The chat will start when you send the first message.
1Haya ndiyo majina ya watoto wa kiume wa Israeli, ambao walikwenda Misri, kila mmoja na jamaa yake:[#1:1 Kitabu cha Kutoka kinaendelea pale simulizi la Mwanzo lilopoishia, jambo ambalo ni dhahiri kwa vile aya 1-5 zinarudia tena habari tunazopewa katika Mwa 46:8-27.; #1:1 Jina lingine la Yakobo (taz Mwa 32:28-29).]
2Reubeni, Simeoni, Lawi, Yuda,
3Isakari, Zebuluni, Benyamini,
4Dani, Naftali, Gadi na Asheri.[#1:2-4 Idadi inayotajwa hapa ni kumi na moja, yaani bila kumhesabu Yosefu ambaye tayari alikuwa kule Misri (taz Mate 7:14).]
5Wazawa wote wa Yakobo walikuwa watu 70. Wakati huo Yosefu alikuwa amekwisha tangulia kukaa huko Misri.[#1:5 Ndivyo ilivyo hapa na katika Mwa 46:27. Tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX), kadhalika na hati moja ya kale ya Kiebrania iliyopatikana kule Kumrani, zina “watu sabini na watano”. Taz pia Mate 7:14 ambapo kama desturi ya A.J. hufuata Septuajinta katika nukuu zake.]
6Baadaye, Yosefu alifariki, hali kadhalika ndugu zake na kizazi kile chote.
7Lakini wazawa wa Israeli waliongezeka sana, wakawa wengi na wenye nguvu mno, wakaenea kila mahali nchini Misri.[#1:7 Kuongezeka kwao kwaweza kuchukuliwa kama kutimia kwa kiasi ile ahadi ya Mwenyezi-Mungu kwa Abrahamu, Isaka na Yakobo (taz Mwa 12:2; 15:5; 17:6-8; 26:4,24; 28:13-14).]
8Basi, akatokea mfalme mwingine huko Misri ambaye hakumjua Yosefu.[#1:8 Huenda huyo alikuwa Farao Ramesesi II (1304-1238 K.K.).; #1:8 Yamkini kwa maana ya kwamba hakuwa na habari za Yosefu au hakujali juu ya mema ya Yosefu kwa Wamisri.]
9Naye akawaambia watu wake, “Tazameni jinsi Waisraeli walivyo wengi na wenye nguvu kuliko sisi.
10Ni lazima tutafute hila ya kuwapunguza na kuzuia wasiongezeke; la sivyo, kama vita vikitokea watajiunga na adui zetu na kuitoroka nchi.”[#1:10 Au: “kuitawala”.]
11Basi, Wamisri wakawateua wanyapara wawasimamie Waisraeli na kuwatesa kwa kazi ngumu. Waisraeli wakafanya kazi ya kumjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi.[#1:11 Jina hili, (Kimisri ni “per-aa”, yaani: “nyumba kubwa”), lilitumika awali kuhusu ikulu ya mtawala. Lakini baadaye likawa ni jina la sifa la kumtaja mtawala wa Misri.; #1:11 Mji ulioko katika bonde kati ya Mto Nili na Ziwa Timsa.; #1:11 Mji huu ulipata jina hilo kutokana na Farao mpya Ramesesi II (taz Mwa 47:11).]
12Lakini kadiri walivyoteswa ndivyo Waisraeli walivyozidi kuongezeka na kuenea nchini. Hivyo Wamisri wakawaogopa sana watu wa Israeli.
13Basi, Wamisri wakawatumikisha Waisraeli kikatili,
14wakayafanya maisha yao kuwa magumu kwa kazi ngumu ya kutengeneza chokaa na kufyatua matofali, na kazi zote za shambani. Katika kazi hizo zote, Waisraeli walitumikishwa kwa ukatili.
15Kisha, mfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Misri, Shifra na Pua, ambao waliwahudumia wanawake wa Kiebrania,[#1:15 Wanawake hawa wawili walikuwa maarufu katika historia ya Waisraeli (taz aya 18,20-21).; #1:15 Taz maelezo ya Mwa 14:13.]
16“Mnapowahudumia wanawake wa Kiebrania wanapojifungua, ikiwa mtoto anayezaliwa ni wa kiume, muueni. Lakini ikiwa ni wa kike, mwacheni aishi.”
17Lakini kwa kuwa wakunga hao walimcha Mungu, hawakufanya kama walivyoamriwa na mfalme wa Misri, bali waliwaacha watoto wa kiume wa Waisraeli waishi.[#1:12-17 Katika aya hizi kuna visa vitatu ambavyo huenda mwandishi aliviweka makusudi kabisa kuonesha tabia yake Mose ambaye ataitwa kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri: Mose ni mtu asiyekubali uonevu (aya 12), asiyekubali mizozo na fujo katika jumuiya (aya 13) na ni mtu anayepinga kukandamizwa kwa wanyonge (aya 17). Mazingira ya kimaandishi ya visa hivyo yanaonesha kwamba Mose ni mtu aliyetayarishwa tayari. Huyu Mose ndiye atakayeitwa kuwaongoza watu kutoka Misri ambako walikuwa wanakandamizwa na kuonewa (3:9).]
18Basi, mfalme wa Misri akawaita wakunga hao, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivyo? Mbona mmewaacha watoto wa kiume waishi?”
19Wao wakamjibu Farao, “Wanawake wa Kiebrania si sawa na wanawake wa Misri. Wao ni hodari; kabla mkunga hajafika, wao huwa wamekwisha jifungua.”
20Basi, Mungu akawajalia mema wakunga hao, nao Waisraeli wakazidi kuongezeka na kuwa na nguvu sana.
21Na kwa vile wakunga hao walimcha Mungu, Mungu akawajalia kupata jamaa zao wenyewe.
22Kisha Farao akawaamuru watu wake wote hivi, “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania mtupeni mtoni Nili. Lakini kila mtoto wa kike, mwacheni aishi.”