The chat will start when you send the first message.
1Miaka ishirini, ambayo Solomoni aliijenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu ilipokwisha kupita,
2Solomoni aliijenga upya miji aliyopewa na Huramu, halafu akawapa Waisraeli miji hiyo waishi humo.[#8:2 Katika 1Fal 9:10-14 Solomoni alimpa Huramu miji hii kama malipo kwa ajili ya miti na dhahabu aliyopokea kutoka Tiro, lakini Huramu aliikataa kwa sababu ilikuwa katika hali duni mno.]
3Baadaye Solomoni alielekea Hamath-zoba na kuuteka,
4na kuujenga mji wa Tadmori nyikani. Aliijenga upya miji ya ghala iliyokuwa huko Hamathi.
5Kadhalika, Solomoni alijenga miji ifuatayo: Beth-horoni wa juu, na Beth-horoni wa chini, miji yenye ngome, kuta, malango na makomeo,[#8:5 Miji mingi ya wakati huo ilikuwa imezungushiwa ukuta na kuwa na lango moja au mawili ya kuingia ndani. Mtindo huo wa kujenga miji ulikuwa kwa ajili ya kujihami na maadui. Eneo karibu na malango hayo lilitumika aghalabu kwa ajili ya kutatua mizozo ya watu.]
6mji wa Baalathi, na miji yake yote ya ghala, magari yake ya kukokotwa na ya wapandafarasi wake, na chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, Lebanoni au kwingineko katika ufalme wake.
7Watu wengine wote waliobaki miongoni mwa Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, yaani wote ambao hawakuwa Waisraeli,[#8:7-9 Watu hawa wote ndio waliokuwa wakazi wa awali wa Kanaani, kabla ya Waisraeli kuingia humo.]
8pia wazawa wao ambao Waisraeli hawakuwaangamiza, Solomoni aliwafanyiza kazi za kulazimishwa, na hivi ndivyo wanavyofanya hata sasa.
9Lakini kati ya watu wa Israeli, Solomoni hakumfanya mtu yeyote kuwa mtumwa kwa ajili ya kazi yake; wao walikuwa askari, makamanda wa maofisa wake, makamanda wa magari yake ya kukokotwa na wapandafarasi wake.
10Ifuatayo ndiyo jumla ya maofisa wakuu wa mfalme Solomoni: walikuwa 250, waliokuwa na mamlaka juu ya watu.
11Solomoni alimhamisha binti Farao mfalme wa Misri, kutoka mji wa Daudi, akampeleka kwenye nyumba aliyomjengea. Alisema, “Mke wangu hataishi katika nyumba ya Daudi mfalme wa Israeli, kwa maana mahali pote ambapo sanduku la Mwenyezi-Mungu limekuwa, ni patakatifu.”
12Solomoni alimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za kuteketeza juu ya madhabahu aliyokuwa amemjengea Mwenyezi-Mungu mbele ya ukumbi wa hekalu.[#8:12-13 Kutambikia au kumtolea Mungu sadaka ilikuwa ni wadhifa wa makuhani au makasisi wa Israeli, lakini hapa Solomoni anatekeleza wadhifa huo.]
13Alitoa tambiko hizo kadiri ilivyotakiwa na amri ya Mose kila siku takatifu, yaani siku za Sabato, sikukuu za mwezi mwandamo, na sikukuu tatu za kila mwaka — sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, sikukuu ya majuma na sikukuu ya vibanda.
14Akifuata maagizo ya Daudi baba yake, alipanga zamu za kila siku za makuhani na za Walawi waliowasaidia makuhani kusifu na kuzitekeleza kazi zao. Kadhalika aliwapanga walinda malango katika makundi aliyoyaweka kulinda kila lango; maana ndivyo alivyoamuru Daudi, mtu wa Mungu.[#8:14 Maneno hayo yanatumiwa tu hapa katika Biblia kuhusu Daudi. Kwa kawaida katika vitabu vya Wafalme, maneno “mtu wa Mungu” yanatumiwa kuwataja manabii, na mara chache sana katika vitabu vya Mambo ya Nyakati ambapo yanatumiwa mara kadhaa kwa Mose (Kumb 33:1; Yos 14:6; 1Nya 23:14 n.k.), kwa Daudi (hapa) na kwa kumtaja nabii mmoja asiyejulikana (2Nya 25:2-9).]
15Nao hawakuyaacha maagizo mfalme aliyowaamuru makuhani na Walawi jambo lolote na kuhusu hazina.
16Basi miradi yote ya Solomoni aliyofanya tangu jiwe la msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu lilipowekwa ilikamilika. Hivyo nyumba ya Mwenyezi-Mungu ilimalizika.
17Kisha Solomoni alikwenda Esion-geberi na Elothi iliyo pwani mwa bahari, katika nchi ya Edomu.
18Huramu alimpelekea merikebu zilizokuwa chini ya uongozi wa maofisa wake, pamoja na mabaharia stadi. Hao, pamoja na maofisa wa Solomoni, walisafiri hadi Ofiri, na kuchukua kutoka huko dhahabu, wakamletea mfalme Solomoni kiasi cha kilo 15,000.[#8:18 Yamkini mahali panapohusika ni Afrika ya Kaskazini; wengine wanafikiri ni eneo la Arabia kusini.]