Kumbukumbu la Sheria 18

Fungu la makuhani

1“Makuhani Walawi, yaani kabila lote la Lawi wasiwe na sehemu wala urithi katika Israeli. Wao watakula sehemu ya sadaka za Mwenyezi-Mungu.

2Wala wasiwe na urithi kati ya ndugu zao; Mwenyezi-Mungu ndiye urithi wao kama alivyoahidi.

3“Na hii itakuwa haki ya makuhani kutoka kwa watu wanaotoa sadaka iwe ni ng'ombe au kondoo: watampa kuhani mguu wa mbele, mashavu na matumbo.

4Mtawapa sehemu ya kwanza ya mazao yenu ya nafaka, divai, mafuta yenu na sufu ya kwanza ya kondoo wenu.

5Katika makabila yenu yote, Mwenyezi-Mungu amechagua kabila la Walawi limtumikie kama makuhani milele.

6“Ikiwa Mlawi yeyote atapenda mwenyewe anaweza kutoka mji wowote ule wa Israeli kwenda pale mahali Mwenyezi-Mungu alipochagua,

7na hapo anaweza kuhudumu kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama wale Walawi wengine wanaohudumu mbele ya Mwenyezi-Mungu.

8Watapata mafungu yao sawa ya kula, ingawa wanayo mapato kutokana na mauzo ya mali za jamaa zao.

Onyo dhidi ya desturi ngeni

9“Mtakapofika katika ile nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawapa, msifuate desturi za kuchukiza za mataifa hayo.[#18:9 Tabia zilizokuwa za mataifa mengine zilikuwa kinyume cha matakwa ya Mwenyezi-Mungu. Taz pia Lawi 18:26; Kumb 12:29.]

10Pasiwe mtu yeyote miongoni mwenu atakayemtambika mtoto wake wa kiume au wa kike kwa moto, wala mtu apigaye ramli, wala mwaguzi, wala mpiga bao,[#18:10 Hiyo ilikuwa desturi mbaya sana ambayo ilifanywa na mataifa mengine kuitambikia miungu yao. Mara nyingi tambiko za namna hiyo zilifanyiwa Moleki, mungu wa Wamoabu (taz Lawi 18:21, 28; 20:2; taz pia Kumb 12:29-31; 18:10). Ahazi aliiga desturi hiyo mbaya (taz 2Fal 16:3). Manase aliiga pia desturi hiyo mbaya (taz 2Fal 21:6; 2Nya 33:6). Taz pia 12:31 maelezo.]

11wala mchawi, wala mlozi, wala mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo au kutoka kwa wafu.

12Maana yeyote atendaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; na kwa ajili ya mambo haya ya kuchukiza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawafukuza watu wa namna hiyo mbele yenu.

13Muwe wakamilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Ahadi ya kupewa nabii

14“Mataifa haya ambayo mtaimiliki nchi yao hufuata maongozi ya waaguzi na wapiga ramli; lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu hawaruhusu nyinyi kufanya hivyo.

15“Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawateulieni nabii aliye kama mimi kutoka miongoni mwenu, nanyi mtamsikiliza huyo.[#18:15 Manabii (na sio watu wenye kutumia mizimu au kupiga bao) ndio watakaopewa jukumu la kuendeleza wadhifa wa Mose (Kut 33:11; Hes 12:6-8; Kumb 34:10) na kuwajulisha watu matakwa ya Mwenyezi-Mungu. Rejea Yer 7:25.]

16Hicho ndicho mlichomwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kule Horebu, siku ile mlipokusanyika na kusema, ‘Tusisikie tena sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala tusiuone tena moto huu mkubwa, tusije tukafa!’

17Naye Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Wamesema ukweli.

18Nitawateulia miongoni mwa ndugu zao wenyewe nabii kama wewe; nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.

19Yeyote ambaye hatasikia maneno atakayosema nabii huyo kwa jina langu, mimi mwenyewe nitamwadhibu.

20Lakini nabii yeyote atakayesema kwa jina la miungu mingine, au atakayejaribu kusema neno kwa jina langu hali mimi sikumwambia aseme, huyo nabii atakufa.’

21“Lakini nyinyi mwaweza kusema, ‘Tutawezaje kutambua neno ambalo Mwenyezi-Mungu hakulisema?’

22Kama nabii akisema kitu ati kwa jina la Mwenyezi-Mungu, na kitu hicho hakifanyiki au hakiwi kweli, jambo hilo hakulisema Mwenyezi-Mungu; nabii amelisema kwa ufidhuli, nanyi msitishwe na jambo hilo.[#18:22 Hapa njia mbili zinatajwa za kutambulisha nabii wa kweli na nabii wa uongo: Kwanza, yeyote anayesema kwa jina la mungu mwingine, huyo si nabii wa kweli wala hakutumwa na Mungu; pili, kama kitu anachotabiri kikifanyika, huyo nabii atakuwa amesema kwa niaba ya Mungu (taz Yer 28:9).]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania