu walibaki hekaluni.

55Wakati huo, Filipo, yule aliyekuwa ameteuliwa na mfalme Antioko wa Nne amlee na kumwelimisha mtoto Antioko hata awe mfalme,

56akarejea kutoka Persia na Media. Alikuwa amerudi na jeshi la mfalme, na alipanga kushika utawala wa serikali. Lisia aliposikia habari hizo,

57akatoa amri ya kuondoka haraka. Akawaambia mfalme kijana, maofisa wake na watu wake: “Kila siku nguvu zetu zinapungua. Hatuna chakula cha kutosha, na mahali hapa tunapopazingira ni pagumu. Isitoshe, kuna mambo ya dharura ya kiserikali ambayo yanadai tuyashughulikie.

58Basi, na tufanye mapatano ya amani na Wayahudi na taifa lao lote sasa.

59Tutawaruhusu kushika na kufuata sheria zao na mila zao kama walivyofanya kabla yake. Matatizo haya yote yalianza tulipowachokoza Wayahudi kwa kuondoa na kutupilia mbali sheria, mila na desturi zao.”[#6:59 Badiliko hili la hali lilitokea kwa kufa kwake Antioko IV ambaye aliwafanya watu wafuate utamaduni wa Kigiriki kwa nguvu.]

60Pendekezo hilo lilipokewa vizuri na mfalme na maofisa wake. Basi Lisia akawapa Wayahudi masharti ya amani, nao wakayapokea.

61Mfalme na maofisa wake walipokubali kwa kiapo kuyashika masharti hayo, Wayahudi wakatoka ngomeni mwao.

62Lakini mfalme alipoingia eneo la mlima Siyoni na kuona jinsi ngome hiyo ilivyokuwa imara, akavunja kiapo chake alichokuwa ameapa, akatoa amri ukuta ulioizunguka ngome ubomolewe.

63Kisha akaondoka kwa haraka, akarejea Antiokia. Huko akamkuta Filipo ameushika mji, lakini akapigana naye, akauchukua mji wa Antiokia kwa nguvu.[#6:63 Lisia aliporudi Siria pamoja na majeshi yake alimwangamiza Filipo.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania