The chat will start when you send the first message.
1Nakuamuru mbele ya Mungu, na mbele ya Kristo Yesu atakayewahukumu watu walio hai na wafu, na kwa sababu anakuja kutawala akiwa Mfalme:[#4:1 Taz Mate 10:42; 1Pet 4:5.]
2hubiri huo ujumbe, sisitiza kuutangaza (iwe ni wakati wa kufaa au wakati usiofaa), karipia, onya na himiza watu ukiwafundisha kwa uvumilivu wote.
3Utakuja wakati ambapo watu hawatasikiliza mafundisho ya kweli, ila watafuata tamaa zao wenyewe na kujikusanyia waalimu tele watakaowaambia mambo yale tu ambayo masikio yao yako tayari kusikia.
4Watakataa kuusikia ukweli, watageukia hadithi za uongo.
5Wewe, lakini, uwe macho katika kila hali; vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Habari Njema, timiza kikamilifu utumishi wako.
6Kwa upande wangu mimi, niko karibu kabisa kutolewa tambiko na wakati wa kufariki kwangu umefika.[#4:6 Au, neno kwa neno, “mimi sasa namiminwa”, picha ya kutolewa kafara.; #4:6 Tangu aya hii mpaka mwishoni mwa hii Barua mambo mengi yanajitokeza ambayo yanatupa picha ya mazingira ya Paulo gerezani kule Roma.]
7Nimefanya bidii katika mashindano, nimemaliza safari yote na imani nimeitunza.[#4:7 Mwandishi anatumia picha mbili kuelezea shughuli za mwaamini wa Kristo: vita (rejea 1Tim 1:18-19; 6:12), na mashindano katika riadha (rejea Mate 20:24; 1Kor 9:24; Ebr 12:1).; #4:7 Kwa maana ya kutekeleza kila kitu kinachotakiwa kwa mtu anayemwamini Kristo na hata kutangaza hayo kwa uaminifu (1Tim 6:14).]
8Na sasa imebakia tu kupewa tuzo la ushindi kwa maisha ya uadilifu, tuzo ambalo Bwana, Hakimu wa haki, atanipa mimi siku ile, na wala si mimi tu, ila na wale wote wanaotazamia kwa upendo kutokea kwake.[#4:8 Au, neno kwa neno: “taji ya uadilifu”. Yaweza pia kueleweka kama tuzo kwa maisha ya uadilifu.]
9Fanya bidii kuja kwangu karibuni.
10Dema ameupenda ulimwengu huu akaniacha na kwenda zake Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia, na Tito amekwenda Dalmatia.[#4:10 Kol 4:14; File 24.; #4:10 Anatajwa hapa tu.; #4:10 Mkoa wa utawala wa Waroma katika Asia Ndogo.; #4:10 2Kor 8:23; Gal 2:3; Tito 1:4.; #4:10 Sehemu ya Kusini ya mkoa wa Waroma wa Iluriko; eneo hili ndilo lililokuwa Yugoslavia ya zamani (Rom 15:19).]
11Luka peke yake ndiye aliye hapa pamoja nami. Mpate Marko uje naye, kwa maana ataweza kunisaidia katika kazi yangu.[#4:11 Taz Kol 4:1 na rejea File 24.; #4:11 Mate 12:12,25; 13:13; 15:37-39; Kol 4:10; File 24.]
12Nilimtuma Tukiko kule Efeso.[#4:12 Mate 20:4; Efe 6:21-22; Kol 4:7-8; Tito 3:12.]
13Utakapokuja niletee koti langu nililoacha kwa Karpo kule Troa; niletee pia vile vitabu, na hasa vile vya ngozi.[#4:13 Haijulikani huyu alikuwa nani.; #4:13 Bandari iliyopo Kusini kabisa na Magharibi mwa Asia Ndogo (Mate 16:8-11; 20:5-13; 2Kor 2:12-13).; #4:13 Vitabu hivyo vya papiri (mafunjo) au pengine vya ngozi, vilikuwa vya mviringo au msokoto, kwa Kiswahili cha zamani kidogo “gombo”. Hatujui kama vitabu hivyo vilihusu Maandiko Matakatifu ya kale au vitabu vya maandishi mengine.]
14Yule sonara aitwaye Aleksanda amenitendea maovu mengi; Bwana atamlipa kufuatana na hayo matendo yake.[#4:14 Huyu aweza kuwa ni yule anayetajwa pia katika 1Tim 1:20.; #4:14 Rejea Zab 62:11-12; Meth 24:12; Rom 2:5-6.]
15Jihadhari naye kwa sababu aliupinga ujumbe wetu kwa ukali.
16Wakati nilipojitetea kwa mara ya kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu; wote waliniacha. Mungu asiwahesabie kosa hilo![#4:16 Maneno ambayo yalitumiwa pia na Stefano (Mate 7:60—8:1).]
17Lakini Bwana alikaa pamoja nami, akanipa nguvu, hata nikaweza kuutangaza ujumbe wote, watu wa mataifa wausikie; tena nikaokolewa katika hukumu ya kifo kama kinywani mwa simba.[#4:17 Msemo wa kuelezea hatari ya kifo; rejea Zab 22:21; na pia Dan 6.]
18Bwana ataniokoa na mambo yote maovu, na kunichukua salama mpaka katika ufalme wake wa mbinguni. Kwake uwe utukufu milele na milele! Amina.
19Wasalimu Priska na Akula, pamoja na jamaa ya Onesiforo.[#4:19 Mate 18:2,18. Priska au Priskila ni jina la mtu yuleyule.; #4:19 Tazama 2Tim 1:16-18.]
20Erasto alibaki Korintho, naye Trofimo nilimwacha Mileto kwa sababu alikuwa mgonjwa.[#4:20 Mate 19:22; Rom 16:23.; #4:20 Mate 20:4; 21:29.; #4:20 Bandari pwani ya Bahari ya Ageo, Kusini mwa Efeso.]
21Fanya bidii kuja kabla ya majira ya baridi. Ebulo, Pudensi, Lino na Klaudio wanakusalimu; vilevile ndugu wengine wote.[#4:21 Wakati ambapo haikuwezekana kusafiri baharini.; #4:21 Hao wote wanaopeleka salamu zao ni Wakristo wa Kanisa la Roma.]
22Bwana awe nawe rohoni mwako. Nawatakieni nyote neema.[#4:22 Hati nyingine zinamalizia kwa neno “Amina”.]