The chat will start when you send the first message.
1Kwanza kabisa, nawasihi muombe dua, msali na kumshukuru Mungu kwa ajili ya watu wote,[#2:1-4 Shukrani na sala Paulo anazowataka waamini watoe zina hadhi ya wakati wote na mahali pote ulimwenguni. Kanisa lilihitaji sana mazingira ya utulivu ili kuweza kuendelea na ufundishaji wa Habari Njema; kwa hiyo watawala pia wanaombewa. Kuhusu fikira za Paulo kuhusu wakuu wa serikali tazama Tito 2:12; 3:1.]
2kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema.[#2:2 Neno “uchaji” (wa Mungu) linatumika mara nyingi katika hizi barua zinazojulikana kama za kichungaji (1Tim 2:2; 3:16; 4:7-8; 6:3,5-6,11; taz pia 2Tim 3:5,12; Tito 2:3,12; 1Pet 1:17; 3:2; 2Pet 1:3,6-7; 3:11). Hili ni jambo la kutazamiwa katika barua ambazo kwa wingi zina shabaha ya kuwaongoza waamini wote kuhusu namna ya kuishi katika mazingira yao ambayo mengine ni magumu.]
3Jambo hili ni jema na lampendeza Mungu Mwokozi wetu,
4ambaye anataka watu wote waokolewe na wapate kuujua ukweli.
5Maana yuko Mungu mmoja, na pia yuko mmoja anayewapatanisha watu na Mungu, binadamu Kristo Yesu,[#2:5 Aya hii yaonekana kutumia maneno ambayo huenda yalikuwa tamko la imani ya waamini wa kale. Rejea Ebr 8:6; 9:15; 12:24. “Yuko Mungu mmoja” rejea Kumb 6:4 sehemu ambayo inagusiwa pia katika Rom 3:30.]
6ambaye alijitoa mwenyewe kuwakomboa watu wote. Huo ulikuwa uthibitisho, wakati ufaao ulipowadia, kwamba Mungu anataka kuwaokoa watu wote.[#2:6 Taz Mat 20:28 maelezo, na rejea Marko 10:45; Gal 1:4; Tito 2:14.]
7Kwa sababu hiyo mimi nilitumwa niwe mtume na mwalimu wa watu wa mataifa, niutangaze ujumbe wa imani na ukweli. Nasema ukweli; sisemi uongo!
8Basi, popote mnapokutana kufanya ibada nataka wanaume wasali, watu waliojitolea kweli na ambao wanaweza kuinua mikono yao wakisali bila hasira wala ubishi.[#2:8 Namna ya kawaida ya Wayahudi kusali ambayo pia imechukuliwa na Wakristo.]
9Hali kadhalika, nawataka wanawake wawe wanyofu na wenye busara kuhusu mavazi yao; wavae sawasawa na si kwa urembo wa mitindo ya kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa,[#2:9-10 Rejea 1Pet 3:3-4. Hapa msomaji lazima afikirie pia desturi za jumuiya nyakati hizo ili kuweza kumwelewa mwandishi ipasavyo, na kuona kwamba kama desturi za nyakati hizo sasa zitakuwa zimepitwa na wakati.]
10bali kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wamchao Mungu.
11Wanawake wanapaswa kukaa kimya na kuwa wanyenyekevu wakati wa kujifunza.[#2:11-12 Kuhusu maagizo ya aya hizi taz 1Kor 11:2-16 maelezo na pia 14:34-35 maelezo.]
12Mimi simruhusu mwanamke amfundishe au amtawale mwanamume; anapaswa kukaa kimya.
13Maana Adamu aliumbwa kwanza, halafu Hawa.
14Na wala si Adamu aliyedanganywa; bali mwanamke ndiye aliyedanganywa, akaivunja sheria ya Mungu.
15Hata hivyo, mwanamke ataokolewa kwa kupata watoto, kama akidumu katika imani, upendo, utakatifu na unyofu.[#2:15 Yamkini hapa mwandishi anatilia mkazo kuwa kuoa na mama kupata watoto ni jambo jema, kupinga fikra nyingine za wakati huo kwamba kuoa ni makosa. Rejea 1Tim 4:3. Hii ni sehemu ngumu karibu kuliko zote za Biblia. Ama kweli hakuna mahali katika Biblia ambapo jambo hilo linasemwa.]