The chat will start when you send the first message.
1“Msimtolee Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, sadaka ya ng'ombe au kondoo mwenye dosari, wala ubaya wowote, maana hilo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.[#17:1 Kila mnyama aliyetolewa kuwa kafara kwa Mwenyezi-Mungu alitakiwa kuwa mzima, asiye na kasoro yoyote (Kut 12:4-5; Lawi 22:20-25).]
2“Kama mkisikia kwamba katika mmoja wa miji yenu kuna mwanamume au mwanamke atendaye maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuvunja agano lake,
3naye amekwenda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, akaabudu hata jua, mwezi au vitu vingine vya mbinguni ambavyo sikuagiza viabudiwe,[#17:2-3 Watu wengine walifikiri kwamba nyota na sayari nyingine zilikuwa miungu na kuziabudu. Taz pia Kut 22:20.]
4nanyi mkaambiwa hayo na mkaisikia taarifa hiyo, mtafanya uchunguzi kamili, na kama ni kweli na ni hakika kuwa kitu hiki kiovu kimefanywa katika Israeli,
5basi, mtoeni mtu huyo nje ya miji na kumpiga mawe mpaka afe.
6Hata hivyo, atauawa ikiwa kuna ushahidi wa watu wawili au watatu. Asiuawe ikiwa kuna ushahidi wa mtu mmoja tu.[#17:6 Taz Hes 35:30; Mat 18:15; 2Kor 13:1. Kipengele hiki kilikuwa na lengo la kuepa kuuawa kwa mtu asiye na hatia. Kwa sababu hiyo hiyo, shahidi wa kwanza alitakiwa awe wa kwanza kumtupia mawe huyo mtu aliyehukumiwa kuuawa.]
7Wale mashahidi ndio watakaoanza kumpiga mawe kwanza, halafu wengine nao wampige mawe. Ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu.
8Inawezekana kukatokea mashtaka mengine yaliyo magumu mijini mwenu, kama vile kesi zihusuzo: unajisi, mambo ya haki za watu, na madhara ya mwili. Ikitokea hivyo, mtaondoka na kwenda mahali alipopachagua Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,[#17:8-13 Kesi au mashtaka mengine yaliyokuwa magumu zaidi kwa hao waamuzi na maofisa yalitakiwa kupelekwa katika mahakama iliyokuwa mahali pa ibada. Mwenyezi-Mungu alichagua mahali hapo, hakimu na makuhani Walawi ambao walikuwa na jukumu la kufundisha na kufanua sheria yake. Uamuzi utakaotolewa katika mahakama hiyo ulichukuliwa kuwa ndio kauli ya Mungu mwenyewe.]
9na huko mtawaendea makuhani Walawi, na mwamuzi aliye kazini wakati huo, nanyi mtatoa mashtaka mbele yao, nao watatoa uamuzi wao.
10Kisha mtafanya kama watakavyowatangazieni pale mahali Bwana atakapopachagua; mtakuwa waangalifu kufanya yote kama watakavyowaagiza.
11Itawabidi kufanya kufuatana na maongozi watakayowapatia na uamuzi watakaoutoa kwenu. Msiache kutimiza kwa dhati hukumu watakayowatangazia.
12Naye mtu asiyejali kumtii kuhani au mwamuzi aliyewekwa hapo kumhudumia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, au mwamuzi, mtu huyo atauawa. Ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu.
13Watu wote watasikia na kuogopa wasifanye tena kitu kwa kutojali.
14“Mtakapokwisha ingia katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni, mkaimiliki na kukaa humo, nanyi mkasema, ‘Tutaweka mfalme juu yetu, kama mataifa yote yanayotuzunguka;’
15mwaweza kumweka mfalme juu yenu mtu ambaye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atamchagua. Mtamweka mmojawapo wa ndugu zenu kuwa mfalme juu yenu. Msimfanye mgeni asiye ndugu yenu kuwa mfalme wenu.
16Hata hivyo, asiwe na farasi wengi kwa ajili yake mwenyewe, wala asiwarudishe watu Misri ili kujipatia farasi zaidi, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amewaonya, ‘Kamwe msirudi huko tena’.
17Wala asijipatie wake wengi, la sivyo moyo wake utaasi; wala asijipatie fedha na dhahabu kwa wingi mno.[#17:17 Wafalme wengi walikuwa na wake wengi, wengine wao wakiwa kutoka mataifa mengine ambayo yaliabudu miungu yao na sio Mwenyezi-Mungu. Tukio kama lile linalotajwa katika 1Fal 11:1-13 (Solomoni) ni kielelezo wazi cha hatari zilizokuwako.]
18Atakapokuwa amekalia kiti cha ufalme lazima afanye nakala ya sheria hii iandikwe mbele ya makuhani wa Kilawi.[#17:18 Tafsiri ya Septuajinta (LXX) hapa ina “Sheria ya Pili” (Deuteronomion) jambo ambalo wataalamu wa Biblia wanafikiri lilikuwa chanzo cha jina la kitabu hiki. Agizo hili linaonesha dhahiri umuhimu wa kufuata sheria ya Mungu kwa upande wa mfalme wa watu wa Israeli.]
19Nakala hiyo atakuwa nayo daima na kuisoma maisha yake yote, ili apate kujifunza kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akishika na kutimiza maneno yote ya sheria hii na masharti haya,
20bila kujikuza mwenyewe juu ya ndugu zake, wala kuiweka kando amri hii kwa namna yoyote, ili aweze kudumu katika utawala, yeye na wazawa wake katika Israeli.