2 Yohane 1

2 Yohane 1

1Mimi mzee nakuandikia wewe Bimkubwa mteule pamoja na watoto wako ninaowapenda kweli. Wala si mimi tu ninayewapenda, bali pia wote wanaoujua ule ukweli wanawapenda nyinyi,[#1 Jina linalotumika hapa na pengine katika A.J. kuwataja watu ambao walikuwa na wadhifa au madaraka fulani katika jumuiya ya waumini wa mahala fulani (Mate 11:30). Hapa mwandishi analitumia kujitaja yeye mwenyewe.; #1 Hapa yahusu jumuiya yote iliyoteuliwa na Mungu na ambayo mwandishi anaitaja hapa kwa picha hiyo ya kimfano (rejea aya 13; 1Pet 5:13).]

2kwa sababu ukweli unakaa nasi milele.

3Neema na huruma na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika ukweli na upendo.

Ukweli na upendo

4Nilifurahi sana kuona kwamba baadhi ya watoto wako wanaishi katika ukweli kama Baba alivyotuamuru.[#4 3Yoh 3.]

5Basi, Bimkubwa, ninalo ombi moja kwako: tupendane. Ombi hili si amri mpya, bali ni amri ileile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo.[#5 Yoh 13:34; 15:12,17; 1Yoh 3:11,23; 4:7,11.; #5 1Yoh 2:7; 3:11.]

6Upendo maana yake ni kuishi kwa kuzitii amri zake Mungu. Amri mliyoisikia tangu mwanzo ndiyo hii: mnapaswa nyote kuishi katika upendo.

7Wadanganyifu wengi wamezuka duniani, watu ambao hawakiri kwamba Yesu Kristo amekuja kwetu, na mwili wa kibinadamu. Mtu asemaye hivyo ni mdanganyifu na ni mpinzani wa Kristo.[#7 1Yoh 2:18,22-23; 4:1-3; ling Mat 7:15. Kuhusu kukana kwamba Yesu Kristo alikuja kwetu katika mwili wa kibinadamu, taz 1Yoh 4:2 na pia utangulizi wa barua hiyo.]

8Basi, jihadharini nyinyi wenyewe ili msije mkapoteza kile mlichokishughulikia, bali mpate tuzo lenu kamili.

9Asiyezingatia na kudumu katika mafundisho ya Kristo, bali anayakiuka, hana Mungu. Lakini anayedumu katika mafundisho hayo anaye Baba na Mwana.[#9 1Yoh 2:22-24; 4:15.]

10Basi, kama mtu akija kwenu bila kuwaleteeni mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani kwenu, wala msimsalimu.[#10-11 Yahusu watu walioitembelea jumuiya ya Wakristo wakifundisha mafundisho tofauti na yale ya kweli wakitumaini kutambuliwa kama waalimu, na kutumia vibaya makaribisho waliyopewa na kanisa la hapo. Rejea Gal 1:7-9 ambapo lugha inayotumika ni kama hii hapa.]

11Maana anayemsalimu mtu huyo, anashirikiana naye katika matendo yake maovu.

Hatima

12Ninayo mengi ya kuwaambieni, lakini sipendi kufanya hivyo kwa karatasi na wino; badala yake, natumaini kuwatembeleeni na kuzungumza nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ikamilike.

13Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu.[#13 Taz 2Yoh 1 maelezo. Neno “Dada” linatumika bila shaka kimfano na yahusu kanisa ambalo mwandishi anaandika Barua hii kutoka huko; baadhi wanafikiri lilikuwa kanisa la Efeso.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania