Kumbukumbu la Sheria 5

Kumbukumbu la Sheria 5

Amri kumi

(Kut 20:1-17)

1Mose aliwaita pamoja Waisraeli, akawaambia: “Enyi Waisraeli, sikilizeni masharti na maagizo ambayo ninayatamka mbele yenu leo. Jifunzeni hayo na kuyatekeleza kwa uangalifu.[#5:1 Hotuba ya pili ya Mose inahusu sehemu kubwa ya kitabu hiki, yaani sura 5—26, na yenyewe inatanguliwa na maneno ya kutia moyo au kuwahimiza Waisraeli washike kwa makini agano au amri za Mungu (aya 5-11). Katika aya 2-3 inaonekana kwamba agano hilo lilikuwa pia kwa ajili ya vizazi vyote (taz pia 4:5-8).]

2Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alifanya agano nasi mlimani Horebu.

3Hakufanya agano hilo na wazee wetu tu, bali alifanya na sisi sote ambao tuko hai hivi leo.

4Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi ana kwa ana huko mlimani katikati ya moto.

5Wakati huo mimi nilisimama kati yenu na Mwenyezi-Mungu, nikawatangazieni yale aliyoyasema, kwa kuwa nyinyi mliogopa ule moto na hamkupanda mlimani. Mwenyezi-Mungu alisema hivi,

6“‘Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri, ambako ulikuwa mtumwa.[#5:6-21 Sehemu hii ya Amri Kumi inapatikana pia katika Kut 20:1-17 ingawaje kuna tofauti kadha wa kadha (taz Kut 20:1-17 maelezo). Jambo la maana ni umuhimu wake. Muundo wake unafanana na miundo ya mikataba kati ya mtawala na mtawaliwa kama ilivyofanyika katika Mashariki ya Kati ya Kale. Mtawala aliahidi kuwalinda watawaliwa nao wakaahidi kuwa waaminifu kwa kushika masharti ya agano au mkataba. Amri hizo zinaanza kwa kitambulisho cha Mwenyezi-Mungu: “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri, ambako ulikuwa mtumwa” (aya 6; Kut 20:2). Amri zinazofuata zilikuwa na shabaha ya kuimarisha ule uhusiano ambao Mungu aliuweka kati yake na watu wake.]

7“‘Usiwe na miungu mingine ila mimi.

8“‘Usijifanyie sanamu za miungu za kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.[#5:8 Watu wa kale walifikiri dunia ilikuwa imekalishwa juu ya minara ambayo ilikuwa na msingi wake katika vilindi vya bahari kuu mno. Taz Zab 18:15; 24:2; 104:5.]

9“‘Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu. Nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wale wanichukiao.[#5:9 Taz 4:24 maelezo.]

10Lakini nawafadhili maelfu ya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.

11“‘Usilitaje bure jina langu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; maana mimi ni Mwenyezi-Mungu sitaacha kumwadhibu yeyote afanyaye hivyo.

12Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka wakfu, kama mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nilivyokuamuru.

13Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote,

14lakini siku ya saba ni siku ya Sabato ambayo imetengwa kwa ajili yangu. Siku hiyo wewe usifanye kazi yoyote, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika vilevile kama wewe.

15Usisahau kwamba wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, nami Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nikakutoa huko kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyoshwa; ndiyo maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako nimekuamuru kuiadhimisha siku ya Sabato.[#5:15 Hapa, sababu za kuadhimisha siku ya Sabato ni tofauti na Kut 20:11 na sababu hii ni kawaida katika kitabu hiki. Taz 15:15; 16:12; 24:18,22.]

16“‘Waheshimu baba yako na mama yako, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako nilivyokuamuru; fanya hivyo ili uishi siku nyingi na kufanikiwa katika nchi ambayo ninakupatia.

17“‘Usiue.

18“‘Usizini.

19“‘Usiibe.[#5:19 Lawi 19:11; Mat 19:18; Marko 10:19; Luka 18:20. “Kuiba” kunajumuisha pia “kumwiba” mtu na pia “kumuuza mtu utumwani” (Kut 24:7).]

20“‘Usimshuhudie jirani yako uongo.

21“‘Usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba yake, wala shamba lake, wala mtumwa wake wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kitu chochote alicho nacho jirani yako.’[#5:21 Rom 7:7; 13:9. Linganisha orodha hii na ile ya Kut 20:17.]

22“Hizi ndizo amri Mwenyezi-Mungu alizowaambieni nyote kwa sauti kubwa kutoka katika moto na lile wingu zito na giza nene. Aliwaambieni mlipokuwa mmekusanyika kule mlimani na hakuongeza hapo amri nyingine. Kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe, akanipatia.

Mose msemaji wa Mungu

(Kut 20:18-21)

23“Wakati mliposikia hiyo sauti kutoka katikati ya lile giza, juu ya ule mlima uliokuwa unawaka moto, viongozi wote wa makabila yenu na wazee walinijia

24wakasema, ‘Sikiliza! Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametufunulia utukufu na ukuu wake; tumeisikia sauti yake kutoka katikati ya ule moto. Leo hivi tumemwona Mungu akiongea na binadamu, naye binadamu badala ya kufa akaendelea kuishi![#5:24 Utukufu ni neno linaloeleza mng'ao wa uzito au ukuu na uwezo wa Mwenyezi-Mungu ukidhihirishwa katika wingu na moto. Taz Kut 24:17.]

25Lakini ya nini kujitia katika hatari ya kufa kwa kuteketezwa na ule moto mkubwa? Tukiisikia tena sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, tutakufa!

26Je, ni binadamu gani aliyepata kumsikia Mungu aliye hai akiongea kutoka katikati ya moto kama tulivyomsikia sisi halafu akaweza kubaki hai?

27Heri wewe Mose uende karibu, ukasikilize yote atakayosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kisha uje kutuambia mambo hayo yote atakayokuambia. Sisi tutayasikiliza na kuyatekeleza’.

28“Mwenyezi-Mungu alisikia maneno yenu hayo, akaniambia ‘Nimesikia maneno waliyokuambia watu hawa; yote waliyosema ni sawa.

29Laiti wangekuwa daima na mawazo kama haya wakaniheshimu na kushika amri zangu! Mambo yao yote yangewaendea vyema daima wao wenyewe na wazawa wao milele.

30Nenda ukawaambie warudi mahemani mwao.

31Lakini wewe Mose usimame hapa karibu nami; mimi nitakuambia amri zote na masharti na maagizo ambayo utawafundisha, ili nchi ambayo ninawapa iwe mali yao.’

32“Nyinyi muwe waangalifu mkafanye kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru; tekelezeni kila kitu barabara.

33Mtafuata njia yote Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyowaamuru kufuata ili mambo yenu yawaendee vyema na mpate kuishi muda mrefu katika nchi mtakayotwaa iwe mali yenu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania