Kumbukumbu la Sheria 23

Kutengwa na watu wa Mungu

1“Mwanamume yeyote aliyehasiwa au aliyekatwa uume wake haruhusiwi kujiunga na kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu.

2“Na mwana haramu yeyote, wala mzawa wake hata kizazi cha kumi, haruhusiwi kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu.

3“Mwamoni au Mmoabu yeyote, wazawa wao wote hata kizazi cha kumi, hawaruhusiwi kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu,

4kwa sababu walikataa kuwapatia chakula na maji mlipokuwa njiani kutoka Misri, na kwa kuwa walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori kule Mesopotamia, awalaani.

5Lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, hakumsikiliza Balaamu; badala yake laana hiyo iligeuka kuwa baraka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwapenda.

6Kwa hiyo, kamwe msiwasaidie hao wapate amani na fanaka.

7“Msiwachukie Waedomu; hao ni ndugu zenu. Na msiwachukie Wamisri, kwani mlikaa katika nchi yao kama wageni.[#23:3-7 Habari zinazotolewa hapa hazipatani kwa kila jambo na habari zinazojatwa mahali pengine katika Biblia. Moabu ilimwalika Balaamu kumlaani Israeli (Hes 22:1-6) lakini katika tukio hilo Amoni halisemwi kwamaba lilihusika. Inawezekana kwamba hapa Waamoni na Wamoabu hawaruhusiwi kujiunga na kusanyiko la watu wa Mungu kwa vile ni wazawa wa Loti na binti zake (Mwa 19:20-28). Lakini Waedomu ambao walikataa kuwaruhusu Waisraeli kupita katika nchi yao, wao hawakatazwi kwa sababu ni jamaa za Waisraeli kwa babu yao Esau. Nao Wamisri wanakubaliwa kwa vile walimsaidia Yosefu na jamaa yake (Mwa 46:1—47:26).]

8Wazawa wao, kuanzia kizazi cha tatu, wataruhusiwa kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu.

Usafi kambini

9“Mkienda vitani, mkapiga kambi, kila mmoja ajihadhari na kitu chochote kiovu.

10Kama miongoni mwenu kuna mtu yeyote ambaye ni najisi kwa sababu ya kutokwa mbegu usiku, huyo atatoka nje ya kambi; hatakaa karibu na kambi.

11Lakini ikifika jioni ataoga, na jua likitua anaweza kurudi kambini.

12“Lazima muwe na mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda haja.

13Kati ya vifaa vyenu mtakuwa na jembe, na hilo mtatumia kuchimba shimo na kufukia kinyesi chenu.

14Kambi yenu lazima iwe takatifu kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anatembea kambini mwenu ili awaokoe na kuwatia adui zenu mikononi mwenu. Kwa hiyo msimwache aone kitu chochote kisichofaa miongoni mwenu, la sivyo atawaacheni.

15“Mtumwa akikimbilia kwako usimrudishe kwa bwana wake.

16Ataishi pamoja nawe mahali atakapochagua katika mojawapo ya makao yako, mahali panapompendeza. Usimdhulumu.

17“Mwisraeli yeyote, mwanamume au mwanamke, haruhusiwi kamwe kuwa kahaba wa kidini.[#23:17 Hapa mwandishi anadokezea desturi ya ukahaba uliofanyika katika ibada za miungu, ukahaba ambao ulienea miongoni mwa watu wa Mashariki ya Kati ya Kale na ambao ulihusika na ibada za kupata rutuba kwa mashamba na mifugo. Taz Lawi 19:29; 1Fal 14:24; 15:12; 22:47.]

18Fedha yoyote iliyopatikana kwa vitendo vya ukahaba huo, isipelekwe hekaluni kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kulipia nadhiri, maana mwanamume au mwanamke aliye kahaba wa kidini ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu.

19“Usimkopeshe ndugu yako Mwisraeli kitu kwa riba; usimtoze riba juu ya mkopo wa fedha, chakula, au chochote ambacho watu hukopesha kwa riba.[#23:19 Hapo kale watu hawakuwa na sarafu za pesa wala noti. Ununuaji wa vitu ulifanyika kwa kutumia dhahabu au madini ya fedha. Gharama ya kukopa dhahabu au fedha iliitwa riba. Waisraeli walikatazwa kuwatoza riba Waisraeli wenzao lakini waliweza kuwatoza riba wageni.]

20Unaweza kutoza riba unapomkopesha mgeni, lakini ndugu yako Mwisraeli usimtoze riba, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atakubariki katika shughuli zako zote utakazofanya katika nchi ambayo unakwenda kuimiliki.

21Unapoweka nadhiri kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, usichelewe kuitekeleza, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wako ataidai kwako, nawe utakuwa na kosa.[#23:21 Nadhiri ilithamaniwa sana katika Israeli. Nadhiri, yaani ahadi rasmi kwa Mungu, ikishafanywa ilikuwa ni lazima itimizwe. Taz pia Hes 30:1-6; Mat 5:33.]

22Lakini ukiacha kuweka nadhiri hutakuwa na dhambi.[#23:22 Hakuna mahali ambapo panasema kuwa mtu lazima aweke nadhiri, isipokuwa mtu akiweka nadhiri hapo anapata maongozi na maonyo (taz aya ya 21 maelezo).]

23Uwe mwangalifu kutimiza nadhiri uliyotamka kwa mdomo wako, maana ulimwahidi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, kwa hiari yako.

24“Ukipitia katika shamba la mzabibu la jirani yako unaweza kula zabibu kadiri uwezavyo, lakini usichume na kuchukua zabibu zozote kikapuni mwako.

25Ukipitia katika shamba la jirani yako lenye nafaka unaweza kukwanyua masuke kwa mkono na kula, lakini usichukue mundu kukata mazao yake.[#23:24-25 Nafaka zilizolimwa huko Palestina wakati huo zilikuwa ngano, shayiri na mawele. Palestina ilisifika pia kwa mizabibu yake. Sheria hii iliruhusu mtu mwenye njaa kuchuma na kula papo hapo; na wala si kupeleka nyumbani maana kufanya hivyo ni kuiba.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania