The chat will start when you send the first message.
1“Adhimisheni mwezi wa Abibu na kufanya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Maana katika mwezi huo wa Abibu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliwatoa Misri wakati wa usiku.[#16:1-17 Bado tupo katika sehemu ile ya kati (12:2—16:17) ambayo inashughulikia uhusiano kati ya watu wa Mungu na Mungu mwenyewe. Hapa katika 16:1-17 tuna maagizo ya kufanya kuhusu sikukuu tatu kubwa za mwaka: sikukuu ya Pasaka ambayo inaendelezwa na sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu (16:1-7), sikukuu ya mavuno (16:9-12) na sikukuu ya vibanda (16:13-17). Ni wakati ambapo watu wa Israeli (wanaume) walitakiwa kwenda mbele ya Mwenyezi-Mungu na zawadi zao (aya 16).; #16:1 Mwezi huo uliitwa pia Nisani (kuanzia katikati ya mwezi Machi mpaka katikati ya mwezi Aprili katika kalenda yetu). Huo ulikuwa mwezi wa kwanza katika Kalenda ya Kiebrania. Sherehe ya Pasaka inahusiana na neno la Kiebrania ambalo linatafsiriwa kwa “kupita” au “kuruka” katika Kut12:1-20,23,27. Sikukuu hiyo ya Pasaka ilikuwa hasa ya kukumbuka wakati Mungu alipowatoa Waisraeli utumwani kule Misri (Kut 12:2), nayo iliadhimishwa siku ya 14 mwezi ya wa kwanza, kuanzia jioni ya tarehe 13. Nayo sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu ilianza baada ya sikukuu hiyo ya Pasaka.]
2Mtatoa sadaka ya Pasaka kutoka mifugo yenu ya kondoo au ng'ombe kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu atachagua likae jina lake.
3Msile sadaka hiyo na mikate iliyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso — kwa sababu mlitoka Misri kwa haraka; kwa hiyo, muda wote mtakaoishi mtakumbuka ile siku mlipotoka Misri.[#16:3 Taz 16:16 ambapo muda huo unaitwa sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu. Mikate hiyo ilikuwa myembamba, mithili ya chapati. Iliwakumbusha Waisraeli kwamba wakati ule walipotoka Misri waliondoka kwa haraka na haukuwako muda wa kutengeneza chachu na kuiweka katika unga wa kukanda ili uumuke. Kwa hiyo walikula mikate myembamba ambayo haikuwa imetiwa chachu.]
4Kwa muda wa siku saba mtu yeyote katika nchi yenu asiweke chachu nyumbani mwake; na nyama ya yule mnyama aliyechinjwa jioni ya siku ya kwanza isibaki mpaka asubuhi.
5Msitolee sadaka ya Pasaka katika mji wowote ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa,
6bali mtaitolea pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atapachagua likae jina lake, hapo ndipo mtakapotolea sadaka ya Pasaka jioni, jua linapotua, wakati uleule mlipotoka Misri.
7Hiyo nyama mtaichemsha na kuila mahali pale Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atakapochagua; asubuhi yake mtageuka na kurudi mahemani mwenu.
8Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu; na mnamo siku ya saba utakuwapo mkutano mkubwa wa kumwabudu Mwenyezi-Mungu, na msifanye kazi yoyote siku hiyo.
9“Mtahesabu majuma saba; mtaanza kuyahesabu tangu mnapoanza kuvuna nafaka.
10Halafu mtaadhimisha sikukuu ya majuma kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kutoa sadaka ya hiari, mtakayotoa kadiri awabarikiavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.[#16:10-11 Au, “Sikukuu ya Mavuno”. Sikukuu hii iliadhimishwa wakati wa mavuno ya mwaka ya nafaka. Wakati huo ulikuwa wakati wa shukrani kwa Mungu na walimtolea zawadi kutoka mavuno yao (Lawi 23:15-21; Hes 28:26-31). Katika A.J. ilijulikana kama “Pentekoste”.]
11Mtafurahia mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi pamoja na wana wenu na binti zenu, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi pamoja nanyi. Fanyeni haya katika mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapochagua likae jina lake.
12Mkumbuke kuwa mlikuwa watumwa kule Misri; basi muwe waangalifu kufuata masharti haya.
13“Baada ya kupura nafaka yenu yote na kukamua zabibu zenu, adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa muda wa siku saba.[#16:13 Taz Hes 29:12-38. Katika Lawi 23:33-36 tunaambiwa kwamba sikukuu hiyo ilitakiwa ifanywe siku ya 15 ya mwezi wa saba katika kalenda ya Kiebrania ambayo kadiri ya kalenda yetu ni mwanzoni mwa mwezi Oktoba. Wakati wa sikukuu hiyo watu walitengeneza vibanda vya dharura kwa matawi na kukaa humo. Hiyo iliwakumbusha kuishi kwa wazee wao kule jangwani baada ya kutoka Misri.]
14Mtafanya sherehe hiyo, nyinyi na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao huishi katika miji yenu.
15Kwa siku saba mtamfanyia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, sherehe mahali ambapo Mwenyezi-Mungu atapachagua; kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki kwa mazao yenu yote na katika shughuli zenu zote nanyi hakika mtafurahi.
16“Wanaume wote wa taifa lenu watakuja mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mara tatu kila mwaka, mahali atakapopachagua: wakati wa sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, sikukuu ya kuvuna majuma na wakati wa sikukuu ya vibanda. Wasiende mbele ya Mwenyezi-Mungu mikono mitupu.
17Wote watatoa kadiri wanavyoweza kulingana na baraka Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alizowajalia.
18“Mtateua waamuzi na maofisa kutoka makabila yenu katika miji yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa, nao watatoa hukumu za haki kwa watu.[#16:18—18:22 Katika sehemu hii, miongoni mwa mengine, kuna maagizo kuhusu watu ambao walikuwa na madaraka juu ya watu wa Israeli kama vile mahakimu (16:18—17:13), wafalme (17:14-20), Walawi (18:1-8) na manabii (18:9-22). Baadhi ya hayo mengine ni maagizo kuhusu ibada na umuhimu wa kupiga vita desturi za kuabudu miungu ya uongo na hasa ibada kwa nyota (17:3).; #16:18 Katika Kut 18:13-27; Kumb 1:9-17 tulipewa habari juu ya kuteuliwa kwa waamuzi. Hapa mwandishi anatoa hasa sifa zao: wawe wasiopendelea, waaminifu na wasiopenda kuhongwa (taz pia Kut 23:6-8). Tofauti na mitindo ya utawala katika mataifa mengine, mtindo wa utawala katika Israeli ulitakiwa kuongozwa na sheria ya Mungu na hivyo mara nyingi suala lilikuwa kwamba uamuzi umeambatana na matakwa ya Mungu au la (aya 20). Taz pia 10:18-19.]
19Msipotoshe haki; msiwe na upendeleo, wala msikubali kupokea rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya watu wenye hekima na kupotosha kesi ya mtu mwadilifu.
20Mtazingatia haki tu, ili mpate kuishi na kuimiliki nchi mnayopewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
21“Msipande mti wowote uwe nguzo ya mungu wa uongo karibu na meza ya madhabahu sadaka mtakayomjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
22Wala msisimamishe nguzo ambayo Mwenyezi-Mungu Mungu wako anaichukia.[#16:21 Ilikatazwa kusimika nguzo au madhabahu kwa heshima ya miungu mingine mahali pale alipochagua Mwenyezi-Mungu kuabudiwa. Katika Kut 34:13 Waisraeli walitakiwa kuvunjilia mbali madhabahu na nguzo za aina hiyo.]