The chat will start when you send the first message.
1Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo mita ishirini na nane na upana mita tatu. Aliisimamisha katika sehemu tambarare ya Dura, mkoani Babuloni.[#3:1 Au: sanamu iliyopakwa dhahabu na sio sanamu yote ya dhahabu tupu. Sanamu hiyo henda hapo awali iliwakilisha mungu wa Wababuloni aitwaye “Beli”.; #3:1 Haijulikani mahali au mji huo ulikuwa wapi lakini huenda ulikuwa kusini mwa mji wa Babuloni (taz 4:28-31). Maana ya jina hilo ni “ngome”.]
2Kisha mfalme akaamuru maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na maofisa wote wa mikoa wahudhurie sherehe ya kuzindua rasmi sanamu aliyoisimamisha.
3Basi, maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na maofisa wote wa mikoa wakakusanyika tayari kwa uzinduzi wa sanamu aliyosimamisha mfalme Nebukadneza.
4Mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote, mnaamriwa kwamba[#3:4 Namna ya mtindo kawaida uliotumika kwa ajili ya kutoa ilani au tangazo rasmi na ambao ulilipa tangazo lenyewe umaarufu wake. Taz Dan 3:29; 4:1; 5:19; 7:14; Esta 1:22; 8:9; Ufu 5:9; 7:9.]
5mkisikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, lazima mwiname chini na kuiabudu sanamu ya dhahabu aliyosimamisha mfalme Nebukadneza.[#3:5 Ala za muziki, kama vile ngoma n.k., zilikuwa sehemu moja muhimu katika shehere na sikukuu za kidini katika utamaduni wa wakati huo na hata katika nchi zetu.]
6Na yeyote ambaye hatainama chini na kuiabudu, atatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali.”[#3:6 Amri hiyo ya kuiabudu ile sanamu ilimtia Danieli na wenzake katika hali ngumu kwa vile sheria yao ilitamka dhahiri: “Usiabudu miungu wengine isipokuwa mimi” (Kut 20:2-17).]
7Kwa hiyo, watu wote, mara waliposikia sauti za baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, walianguka kifudifudi na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo mfalme Nebukadneza aliisimamisha.
8Wakati huo, baadhi ya Wakaldayo wakajitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Walimwambia mfalme Nebukadneza,
9“Uishi, ee mfalme!
10Wewe, ee mfalme, ulitoa amri kuwa kila mtu anaposikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na kila aina ya muziki, ainame chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu.
11Na kwamba mtu yeyote asiyeinama chini na kuiabudu sanamu hiyo, atupwe ndani ya tanuri ya moto mkali.
12Sasa, kuna Wayahudi fulani uliowateua kushughulikia mambo ya utawala wa mkoa wa Babuloni, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego; watu hawa, ee mfalme, hawakuitii amri yako. Wanakataa kuitumikia miungu yako na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
13Hapo mfalme Nebukadneza, huku akiwaka hasira, akaamuru Shadraki, Meshaki na Abednego waletwe mbele yake. Nao wakawaleta mbele ya mfalme.
14Mfalme Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba wewe Shadraki, wewe Meshaki na wewe Abednego, hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?
15Basi, mtakaposikia tena sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, je, mko tayari kuinama chini na kuiabudu sanamu niliyotengeneza? Kama mkikataa, mtatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali. Je, ni mungu gani anayeweza kuwaokoa mikononi mwangu?”
16Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, sisi hatuhitaji kukujibu kuhusu jambo hilo.
17Ikiwa ndivyo, Mungu wetu ambaye tunamtumikia aweza kutuokoa katika tanuri ya moto mkali; tena atatuokoa mikononi mwako, ee mfalme.[#3:17 Tamko hili ni wazo muhimu sana katika kitabu cha Danieli. Taz pia Dan 6:16,26-27; 12:1-2.]
18Lakini, hata kama haitafanyika hivyo, ujue wazi, ee mfalme, kwamba sisi hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyosimamisha.”
19Hapo, mfalme Nebukadneza akawaka hasira, sura yake ikabadilika kwa chuki dhidi ya Shadraki, Meshaki na Abednego. Akaamuru mwako wa moto wa tanuri uongezwe mara saba kuliko kawaida yake.
20Akaamuru watu fulani wenye nguvu kabisa katika jeshi lake wawafunge Shadraki, Meshaki na Abednego na kuwatupa katika ile tanuri ya moto mkali.
21Basi, vijana hao wakafungwa hali wamevaa makoti yao, kanzu zao, kofia na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuri ya moto mkali.
22Kwa vile amri ya mfalme ilikuwa kali, ule moto ulikuwa umewashwa ukawa mkali sana, hata ndimi za moto zikawateketeza wale watu waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego.
23Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego, wakiwa wamefungwa, wakatumbukia katika ile tanuri ya moto mkali.[#3:23 Katika tafsiri ya Kigiriki ya Septuaginta (LXX), baada ya aya hii na kabla ya 3:24 kuna nyongeza (katika toleo hili imechapishwa kwa italiki) inayohusu kwanza “Sala ya Azaria” na pili “Wimbo wa Vijana Watatu” na ambayo haipo katika Biblia ya Kiebrania.]
24Basi, mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hatukuwafunga watu watatu na kuwatupa motoni?” Nao wakamjibu mfalme, “Naam, mfalme! Ndivyo!”
25Kisha akauliza, “Lakini sasa mbona ninaona watu wanne wakitembeatembea humo motoni bila kufungwa na wala hawadhuriki, na mtu wa nne anaonekana kama mwana wa miungu?”[#3:25 Au: “mtu wa nne … kama malaika” (taz aya 28 ambapo Nebukadneza anamwita mtu huyo huyo “malaika”).]
26Basi, mfalme Nebukadneza akaukaribia mlango wa tanuri ya moto mkali, akaita, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Mkuu, tokeni mje hapa!” Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka motoni.[#3:26 Nebukadneza anatumia jina hili hapa kumtaja Mungu wa Danieli, jina la sifa ambalo katika Biblia lilitumiwa siyo tu na Waisraeli bali pia na watu wa mataifa mengine. Katika Mwa 14:22 Abrahamu analitumia jina hili kwa Mwenyezi-Mungu. Taz pia Hes 24:16; Kumb 32:8; Zab 46:4; Mate 16:17.]
27Maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa na washauri wa mfalme, wote wakakusanyika pamoja, wakaona ya kuwa ule moto haukuweza kuwaunguza hao watatu. Nywele zao hazikuungua, mavazi yao hayakuungua, wala hawakuwa na harufu yoyote ya moto.
28Basi, mfalme Nebukadneza akasema, “Na asifiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego kwa kuwa alimtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake ambao wanamtegemea. Wao walikataa kutii amri yangu ya kifalme, wakaitoa mhanga miili yao badala ya kuabudu mungu mwingine, ila Mungu wao peke yake.[#3:28 Taz 3:25 maelezo. Jina malaika katika Kiebrania lina maana ya “mjumbe”. Katika Biblia malaika wanaonekana kuwa wajumbe na pia watumishi wa Mungu.]
29Kwa hiyo, naamuru kwamba watu wa kabila lolote, taifa lolote au lugha yoyote, watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, watang'olewa viungo vyao kimojakimoja na nyumba zao zitabomolewa. Maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”
30Basi, mfalme Nebukadneza akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika mkoa wa Babuloni.