The chat will start when you send the first message.
1Samueli alipokuwa mzee, aliwafanya watoto wake wa kiume kuwa waamuzi wa Israeli.[#8:1—12:25 Matukio yanayosimuliwa kuanzia sura hii ya nane yanalenga mazingira mapya au hali mpya katika historia ya Waisraeli na jambo lake muhimu ni kuhusu kuanzishwa kwa utawala wa kifalme ambao unaanza na mfalme Shauli.]
2Mtoto wake wa kwanza wa kiume aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya. Wote wawili walikuwa waamuzi huko Beer-sheba.
3Lakini watoto hao hawakufuata mwenendo wa baba yao. Bali walianza kujitafutia faida. Wakapokea rushwa na kupotosha haki.[#8:3 Kupokea rushwa ilikatazwa katika sheria ya Mungu (Kut 23:8; Kumb 16:18-19).]
4Basi, viongozi wote wa Israeli walikusanyika pamoja, na kumwendea Samueli mjini Rama,
5wakamwambia, “Tazama, wewe sasa ni mzee na watoto wako hawafuati mwenendo wako. Hivyo, tuteulie mfalme wa kututawala kama yalivyo mataifa mengine.”[#8:1-5 Viongozi wa Waisraeli (wazee) walichukua hali ya uzee ya Samueli na utovu wa maadili wa watoto wake kuwa kisingizio cha kuomba wapewe mfalme wa kuwatawala (8:19-20; 10:19; 12:12).]
6Lakini jambo la Waisraeli kutaka wapewe mfalme wa kuwatawala, halikumpendeza Samueli. Naye akamwomba Mwenyezi-Mungu.
7Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sikiliza kila kitu ambacho watu wanakuambia; maana hawajakukataa wewe, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme juu yao.[#8:7 Jambo la Waisraeli kuomba wapewe mfalme lilikuwa sawa na kuvunja ahadi yao ya kwamba watamtegemea Mungu peke yake ambaye atawaokoa na kuwalinda (Hes 23:21; Kumb 33:5; 1Sam 12:12). Katika Kumb 17:14 Mose alikwisha sema kwamba wangemkataa Mungu na kuomba wapewe mfalme.]
8Tangu nilipowatoa Misri, wameniacha mimi, wamekuwa wakiitumikia miungu mingine mpaka leo. Sasa hayo matendo ambayo wamekuwa wakinitendea mimi, ndiyo wanayokutendea na wewe.
9Basi, wasikilize, lakini, waonye vikali, na waeleze waziwazi jinsi mfalme atakayewatawala atakavyowatendea.”
10Kwa hiyo, Samueli akawaambia wale watu waliokuwa wanaomba wapewe mfalme maneno yote ya Mwenyezi-Mungu.
11Samueli aliwaambia, “Hivi ndivyo mfalme wenu atakayewatawala atakavyowatendea: watoto wenu wa kiume atawafanya wawe waendeshaji wa magari yake, na wengine kuwa wapandafarasi wake, na wengine watapiga mbio mbele ya magari yake.[#8:11-18 Samueli anawakumbusha watu hasara na matatizo yatakayowapata kutokana na kutawaliwa na mfalme wa kibinadamu.]
12Atajichagulia wengine wawe makamanda wa vikosi vyake vya maelfu na wengine wawe makamanda wa vikosi vya watu hamsinihamsini. Atawafanya wengine wamlimie mashamba yake na kuvuna mazao yake. Atawafanya wengine pia wamtengenezee zana za vita, na wengine wamtengenezee vipuli vya magari yake.
13Binti zenu atawachukua kuwa watengenezaji marashi, wengine wapishi na wengine waokaji mikate.
14Atayachukua mashamba yenu mazuri, mashamba ya mizeituni, na mashamba ya mizabibu na kuwapa watumishi wake.
15Atachukua sehemu ya kumi ya nafaka zenu na ya zabibu zenu na kuwapa maofisa wake na watumishi wake.
16Atachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike na ng'ombe wenu wazuri na punda wenu wazuri kabisa na kuwafanya wamfanyie kazi zake.
17Atachukua sehemu ya kumi ya kondoo wenu. Na nyinyi wenyewe mtakuwa watumwa wake.
18Wakati huo, nyinyi mtalalamika kwa sababu ya mfalme wenu ambaye mmejichagulia nyinyi wenyewe. Lakini Mwenyezi-Mungu hatawajibu.”
19Hata hivyo watu walikataa kumsikiliza Samueli, wakasema, “La! Sisi tutakuwa na mfalme juu yetu,
20ili nasi pia tuwe kama mataifa mengine. Mfalme wetu, atatuhukumu, atatuongoza na kutupigania vita vyetu.”
21Samueli alipokwisha sikiliza kila kitu walichosema, akaenda na kumweleza Mwenyezi-Mungu.
22Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Wasikilize na wapatie mfalme.” Kisha Samueli akawaambia Waisraeli warudi nyumbani, kila mtu mjini kwake.