The chat will start when you send the first message.
1Wakati huo, Wafilisti walikutana pamoja, wapigane na Waisraeli. Waisraeli walipiga kambi yao huko Ebenezeri, na Wafilisti wakapiga kambi yao huko Afeka.[#4:1-22 Sura 4—6 zahusu mambo yaliyolisibu lile sanduku la agano. Katika sehemu hii Samueli hatajwi ila familia ya Eli ambayo ni ya kuangamizwa kama ilivyotangazwa katika 3:11-14. Kilele cha simulizi hili ni ule wakati sanduku hilo la agano lilipopelekwa kwa sherehe mjini Yerusalemu (1Sam 6:1-23).; #4:1 Kuna mahali kadhaa panapotajwa kwa jina hili lakini hapa yamkini ni mahali kwenye bonde la Yezreeli ambapo pia panatajwa katika 29:1.]
2Wafilisti waliwashambulia Waisraeli, na baada ya mapigano makali, Waisraeli walishindwa. Waisraeli 4,000 waliuawa kwenye uwanja wa mapambano.
3Wanajeshi walionusurika walipowasili kambini, wazee wa Israeli walisema, “Kwa nini Mwenyezi-Mungu amewaacha Wafilisti watushinde leo? Twendeni tukalilete sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu kutoka Shilo, ili aweze kwenda nasi vitani na kutuokoa kutoka na zetu.”[#4:3 Agano la Mwenyezi-Mungu (au amri kumi) lilikuwa limeandikwa juu ya vibao viwili vya mawe na kuhifadhiwa katika sanduku lililotengenezwa kwa mti wa mgunga. Sanduku hilo linatajwa kwa namna mbalimbali katika Biblia: “sanduku la Mungu” mara 36; “sanduku la agano la Mungu” mara 4; “sanduku la agano” mara 43. Katika tafsiri hii, ili kuepa msomaji asije akafikiri ni sanduku lolote lile kila mara tumetaja kuwa ni sanduku la agano na pale ambapo Mungu ametajwa nalo tumesema ni “sanduku la agano la Mungu / Mwenyezi-Mungu”.]
4Hivyo, walituma watumishi huko Shilo, nao wakalileta sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu wa majeshi ambaye anakaa kifalme juu ya viumbe wenye mabawa. Wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi walikuja pamoja na lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.[#4:4 Taz Kut 25:17-22 ling 2Sam 6:2; Zab 80:1; 99:1. Hivyo viliashiria kuweko kwa Mungu miongoni mwa watu wake.]
5Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipofika kambini Waisraeli wote walishangilia kwa furaha, hata nchi yote ikatikisika.
6Wafilisti waliposikia sauti hiyo ya furaha walisema “Kelele hizo zote kambini mwa Waebrania zina maana gani?” Walipojua kwamba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilikuwa limewasili kambini mwa Waisraeli,[#4:6 Katika Biblia ya Kiebrania, jina hili linapotumiwa (badala ya Waisraeli) huonesha kwamba anayelitaja ni mtu asiye Mwisraeli.]
7Wafilisti waliogopa; wakasema, “Bila shaka, miungu imewasili kambini mwao! Ole wetu! Jambo kama hili halijawahi kutokea.[#4:7 Wafilisti walifikiri Waisraeli kama vile wao walikuwa pia na miungu mingi.]
8Ole wetu! Ni nani atakayeweza kutuokoa kutokana na miungu hiyo yenye nguvu? Hiyo ni miungu iliyowaua Wamisri kwa kila aina ya mapigo jangwani.
9Sasa, enyi Wafilisti, jipeni moyo. Muwe, hodari msije mkawa watumwa wa Waebrania kama wao walivyokuwa watumwa wetu. Muwe hodari kama wanaume na kupigana.”
10Wafilisti walipiga vita, na Waisraeli walishindwa na kukimbia kila mtu nyumbani kwake. Siku hiyo kulikuwa na mauaji makubwa kwani askari wa miguu 30,000 wa Israeli waliuawa.
11Sanduku la agano la Mungu lilitekwa, na wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.
12Siku hiyohiyo, mtu mmoja wa kabila la Benyamini alikimbia kutoka mstari wa mbele wa mapigano mpaka Shilo huku mavazi yake yakiwa yamechanika na akiwa na mavumbi kichwani.[#4:12 Kuwa na mavazi yaliyochanika na mavumbi kichwani kulikuwa ishara ya huzuni na kilio.]
13Eli, akiwa na wasiwasi moyoni kuhusu sanduku la Mungu, alikuwa ameketi kwenye kiti chake, kando ya barabara akiangalia. Yule mtu alipowasili mjini na kueleza habari hizo, mji mzima ulilia kwa sauti.
14Eli aliposikia sauti ya kilio, akauliza, “Kelele hizo ni za nini?” Yule mtu akaenda haraka kwa Eli ili kumpa habari hizo.
15Wakati huo, Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane na macho yake yalikuwa yamepofuka.
16Yule mtu akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi; nimekimbia kutoka vitani leo.” Eli akamwuliza, “Mwanangu, mambo yalikuwaje huko?”
17Yule aliyeleta habari akasema, “Waisraeli wamewakimbia Wafilisti. Kumekuwa na mauaji makubwa miongoni mwa Waisraeli. Zaidi ya yote, wanao wote wawili, Hofni na Finehasi, wameuawa, na sanduku la agano la Mungu limetekwa.”
18Huyo mtu alipotaja tu sanduku la Mungu, Eli alianguka chali kutoka kwenye kiti chake kando ya lango. Eli alipoanguka hivyo, shingo yake ilivunjika kwani alikuwa mzee na mnene, naye akafariki. Eli alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka arubaini.[#4:18 Yaani kwenye mlango wa kuingia katika mahali hapo patakatifu kule Shilo, mahali ambapo Eli alikaa kufanya huduma yake.]
19Tena ilitokea kwamba, mkwewe Eli, yaani mke wa Finehasi, wakati huo alikuwa mjamzito, na muda wake wa kujifungua ulikuwa umekaribia. Aliposikia kwamba sanduku la agano la Mungu limetekwa na kwamba baba mkwe wake, hata na mumewe wamefariki, mara moja alipata utungu, na kujifungua.
20Basi, alipokuwa anakufa, wanawake waliokuwa wanamsaidia walimwambia, “Usiogope, maana umejifungua mtoto wa kiume.” Lakini yeye hakujibu neno, wala hakuwasikiliza.
21Naye akamwita mtoto wake Ikabodi, akimaanisha, “Utukufu wa Mungu umeondoka Israeli,” akiwa na maana kwamba sanduku la agano lilikuwa limetekwa, tena baba mkwe wake na mumewe, wote walifariki.
22Akasema, “Utukufu wa Mungu umeondoka Israeli kwani sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu limetekwa.”[#4:21-22 Jina “Ikabodi” Kiebrania ni kama maana ya “Wapi ule utukufu?” au: “Hamna utukufu”. Mkewe Finehasi aliona kutoweka kwa lile sanduku la agano kuwa sawa na kutoweka kwa Mwenyezi-Mungu maana kuweko kwa wingu juu ya sanduku la agano kuliashiria kuweko kwa Mwenyezi-Mungu (Kut 40:34).]