The chat will start when you send the first message.
1Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa hekalu pamoja na Masadukayo walifika.[#4:1 Katika Halmashauri au Baraza Kuu la Wayahudi Masadukayo walikuwa na nguvu sana kuhusu maamuzi yake. Masadukayo walikuwa wanachama wa chama cha kidini ambacho kilishikilia kwamba wafu hawafufuki; taz Mat 22:25; Mate 23:6-8 na pia Fahirisi.]
2Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonesha wazi kwamba wafu watafufuka.
3Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake.
4Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu wanaume 5,000.
5Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na waalimu wa sheria walikusanyika pamoja huko Yerusalemu.
6Walikutana pamoja na Anasi kuhani mkuu, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa kuhani mkuu.[#4:6 Huyu alikuwa mwenyekiti wa Baraza au Halmashauri Kuu. Kayafa ndiye aliyekuwa kuhani mkuu rasmi, lakini baba mkwe wake, Anasi, aliendelea kutambuliwa na Wayahudi kuwa pia kuhani mkuu walau kwa jina tu (Luka 3:2).]
7Walipowasimamisha mitume mbele yao, waliwauliza, “Nyinyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?”[#4:7 Swali hilohilo aliulizwa Yesu hekaluni na Halmashauri au Baraza Kuu la Wayahudi (taz Mat 21:23 na sehemu sambamba za Injili).]
8Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, “Viongozi na wazee wa watu!
9Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima,
10basi, nyinyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye nyinyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu.
11Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema:
‘Jiwe mlilokataa nyinyi waashi,
sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.’
12Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.”[#4:12 Hapa pana kile tunachokiita katika utafiti wa lugha: “mchezo wa maneno”, yaani neno lile lile la Kigiriki lina maana mbili hapo papo: “kuokoa na kuponya” (aya 9).]
13Hao wazee wa Baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu.[#4:13 Yaani hawakuwa wamesoma kwa waalimu wa sheria. Yaani walikuwa wanafunzi wake.]
14Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu.
15Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha.
16Wakaulizana, “Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba muujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo.
17Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu.”
18Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu.
19Lakini Petro na Yohane wakawajibu, “Amueni nyinyi wenyewe kama ni sawa mbele ya Mungu kuwatii nyinyi kuliko kumtii Mungu.
20Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia.”
21Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo.
22Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arubaini.
23Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee.
24Nao waliposikia habari hizo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, “Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo![#4:24 Kut 20:11; Neh 9:6; Zab 146:6. Sala ya 4:24-30 inafanana na ile ya mfalme Hezekia katika Isa 37:16-20.]
25Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, baba yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu:
‘Kwa nini mataifa yameghadhibika?
Mbona watu wamefanya mipango ya bure?
26Wafalme wa dunia walijiweka tayari,
na watawala walikutana pamoja,
dhidi ya Bwana na dhidi ya Kristo wake.’
27“Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye ulimweka wakfu.[#4:27 Huyo alikuwa Herode Antipa, mwanawe Herode Mkuu. Alikuwa gavana wa Galilaya tangu mwaka 4 K.K. mpaka 39 B.K. Ingawa makazi yalikuwa Kaisaria alikuwako Yerusalemu wakati Yesu alipokamatwa. Taz Luka 23:6-12. Mat 27:1-2 na sehemu sambamba.; #4:27,30 Taz Mate 3:13 maelezo.]
28Naam, walikutana ili wafanye mambo yale uliyokusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako.
29Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari.
30Nyosha mkono wako ili uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu.”
31Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila woga.[#4:31 Alama au ishara ya kuweko kwake Mungu na kwamba Mungu ameisikia sala yao; angalia Kut 19:18; Isa 6:4.; #4:31 Jambo lililotukia siku ya Pentekoste (Mat 2:2-4).]
32Jumuiya yote ya waumini ilikuwa na moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo.[#4:32 Taz Mate 2:43-47 maelezo.]
33Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi.[#4:33 Yaani nguvu ambayo ilidhihirika katika kutendeka kwa miujiza. Taz 2:22; 3:12; 4:7; 6:8; 8:13; 10:38.]
34Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza
35na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake.
36Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake, “Mtu mwenye kutia moyo”).[#4:36 Mmoja wa watu wa kabila la Lawi, ambalo lilikuwa na jukumu la kutumikia hekaluni. Taz pia Luka 10:32. Walawi hawakuruhusiwa kumiliki mashamba (Hes 18:23-24; Kumb 10:9).; #4:36 Kisiwa kimoja katika bahari ya Mediteranea ambapo kulikuwa na jumuiya maarufu ya Wayahudi (angalia Mate 11:19).; #4:36 Au: neno kwa neno ni “mwana wa faraja” msemo wa Kisemiti wenye maana ya mtu ambaye (Mate 11:23).]
37Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.