1 Petro 5

1 Petro 5

Kundi la Mungu

1Mimi mzee miongoni mwenu wazee wenzangu, mimi ambaye nilishuhudia mateso ya Kristo na kushiriki ule utukufu utakaofunuliwa, nawasihini[#5:1 Wale ambao walikuwa wakurugenzi wa jumuiya ya Kikristo; Mate 11:30.; #5:1 Petro alishuhudia kwa macho yake mwenyewe mateso na kusulubiwa kwake Kristo.]

2mlichunge lile kundi la Mungu mlilokabidhiwa; mlitunze si kwa kulazimika, bali kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo si kwa tamaa ya fedha, bali kwa moyo wenu wote.[#5:2 Mate 20:28. Rejea maneno ya Yesu kwa Petro katika Yoh 21:15-17.]

3Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa hilo kundi.

4Na wakati Mchungaji Mkuu atakapotokea, nyinyi mtapokea taji ya utukufu isiyofifia.[#5:4 Yaani, Yesu Kristo; taz Yoh 10:11 maelezo.; #5:4 Taz 2Tim 4:8 maelezo.]

5Kadhalika nanyi vijana mnapaswa kujiweka chini ya mamlaka ya wazee. Nyinyi nyote mnapaswa kuwa na unyenyekevu mpate kutumikiana; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwajalia neema wanyenyekevu.”[#5:5 Meth 3:34 (LXX); yamenukuliwa pia katika Yak 4:6.]

6Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa enzi wa Mungu, ili awainue wakati ufaao.

7Mwekeeni matatizo yenu yote, maana yeye anawatunzeni.

8Muwe macho; kesheni! Maana adui yenu, Ibilisi, huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mawindo.

9Muwe imara katika imani na kumpinga, mkijua kwamba ndugu zenu pote duniani wanapatwa na mateso hayohayo.

10Lakini mkisha teseka muda mfupi, Mungu aliye asili ya neema yote na ambaye anawaiteni kuushiriki utukufu wake wa milele katika kuungana na Kristo, yeye mwenyewe atawakamilisheni na kuwapeni uthabiti, nguvu na msingi imara.[#5:10 Au, “Atawathibitisheni”.]

11Kwake yawe mamlaka milele! Amina.

Salamu za mwisho

12Nimewaandikieni barua hii fupi kwa msaada wa Silwano, ndugu ambaye namjua na kumwamini. Nataka kuwapeni moyo na kushuhudia kwamba jambo hili ni neema ya Mungu kweli. Kaeni imara katika neema hiyo.[#5:12 Labda ni yule yule anayetajwa kama Sila katika Mate 15:22,40, na ambaye Paulo anamtaja katika 2Kor 1:19 na katika 1Thes 1:1; 2Thes 1:1.]

13Jumuiya ya wenzenu walioteuliwa na Mungu hapa Babuloni wanawasalimuni. Vilevile mwanangu Marko anawasalimuni.[#5:13 Wakristo wa kwanza walitumia jina Babuloni kutaja Roma na hivyo kuepa kuutaja moja kwa moja huo mji mkuu wa himaya ya Waroma (Ufu 14:8; 17:5; 18:2). Hapa yaonekana kwamba barua hii iliandikwa mjini humo.]

14Salimianeni kwa ishara ya upendo wa Kikristo.[#5:14 Taz Rom 16:16 maelezo.]

Nawatakieni amani nyinyi mlio wake Kristo.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania