2 Wafalme 19

2 Wafalme 19

Mfalme aomba shauri kwa Isaya

(Isa 37:1-7)

1Mfalme Hezekia alipopata habari hizo, alirarua mavazi yake, akavaa gunia akaingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

2Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia.[#19:2 Nabii Isaya anatajwa hapa kwa mara ya kwanza katika vitabu vya 1 na 2 Wafalme. Yapata miaka arubaini kabla ya wakati huu, nabii Isaya alikuwa ameanza kuwaletea watu wa Yuda ujumbe wa Mungu wa hukumu na matumaini. Huo ulikuwa wakati wa mfalme Azaria. Isaya anatajwa katika 2Nya 26:22 kama mwandishi wa historia ya mfalme Azaria (aitwaye pia Uzia).]

3Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama ambaye anataka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa.

4Inawezekana Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya jemadari mkuu, ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai; naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atakaripia maneno aliyosikia. Kwa hiyo waombee watu waliobaki.’”[#19:4 Jambo la kuwataka ushauri manabii wakati wa vita au matatizo ya kitaifa lilikuwa la kawaida katika A.K. (1Fal 22:6-23; 2Fal 3:11; Yer 21:1-2).]

5Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya,

6aliwaambia “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Usiogope kwa sababu ya maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wameyasema kunikebehi.

7Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi, halafu atarudi katika nchi yake na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’”

Tisho jingine la Waashuru

8Kisha yule jemadari mkuu aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akiushambulia mji wa Libna.

9Halafu mfalme alipopata habari kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi anakuja kupigana naye, alituma wajumbe kwa Hezekia, akisema,[#19:9 “Tirhaka” alitawala mwaka 689-664 K.K. Na kuhusu “Kushi” ni jina linalotumika mara kwa mara kutaja sehemu ya Afrika Kaskazini, kusini mwa Misri, sehemu inayojumuisha nchi za Ethiopia, Eritrea, Sudani na sehemu za jirani. Tafsiri ya Septuajinta (LXX) ina: “Taraka mfalme wa Ethiopia”. Lakini, kwa ukubwa na eneo, Ethiopia ya wakati ule si sawa na Ethiopia ya sasa.]

10“Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda, ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba mji wa Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru.

11Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, wadhani wewe utaokoka?

12Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, na Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo babu zangu waliyaangamiza?

13Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na wa Iva?’”[#19:12-13 Orodha ya miji inayotajwa hapa ina shabaha ya kumfanya mfalme Hezekia atambue uwezo na nguvu ya Ashuru juu ya mataifa mengine ya huko Mesopotamia na pia Siria.]

14Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akaiweka mbele yake Mwenyezi-Mungu.

15Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, unayekaa katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa, ni wewe tu uliye Mungu, unayetawala falme zote za ulimwengu. Wewe uliumba nchi na mbingu.[#19:14-15 Viumbe viwili vyenye mabawa ambavyo vilitengenezwa kwa dhahabu viliwekwa juu ya sanduku la agano na vilikuwa mfano au ishara ya kiti cha enzi cha Mwenyezi-Mungu duniani (Kut 25:18-22; 2Sam 6:2). Sanamu za aina hizo ziliitwa pia “Makerubi”. Makerubi mengine yanaelezwa kwamba yana sura ya mtu, simba, tai au ng'ombe (Mwa 3:24; Eze 1:10; 10:12-14; 41:18-20).]

16Ee Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka kukutukana wewe Mungu uliye hai.

17Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa na nchi zao.

18Walitupa miungu yao motoni kwa sababu haikuwa miungu ya kweli, bali sanamu za miti na mawe zilizochongwa na mikono ya watu.

19Sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, nakusihi utuokoe makuchani mwa Senakeribu, falme zote za dunia zijue kwamba ni wewe peke yako, ee Mwenyezi-Mungu, uliye Mungu.”

Ujumbe wa Isaya kwa mfalme

(Isa 37:21-38)

20Kisha Isaya, mwana wa Amozi akatuma ujumbe kwa Hezekia, akisema, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ‘Nimesikia ombi lako kwangu kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru:’

21Hili ndilo neno la Mwenyezi-Mungu alilosema kumhusu Senakeribu:

Anakudharau, anakubeza binti Siyoni,

anatikisa kichwa chake nyuma yako binti Yerusalemu.

22Je, uliyekuwa unamkashifu na kumdhihaki ni nani?

Nani umemwinulia sauti

na kumkodolea macho kwa kiburi?

Juu ya Mtakatifu wa Israeli!”

23Kwa kuwatuma wajumbe wako umemkashifu Bwana,

wewe umesema, “Kwa magari yangu mengi ya vita,

nimekwea vilele vya milima

mpaka kilele cha Lebanoni.

Nimekata mierezi yake mirefu,

na misonobari mizurimizuri;

nimeingia mpaka ndani yake

na ndani ya misitu yake mikubwa.

24Nimechimba visima

na kunywa maji mageni

nilikausha mito yote ya Misri

kwa nyayo za miguu yangu.

25‘Je, hujasikia,

kwamba nilipanga jambo hili tangu awali?

Ninachotekeleza sasa nilikipanga zamani.’

Nilikuweka uijenge miji yenye ngome

kwa rundo la magofu.

26Wakazi wake wakiwa wameishiwa nguvu,

wametishika na kufadhaika,

wamekuwa kama mimea ya shambani,

kama majani yasiyo na nguvu.

Kama majani yaotayo juu ya paa;

yakaukavyo kabla ya kukua.

27Najua kuketi kwako,

na kuamka kwako

nako kuingia kwako;

nayo mipango yako dhidi yangu.

28Kwa vile umefanya mipango dhidi yangu

na nimeusikia ufidhuli wako,

nitatia ndoana yangu puani mwako,

na lijamu yangu kinywani mwako.

Nitakurudisha njia ileile uliyojia.”

29Kisha Isaya akamwambia mfalme Hezekia, “Na hii ndio itakuwa ishara kwako Hezekia: mwaka huu na mwaka ujao mtakula kinachomea chenyewe bila kupandwa. Lakini katika mwaka wa tatu mtapanda na kuvuna mavuno; mtapanda mizabibu na kula matunda yake.[#19:29 Kwa kawaida katika nchi hizo wakulima walipovuna, mbegu nyingine zilianguka chini na kuota, hivyo kwamba msimu uliofuata kulikuwa na mavuno ambayo hayakupandwa na watu lakini yalikuwa kidogo na hafifu. Kwa namna hiyo Mungu anawatayarisha watu kwa nyakati ngumu (za vita) kwa miaka miwili ambapo hawataweza kupanda mazao lakini watapata chakula. Na kwa upande mwingine anawapa tumaini: mwaka wa tatu watapanda na kuvuna.]

30Wale watakaobaki katika ukoo wa Yuda wataongezeka na kuwa wengi kama vile mti unavyotoa mizizi yake udongoni na kuzaa matunda juu.

31Maana kutakuwako watu watakaosalia huko Yerusalemu; naam, huko mlimani Siyoni kutakuwako watu wachache watakaosalimika; maana Mwenyezi-Mungu amedhamiria kukamilisha hayo.

32“Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya mfalme wa Waashuru: ‘Hataingia katika mji huu wala kuupiga mshale wala kuujia kwa ngao wala kuuzingira.

33Atarudi kwa njia ileile aliyoijia na wala hataingia katika mji huu,’ ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu.

34‘Naam, kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi nitaulinda na kuokoa mji huu.’”

35Basi, usiku huo malaika wa Mwenyezi-Mungu aliingia kambini mwa Waashuru na kuwaua watu laki moja. Kulipopambazuka watu wakaamka, hao wote walionekana wakiwa maiti.

36Kisha Senakeribu mfalme wa Ashuru aliondoka akaenda zake na kukaa Ninewi.[#19:36-37 Huyu aliuawa miaka ishirini baadaye katika mwaka 681 K.K.]

37Siku moja wakati Senakeribu alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki mungu wake, wanawe wawili, Adrameleki na Sharezeri walimuua kwa upanga, halafu wakakimbilia nchini Ararati. Naye Esar-hadoni, mwanawe akatawala badala yake.[#19:37 Huyu alitawala Ashuru mwaka 681-669 K.K.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania