The chat will start when you send the first message.
1Maana tunajua kwamba hema hii ambamo tunaishi sasa hapa duniani yaani mwili wetu, itakapong'olewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono.[#5:1-5 Katika sehemu hii Paulo anatueleza juu ya hali ya maisha yajayo ya uhai pamoja na Mungu kwa kutumia picha za mifano ya maisha hapa duniani: mwili wa duniani, mwili wa mbinguni; hema la shambani ambalo ni la muda tu na hema la mbinguni ambalo ni la milele. Paulo alikwisha tumia namna hii ya kueleza ukweli wa mambo ya kiroho hasa kuhusu ufufuo katika 1Kor 15:37-49.]
2Na sasa, katika hali hii, tunaugua tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni.
3Naam, tunapaswa kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi.[#5:3 Paulo anaendelea na picha ya kueleza hayo mabadiliko muhimu ya makao ya duniani na ya mbinguni (aya 2) kwa picha nyingine ya mfano: vazi la mbinguni. Mungu atafanya mabadiliko thabiti kuhusu miili yetu yenye kufa (taz 4:11).]
4Tukiwa bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile chenye kufa kimezwe kabisa na uhai.
5Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea.[#5:5 Taz maelezo ya 2Kor 1:22 na ling na Rom 8:23; Efe 1:13.]
6Tuko imara daima. Tunajua kwamba kuishi katika mwili huu tu ni kukaa mbali na Bwana.
7Maana tunaishi kwa imani, na si kwa kuona.
8Lakini tuko imara na tungependelea hata kuyahama makao haya, tukahamie kwa Bwana.
9Lakini jambo la maana zaidi, tunataka kumpendeza, iwe tunaishi hapa duniani au huko.
10Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya.[#5:10 Au, “kwa mwili wake”.]
11Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga.[#5:11 Ling 2Kor 3:1; Paulo anarudia wazo lile lile.]
12Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa nyinyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni.
13Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu.[#5:13 Ling Mate 26:24.]
14Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake.[#5:14 Yaani Kristo.]
15Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao.
16Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu. Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena.[#5:16 Bila shaka yahusu fikra alizokuwa nazo Paulo juu ya Yesu Kristo kabla ya kuongoka kwake; yaani kama Masiha wa uongo; lakini sasa anamtambua kama Bwana aliyefufuka, kiini au kitovu cha kiumbe kipya (5:17).]
17Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika.[#5:17 Gal 6:15; Tito 3:5; 1Pet 1:3,23. Kiumbe kipya au, mtu mpya.]
18Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo, na kutupa jukumu la kuwapatanisha watu naye.[#5:18-20 Taz Efe 2:12-16; Kol 1:20-22. Kadiri ya fikra za Wagiriki, Mungu akiwa adui wa watu, ni wao wenyewe ambao wanapaswa kutafuta tena urafiki naye. Lakini Paulo, akichota mawazo yake kutoka A.K., anaona kwamba watu wanahitaji kupatanishwa, na anatamka kwamba Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwezesha upatanisho huo kwa njia ya Kristo. Binadamu inawabidi kupokea zawadi hiyo.]
19Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye.
20Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi nyinyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu.
21Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki uadilifu wake Mungu.[#5:21 Neno kwa neno: alimfanya dhambi. Kwa maana ya au (1) Mungu alimfanya kuwa kafara ya kuondoa dhambi (rejea Lawi 4:27-35); au (2) kwamba Yesu mwenyewe bila kutenda dhambi yeye mwenyewe alifananishwa na dhambi.]