The chat will start when you send the first message.
1Mimi Petro, mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi wateule wa Mungu Baba, ambao mmetawanyika na mnaishi kama wakimbizi huko Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithunia.[#1:1 Mate 1:15 maelezo.; #1:1 Rejea Fil 3:20; Ebr 11:13; 13:14.; #1:1 Hiyo ni mikoa ya Kiroma ya Asia Ndogo (sasa ni sehemu ya nchi ya Uturuki).]
2Mungu Baba aliwateua nyinyi kufuatana na kusudi lake, na mmefanywa watakatifu na Roho, mpate kumtii Yesu Kristo na kusafishwa kwa damu yake.[#1:2 Wafuasi wa Yesu wanafanywa kuwa “watakatifu” yaani, kuwa mali yake Mungu, kwa Roho Mtakatifu, ili waweze kumtumikia Mungu peke yake.; #1:2 Yahusu kifo cha Yesu Kristo msalabani ambacho kiliwakomboa watu. Rejea 1Pet 1:19; Ebr 9:14. Katika aya hii, kitendo cha ukombozi kinamhusisha “Mungu Baba, Roho Mtakatifu na Yesu Kristo”; (taz 2Kor 13:13 maelezo).]
Nawatakieni neema na amani tele.
3Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Ametujalia tumaini lenye uhai,[#1:3 Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu siku tatu baada ya kufa msalabani (taz Mat 28:1-10; Mate 2:22-23).; #1:3-4 Tumaini hili linasemwa kuwa “hai” kwa vile msingi wake ni ufufuo wa Yesu Kristo ambao ni asili ya uhai mpya kwa Wakristo. Rejea Yoh 11:25-26.]
4na hivyo tunatazamia kupata baraka zile ambazo Mungu aliwawekea watu wake. Mungu amewawekeeni baraka hizo mbinguni ambako haziwezi kuoza, au kuharibika, au kufifia.[#1:4 Rejea Rom 8:17 ambapo maneno hayo yanatumiwa kutafsiri neno “urithi”. Neno urithi katika A.K. linatumika mara nyingi kwa maana yake ya kawaida yaani mali anayoachiwa mtu aghalabu baada ya kifo cha mzazi. Lakini hutumika pia kuhusu ile nchi ambayo Mungu aliahidi kuwapa Waisraeli. Baadaye hasa katika A.J. matumizi yake yanahusu hasa baraka za Mungu kwa watu wake au wokovu ambao Mungu anawapa wale wanaomtegemea na huo ndio tumaini la Wakristo. Wazo hilo linarudiwa katika Barua hii (1:13,21; 3:5,15). Taz pia Gal 3:29.]
5Hizo zitakuwa zenu nyinyi ambao kwa imani mnalindwa salama kwa nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu ambao uko tayari kufunuliwa mwishoni mwa nyakati.
6Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka,[#1:6-7 Rejea Rom 5:3-5; Yak 1:2-3; 1Pet 4:12. Dhahabu ilisafishwa katika moto ili kuithibiti na kuondoa takataka nyingine, ikabaki kuwa madini safi. Hapa yahusu mateso ambayo Wakristo wanateseka au watateseka mikononi mwa wakuu wa Kiroma.]
7majaribio ambayo shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe, ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu, ambayo ni ya thamani kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa.
8Nyinyi mnampenda, ingawaje hamjamwona, na mnamwamini, ingawa hammwoni sasa. Hivyo, mnafurahi kwa furaha tukufu isiyoelezeka,
9kwa sababu mnapokea wokovu wa roho zenu ambao ni lengo la imani yenu.[#1:9 Neno “roho” katika lugha ya Biblia laweza kumaanisha nafsi na hata maisha, na sio tu roho kwa kubainisha na mwili. Rejea 1:22 na 2:25.]
10Manabii walipeleleza na kufanya uchunguzi juu ya wokovu huo, wakabashiri juu ya neema hiyo ambayo nyinyi mngepewa.
11Walijaribu kujua nyakati na mazingira ya tukio hilo, yaani wakati alioudokezea Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, akibashiri juu ya mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaofuata.
12Mungu aliwafunulia kwamba wakati walipokuwa wanasema juu ya hayo mambo ambayo nyinyi mmekwisha sikia sasa kutoka kwa wale wajumbe waliowatangazieni Habari Njema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni, hiyo kazi yao haikuwa kwa faida yao wenyewe, bali kwa ajili yenu. Hayo ndiyo mambo ambayo hata malaika wangependa kuyafahamu.
13Kwa hiyo, basi, muwe tayari kabisa, na kukesha. Wekeni tumaini lenu lote katika neema ile mtakayopewa wakati Yesu Kristo atakapoonekana!
14Kama watoto wa Mungu wenye utii, msikubali kamwe kufuata tena tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mlipokuwa wajinga.[#1:14 Yaani wakati ule ambapo hawakuwa wamemjua Mungu wa kweli na sheria aliyowapa watu wa Israeli. Ling Efe 2:3; 4:17-18.]
15Bali mnapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote, kama vile yule aliyewaiteni ni mtakatifu.
16Maandiko yasema: “Muwe watakatifu, kwa kuwa mimi alivyo mtakatifu.”
17Mnapomtaja Mungu, nyinyi humwita Baba. Basi, jueni kwamba yeye humhukumu kila mmoja kadiri ya matendo yake, bila ubaguzi. Hivyo tumieni wakati wenu uliowabakia hapa ugenini katika kumcha Mungu.[#1:17 Rejea Luka 11:2 maelezo (na taz Zab 89:26; Isa 64:8).; #1:17 Kumb 10:17; Rom 2:11; Efe 6:9; Kol 3:25. Wazo hilohilo limo katika hotuba ya Petro katika Mate 10:34.]
18Maana mnajua kwamba nyinyi mlikombolewa katika mwenendo wenu usiofaa ambao mliupokea kutoka kwa wazee wenu. Lakini hamkukombolewa kwa vitu vyenye kuharibika: kwa fedha na dhahabu;[#1:18 Au, “wa ubatili”, neno ambalo katika A.K. linatumika kuitaja miungu ya uwongo (Isa 41:29; Yer 8:19).]
19bali kwa damu ya thamani ya Kristo, ambaye alikuwa kama mwanakondoo asiye na dosari wala doa.[#1:19 Taz Yoh 1:29. Yahusu mwanakondoo asiye na dosari ambaye alitambikwa wakati wa Pasaka (Kut 12:5; 1Kor 5:7) na nyakati nyingine (Kut 29:38-42). Rejea Ufu 5:12; 13:8.]
20Yeye alikuwa ameteuliwa na Mungu kabla ya ulimwengu kuumbwa, akafunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu.
21Kwa njia yake, mnamwamini Mungu aliyemfufua kutoka kwa wafu na kumpa utukufu; na hivyo imani na matumaini yenu yako kwa Mungu.
22Maadamu sasa, kwa kuutii ukweli, nyinyi mmezitakasa roho zenu na kuwapenda wenzenu bila unafiki, basi, pendaneni kwa moyo wote.
23Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, nyinyi mmezaliwa upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele.
24Kama Maandiko yasemavyo:
“Kila binadamu ni kama majani,
na utukufu wake wote ni kama ua la majani.
Majani hunyauka na maua huanguka.
25Lakini neno la Bwana hudumu milele.”
Neno hilo ni hiyo Habari Njema mliyohubiriwa.