1 Timotheo 1

1 Timotheo 1

1Mimi Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo tumaini letu,[#1:1-2 Barua hii, kama kawaida ya barua za nyakati hizo, inaanza na kujitambulisha kwa mwandishi na salamu. Taz Rom 1:1-7 maelezo.]

2nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani.[#1:2 Msaidizi wa karibu sana katika huduma za Paulo za kuhubiriIinjili. Taz utangulizi na Mate 16:1 maelezo; Fil 2:22; 2Tim 1:2.]

Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu.

Maonyo kuhusu mafundishoya uongo

3Napenda ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao.[#1:3 Safari hiyo ya Paulo kwenda Makedonia wakati Timotheo yuko Efeso haitajwi katika habari tunazopewa katika Matendo ya Mitume.]

4Waambie waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani.[#1:4 Ni nini hasa ilihusika katika hizo hadithi tupu (Kigiriki “miythos”) na orodha za mababu haijulikani. Labda ilihusu mapokeo fulani juu ya wazee wa historia ya Biblia. Iwe iwavyo, kadiri ya Paulo hivyo havikuwa na faida kwa maisha ya kiroho (Tito 1:13-14).; #1:4 Au, “huleta maswali”, hapa kwa maana mbaya.]

5Shabaha ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na imani ya kweli.

6Watu wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana.

7Wanapenda kuwa waalimu wa sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo wanayosisitiza.

8Twajua kwamba sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo.

9Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na dini na wa kidunia, watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale;[#1:9-10 Orodha hii ya vitendo vya ufisadi inafuata karibu moja kwa moja mpango wa orodha ya amri kumi hasa zile zinazohusu uhusiano kati ya watu (Kut 20:12-16).]

10sheria imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wezi wa watu, waongo na wanaoapa uongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho sahihi.[#1:10 Kitendo hiki ni mojawapo ya vitendo vinavyoorodheshwa katika aya 9-10. Baadhi ya wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu wanafikiri hapa vitendo kama vile kuwateka nyara watu na kuwafanya watumwa vinahusika. Wengine wanafikiri Paulo anasema juu ya kuiba mtoto au kumteka nyara mtu na kumweka kwa nguvu bila hiari yake. Taz pia Kut 21:16 na Kumb 24:7 (kuhusu orodha hii ya vitendo vya ufisadi tazama pia Rom 1:31).; #1:10 Msemo wa kawaida katika barua za Paulo zijulikanazo kama za kichungaji (1Tim 6:3; 2Tim 1:13; 4:3; Tito 1:9; 2:1) ambao maana yake ni “mafundisho safi” ambayo hayakuchangayika na uongo au kuwa na dosari yoyote.]

11Mafundisho hayo hupatikana katika injili ya Mungu mtukufu na mwenye heri ambayo mimi nimekabidhiwa niihubiri.[#1:11 Msemo huu unatumika kuwataja watu walioneemeshwa na Mungu; ni tafsiri ya neno la Kigiriki “makarios” ambalo linatumika katika zile heri zinazotajwa katika Mat 5:3-12. Pale linatumiwa kuhusu watu. Ni hapa tu na katika 1Tim 6:15 ambapo linatumiwa kwa Mungu na si dhahiri kwa maana ipi. Lakini, kutokana na mazingira haya ya maandishi ambapo limetumika pamoja na neno “tukufu”, tunaweza kuona hapa wazo kwamba Mungu anatajwa hivyo kwa sababu yeye ndiye hasa anayestahili “kusifiwa”.]

Shukrani kwa ajili ya huruma ya Mungu

12Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie,

13ingawa pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa ninafanya.

14Lakini Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika kuungana na Kristo Yesu.

15Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote,[#1:15 Namna hii ya kusema inatumika tu katika barua hizi zijulikanazo kama za kichungaji (rejea 1Tim 3:1; 4:9; 2Tim 2:11; Tito 3:8).; #1:15 Luka 5:32.]

16lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aoneshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uhai wa milele.

17Kwake yeye aliye Mfalme wa milele, asiyekufa, asiyeonekana na aliye Mungu pekee — kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina.

18Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana vita vizuri,[#1:18 Yamkini wakati alipowekwa wakfu kwa ajili ya kuihubiri Injili (1Tim 4:14).; #1:18-20 Aya hizi tatu zinamalizia sura hii ya kwanza na Timotheo anatajwa tena hapa kama mwanzoni, ila sasa anatiwa moyo aendelee kuwa imara katika imani. Msamiati wa vita unatumiwa mara kwa mara katika A.J. kuonesha mapambano ya Kiristo dhidi ya uovu (rejea 1Tim 6:12; 2Tim 4:7; Yuda 3; taz pia Efe 6:10-17; Fil 2:25; 1Thes 5:8).]

19na ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na hivyo wakaiharibu imani yao.

20Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.[#1:20 Kuna mtu anayetajwa kwa jina hilo katika 2Tim 2:17. Kama ni huyo huyo, basi tunaweza pia kusema aliyofundisha: yaani ufufuo ni jambo lililokwisha tukia (2Tim 2:17-18).; #1:20 Labda ni yule yule anayetajwa katika 2Tim 4:14. Inasemekana kwamba alimtendea Paulo vibaya sana lakini hatuambiwi kwa vipi.; #1:20 Itakumbukwa kwamba katika 1Kor 5:5 Paulo anatumia maneno hayo hayo ya hukumu. Yahusu basi, kuwatenga hao kutoka jumuiya ya waamini au Kanisa.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania