The chat will start when you send the first message.
1Kulikuwa na mtu mmoja mjini Rama katika nchi ya milima ya Efraimu aitwaye Elkana wa kabila la Efraimu. Yeye alikuwa mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu.[#1:1 Makala ya Kiebrania inamtambulisha baba yake Samueli, yaani Elkana kama mwenyeji wa “Ramathaim-zofim”, katika nchi ya milima ya Efraimu. Katika habari zinazofuata juu ya Samueli kila mara jina hilo ni “Rama” (1:19; 2:11; 7:17 n.k.). Wengi wanafikiri basi kuwa “Rama” ni kifupi cha “Ramathaimu” ambalo lina maana ya “miinuko miwili” au “vilele viwili”.; #1:1-28 Sura 1—3 kimaandishi zina umoja ambao waweza kuitwa kwa jumla: historia ya kuzaliwa kwa Samueli na ujana wake. Hata hivyo umoja huo pia waweza kubainishwa katika visehemu vifuatavyo: habari za kuzaliwa kwake Samueli ambayo ni matokeo ya ahadi na ombi la mama yake kwa Mungu (1:1-23), utenzi wa shukrani (2:1-10), kuwekwa wakfu kwa Samueli (1:23-28; 2:11) simulizi la wito wake wa kuwa nabii (3:1-16) na kitendo cha kwanza cha huyo kijana nabii kama msemaji wa Mwenyezi Mungu (3:18).]
2Elkana alikuwa na wake wawili, mmoja aliitwa Hana na wa pili Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto.[#1:2 Katika Agano la Kale wanaume waliruhusiwa kuwa na mke zaidi ya mmoja (Kumb 21:15-17) lakini mara nyingi ni wachache walioweza kuwa na mke zaidi ya mmoja (k.m. viongozi n.k.) kwa sababu ya uwezo mdogo kiuchumi. Rejea Mwa 16:1-3; 29:28.]
3Kila mwaka Elkana alisafiri kutoka Rama kwenda kuabudu na kumtambikia Mwenyezi-Mungu wa majeshi kule Shilo. Huko, watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu.[#1:3 Elkana alisafiri kutoka Rama kwenda kumwabudu na kumtambikia Mwenyezi-Mungu katika mahali pa ibada kule Shilo. Kila mwanamume alitakiwa kwenda mara tatu kwa mwaka mbele ya Mwenyezi-Mungu hekaluni (taz Kut 23:14-19, Kumb 16:16-17). Sikukuu inayotajwa hapa yawezekana ni sikukuu ya vibanda ambayo Waisraeli waliadhimisha kukumbuka Mungu alivyowalinda katika safari ya wazee wao jangwani kuelekea Kanaani (taz Lawi 23:43). Lakini pia walimshukuru Mungu kwa kuwapa mazao mema mwaka huo (Kumb 16:13-15). Katika sherehe hii Hana alipatwa na huzuni kubwa kwa sababu yeye alikuwa tasa.; #1:3 Taz orodha ya majina ya Mungu katika Kut 3:15. Kiebrania ni “Yahweh sebaot”. Na kuhusu “majeshi” (sebaot) inafikiriwa kwamba hapo awali neno hilo lilitaja majeshi ya Israeli (1Sam 17:45; rejea 4:4-5). Lakini jina hili la sifa lilipotumiwa baadaye na manabii neno “majeshi” lilikuwa limepoteza maana yake ya majeshi ya Israeli likatumika kutaja majeshi ya mbinguni (rejea Zab 103:21). Hapa ilihusu sio tu malaika bali pia sayari za angani: nyota, jua n.k. Taz Zab 24:10. Jina hili la sifa la Mungu linatumiwa kwa mara ya kwanza hapa katika Biblia. Kwa ujumla “Mwenyezi-Mungu wa majeshi” humaanisha Mungu ni mwenye enzi, mwenye nguvu zote katika ulimwengu (katika tafsiri nyingine husema “Mungu mwenye uwezo wote”).; #1:3 Palikuwa mahali pakuu pa ibada wakati wa miaka ya mwanzo Waisraeli walipoingia Palestina. Taz Yos 18:1 maelezo na rejea Amu 21:19.]
4Kila wakati Elkana alipotoa tambiko alimpa mkewe Penina fungu moja la nyama ya tambiko na fungu mojamoja kwa watoto wake wa kiume na wa kike.
5Lakini Elkana alimpa Hana fungu moja ingawa alikuwa anampenda sana, na Mwenyezi-Mungu hakuwa amemjalia watoto.[#1:5 Aya hii yaweza pia kutafsiriwa: “Elkana alimpa Hana fungu maalumu la nyama ya tambiko kwa sababu alimpenda sana ingawa Mwenyezi-Mungu hakuwa amemjalia watoto”. Na kuhusu jambo la Mungu kuwajalia watu watoto ni imani ya watu wa kale na hata watu wa makabila mengi katika nchi zetu. Taz Mwa 16:2; 30:1-2,22-23; Amu 13:2; Luka 1:25.]
6Lakini Penina, mchokozi wa Hana, daima alikuwa akimkasirisha vikali na kumuudhi Hana kwa kuwa Mwenyezi-Mungu hakumjalia watoto.
7Mambo haya yaliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Penina alimkasirisha Hana hata ikawa Hana analia na kukataa kula chochote.[#1:7 Hili ni jina lingine la pale mahali pa ibada kule Shilo. Yawezekana kwamba hapo kulikuwa na hekalu ambalo baadaye liliharibiwa na Wafilisti. Lakini mara nyingi wakati huu yahusu lile hema la mkutano ambalo Mungu alimwamuru Mose kulitengeneza na ambalo ndani yake kulikuwa na lile sanduku la agano.]
8Elkana, mumewe, kila mara alimwuliza, “Kwa nini unalia? Kwa nini hutaki kula? Kwa nini una huzuni moyoni mwako? Je, mimi si bora kwako kuliko watoto kumi wa kiume?”
9Siku moja, walipokuwa wamemaliza kula na kunywa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, Hana akasimama. Wakati huo, kuhani Eli alikuwa amekaa kwenye kiti karibu na mwimo wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
10Hana alikuwa na huzuni sana. Na alipokuwa anamwomba Mwenyezi-Mungu akawa analia kwa uchungu.
11Akaweka nadhiri akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kama tu utayaangalia mateso yangu mimi mtumishi wako ukanikumbuka mimi, bila kunisahau, mimi mtumishi wako, ukanijalia mimi mtumishi wako, mtoto wa kiume, nitakupa wewe Mwenyezi-Mungu mtoto huyo awe wako maisha yake yote; wembe hautapita kichwani pake kamwe.”[#1:11 Yaani, hatanyoa nywele zake. Katika Amu 13:5 Mungu alitaka Samsoni asinyoe nywele zake; hapa Hana anamwahidi Mungu kwamba akimpata mtoto huyo hatanyoa nywele zake. Kitendo hicho pale na hapa kinaashiria mtu aliyewekwa wakfu kwa Mungu na ilikuwa mojawapo ya mambo yaliyotakiwa kwa mtu wa namna hiyo. Kuweka nadhiri ni kuapa rasmi kwa Mungu kufanya au kutofanya kitu fulani. Kwa kawaida nadhiri huwa ni za muda lakini kama hapa (siku zote za maisha yake) ni nadhiri ya kudumu (taz Hes 6:1-21).]
12Hana aliendelea kumwomba Mwenyezi-Mungu kwa muda mrefu, na kuhani Eli akawa anaangalia midomo yake.
13Hana alikuwa akiomba kimoyomoyo, lakini midomo yake ilikuwa inachezacheza, ila sauti yake haikusikika. Hivyo Eli akafikiri kuwa Hana amelewa.
14Kwa hiyo Eli akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achana na kunywa divai.”
15Lakini Hana akamjibu, “Sivyo bwana wangu; mimi ni mwanamke mwenye taabu mno; mimi sijanywa divai wala kinywaji kikali, bali nimekuwa nikimtolea Mwenyezi-Mungu yaliyomo rohoni mwangu.
16Usinidhanie kuwa mimi ni mwanamke asiyefaa kitu. Kwa muda wote huu nimekuwa nikisema mahangaiko yangu na taabu yangu.”
17Ndipo Eli akamwambia, “Nenda kwa amani; naye Mungu wa Israeli akupe kile ulichomwomba.”
18Hana akasema, “Naomba nami mtumishi wako nipate kibali mbele yako.” Hana akaenda zake, akala chakula na hakuwa na huzuni tena.
19Kesho yake asubuhi, Elkana na jamaa yake waliamka asubuhi na mapema, na baada ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu, walirudi nyumbani Rama. Elkana akalala na mkewe Hana, naye Mwenyezi-Mungu akamkumbuka.
20Hivyo Hana akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Hana akamwita mtoto huyo Samueli, kwani alisema, “Nimemwomba kwa Mwenyezi-Mungu.”[#1:20 Jina hili katika Kiebrania linafanana na neno lenye maana ya “jina lake ni Mungu”; au sehemu ya kwanza yaweza kuchukuliwa kama kitenzi na hivyo kuwa na maana: “aliyeombwa kwa Mungu” au pia “atokaye kwa Mungu”.]
21Elkana na jamaa yake yote wakaenda tena Shilo na kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko ya kila mwaka na kutimiza nadhiri.
22Lakini safari hii Hana hakwenda, kwani alimwambia hivi mumewe, “Mara mtoto atakapoachishwa kunyonya, nitampeleka ili awekwe mbele ya Mwenyezi-Mungu, abaki huko daima.”[#1:22 kwa kawaida watoto wachanga walinyonyeshwa kwa muda wa miaka mitatu.]
23Elkana, mumewe, akamjibu, “Fanya unaloona linafaa. Ngojea hadi utakapomwachisha mtoto kunyonya. Mwenyezi-Mungu aifanye nadhiri yako kuwa kweli.” Basi, Hana alibaki nyumbani, akaendelea kumlea mtoto wake hadi alipomwachisha kunyonya.
24Alipomwachisha kunyonya alimpeleka pamoja na fahali wa miaka mitatu, gunia la unga na kiriba cha divai. Hana alimwingiza mtoto kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, naye mtoto alikuwa mdogo tu.[#1:24 Hivyo katika makala za Bahari ya Chumvi (Kumrani) na tafsiri mbili za kale; Kiebrania kina: “fahali watatu”.]
25Walipokwisha kumchinja yule fahali, walimpeleka mtoto kwa kuhani Eli.
26Hana akamwambia, “Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyekuwa anasimama mbele yako akimwomba Mwenyezi-Mungu.[#1:26 Msemo wa wakati huo sawa na kuapa kwamba jambo fulani ni kweli.]
27Nilimwomba anipe mtoto huyu, na yeye alinipa kile nilichomwomba.
28Kwa sababu hiyo, mimi ninampa Mwenyezi-Mungu mtoto huyu; wakati wote atakapokuwa hai, ametolewa kwa Mwenyezi-Mungu.” Halafu, wakamwabudu Mwenyezi-Mungu hapo.