The chat will start when you send the first message.
1Watumwa wote wanapaswa kuwaheshimu wakuu wao ili kusiwe na sababu ya watu kulitukana jina la Mungu na mafundisho yetu.[#6:1-2 Tito 2:9-10; 1Pet 2:18; rejea Efe 6:5-9. Kol 3:22—4:1. Utumwa ulikuwa kitu cha kawaida kwa watu wa nyakati hizo huko Mashariki ya Kati. A.J. lafundisha kwamba kwake Kristo hakuna mtumwa wala mtu huru (Gal 3:28; Efe 6:8; Kol 3:11) na kwamba sote tunapaswa kumtumikia jirani kwa upendo (rejea Mat 20:25-28 na sehemu sambamba). Katika Kol 3:22 watumwa wanahimizwa watumikie kwa uaminifu na mabwana zao wawatendee watumwa wao kwa haki na usawa. Walau kwa kusema hivyo, ukatili ule tunaoujua kuhusu watumwa haukubaliki katika A.J.]
2Watumwa ambao wakuu wao ni Wakristo wasiwadharau kwani ni ndugu zao. Badala yake, wanapaswa kuwatumikia hata vizuri zaidi, maana hao wanaopata faida kutokana na kazi yao ni waumini ambao wanawapenda.
Unapaswa kufundisha na kuhubiri mambo haya.
3Mtu yeyote anayefundisha kinyume cha mambo haya, na ambaye hakubaliani na maneno ya kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo na mafundisho ya uchaji wa Mungu,[#6:3 Au, “Mafundisho yaliyonyooka”; au, “mafundisho safi”. Tazama 1Tim 1:10.]
4huyo amejaa majivuno na wala hajui chochote. Ni mtu wa kupenda ubishi na magombano juu ya maneno matupu, na hiyo husababisha wivu, ugomvi, matusi, shuku mbaya,
5na ubishi usio na kikomo kutoka kwa watu ambao akili zao zimeharibika, na ambao hawana tena ukweli. Wanadhani dini ni njia ya kujipatia utajiri.
6Kweli kumcha Mungu humfanya mtu awe tajiri sana, ikiwa anatosheka na vitu alivyo navyo.[#6:6-10 Baada ya Paulo kusema katika aya iliyotangulia kwamba watu wengine walidhani dini ni njia ya kujitajirisha, sasa anachukua nafasi ya kueleza zaidi juu ya hatari za utajiri.; #6:6 Rejea Efe 4:11-12; Ebr 13:5. Sehemu ya pili ya aya hii “ikiwa anatosheka na vitu alivyo navyo” ni muhimu katika kuelewa hoja ya Paulo. Yaani, hali ya mtu kiroho haitegemei mambo ya nje au mali.]
7Maana hatukuleta kitu chochote hapa duniani, wala hatutachukua chochote.
8Kwa hiyo basi, kama tunacho chakula na mavazi, tunapaswa kuridhika navyo.
9Lakini wale wanaotaka kutajirika huanguka katika majaribu, na kunaswa katika mtego wa tamaa nyingi mbaya za kipumbavu, ambazo huwavuta mpaka kwenye uharibifu na maangamizi.
10Kwa maana kupenda sana fedha ni chanzo cha uovu wote. Watu wengine wametamani sana kupata fedha hata wakatangatanga mbali na imani, na wameivunja mioyo yao kwa huzuni nyingi.
11Lakini wewe, mtu wa Mungu, jiepushe na mambo hayo. Zingatia uadilifu, uchaji wa Mungu, imani, upendo, subira na unyenyekevu.[#6:11 Katika A.K. maneno haya yanatumiwa kuwataja watu ambao ni wasemaji wa Mungu, au manabii (Kumb 33:1; 1Fal 12:22; 13:31). Katika A.J. maneno hayo yanatumiwa hapa na katika 2Tim 3:17 kuhusu Timotheo ambaye aliitwa kuhubiri Habari Njema ya Mungu.]
12Piga mbio kadiri uwezavyo katika shindano la mbio za imani, ukajipatie tuzo la uhai wa milele uliloitiwa wakati ulipokiri imani yako mbele ya mashahidi wengi.[#6:12 Wengi wanafikiri tukio hilo lilikuwa wakati ule alipoteuliwa na kuwekwa wakfu kwa ajili ya kuitangaza Injili (rejea 1Tim 1:18-19; 4:14).]
13Mbele ya Mungu anayevipa vitu vyote uhai, na mbele ya Yesu Kristo aliyetoa ushahidi na kukiri ukweli mbele ya Pontio Pilato,[#6:13 Rejea Yoh 18:36-37. Ushahidi alioutoa Yesu si tu maneno aliyotamka, bali pia juu ya uhai wake na kifo chake (taz Ufu 1:2 maelezo).]
14nakuamuru ushike maagizo yako na kuyatii kwa uaminifu mpaka siku ile atakapotokea Bwana wetu Yesu Kristo.
15Kutokea kwake kutafanyika wakati ufaao uliopangwa na Mungu mwenye heri na aliye Mtawala pekee, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.[#6:15 Taz 1Tim 1:11 maelezo.]
16Yeye peke yake anaishi milele katika mwanga usioweza kukaribiwa na mtu. Hakuna mtu aliyepata kumwona au awezaye kumwona. Kwake iwe heshima na uwezo wa milele! Amina.[#6:16 Zab 104:2.; #6:16 Kut 33:20; Yoh 1:18.]
17Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie.[#6:17 Ona jinsi wazo la utajiri (au mali) linavyorudi tena na tena kwa maana tofauti tofauti katika sehemu hii ya aya 17-19.]
18Waamuru watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, na wawe wakarimu na walio tayari kuwashirikisha wengine mali zao.
19Kwa namna hiyo watajiwekea hazina ambayo itakuwa kwao msingi imara kwa wakati ujao. Hapo wataweza kujipatia uhai ambao ni uhai wa kweli.
20Timotheo, tunza salama yote yale uliyokabidhiwa. Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ubishi wa kipumbavu juu ya kile wanachokiita watu wengine “Elimu.”[#6:20 Yaani imani na ukweli wa Habari Njema (rejea 2Tim 1:14 na Kol 4:17).; #6:20 Labda yahusu mafundisho ambayo yalihusu ujuzi fulani wa pekee. Mafundisho hayo yalizuka nyakati hizo na kuenea mahali pengi mnamo karne ya pili B.K.]
21Maana wengine wamejidai kuwa na hiyo elimu, na matokeo yake wamepoteza imani.[#6:21 1Tim 1:6; 4:1-5; 2Tim 2:18.]
Nawatakieni nyote neema!